HADITHI
KISIWA CHA HARISHI (16)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
“Kaka Masudi ana matatizo sana. Kwanza
hatuelewi ni kitu kilichomfanya amsindikize yule msichana” Shazume akasema.
“Tusiwe na wasiwasi naye sana. Huenda mwenyewe
ameamua kubaki” nikawambia wenzangu.
“Atabakije kule wakati anajua
kuwa lazima Harishi atakuja?” Haji akauliza.
“Kila mtu ana akili yake jamani
tusimuhukumu” nikawambia Shazume na Haji.
“Atajua mwenyewe, shauri
yake” ilikuwa sauti ya kukata tamaa ya
Haji.
Baada ya kujadiliana kwa
kirefu tuliamua kwenda kulala. Kila mtu aliingia kwenye chumba chake.
Unapofika wakati wa kulala
mawazo hubadilika. Fikira zote huondoka na kichwa kujaa mawazo ya Harishi.
Nilikuwa na hakika kuwa
sikuwa mimi peke yangu bali wenzangu wote walikuwa na mawazo kama
yangu. Likini hatukuwa na lolote la kufanya zaidi ya kukubali matokeo
yatakayotokea usiku huo kwa Masudi.
SASA ENDELEA
Usiku ule tulilala na kuamka
salama ingawa tulilala kwa mashaka.
Lakini Masudi hakuwa miongoni
mwetu. Tukadhani kwamba atatokea wakati ule wa asubuhi baada ya kushindwa
kurudi usiku. Lakini tulikaa hadi majira ya saa bila kumuona yeye wala Yasmin.
“Wenzangu mnaonaje twende
tukamuangalie Masudi au tuendelee kumsubiri?” nikawauliza wenzangu.
“Kwenda kumuangalia ni jambo
zuri lakini tunaweza kukutana na Harishi” Haji akasema.
“Nina wasiwasi kwa sababu
Yasmin pia amekaa kimya. Kwa kawaida muda huu angekuwa ameshakuja” nikawambia
wenzangu.
“Hatuwezi kujua lolote
linaweza kuwa limetokea” Shazume naye akasema.
“Basi tusiende, tuendelee
kusubiri hapa hapa hadi atakapokuja Masudi au Yasmin” nikawambia.
Wakati tunaendelea
kujadiliana tulimuona Yasmin akiingia. Sote tukageuka na kumtazama. Kitu
kilichotushitua si tu alikuwa peke yake bali macho yake yalikuwa mekundu
yaliyoonesha alikuwa analia.
Akatusalimia na kutuambia
kuwa amepatwa na fadhaa.
“Kwanini?” akatuuliza.
“Kaka yenu Masudi hakutumia
busara hata kidogo” Masudi alituambia huku akitikisa kichwa kusikitika.
“Kwanini hakutumia busara?”
nikamuuliza huku nikifikiria mengine. Nilifikiria ama Masudi alitaka kumbaka
Yasmin au alimbaka kwani ile hali niliyowakuta nayo usiku uliopita haikuwa ya
kawaida.
“Kama yeye amenipenda mimi kama alivyoniambia mwenyewe ni sawa lakini kitendo
alichokifanya si kizuri kwa sababu anajua mimi nimemilikiwa na Harishi”
Hapo nilijua moja kwa moja
kuwa Masudi amembaka Yasmin na ndio sababu alikuwa analia.
“Kwani amefanya nini?”
nikamuuliza.
“Ungetueleza alichofanya”
Haji naye akamwambia.
“Jana usiku nilimwambia arudi
huku, ulikuwa ni usiku. Lakini alikataa kurudi, akataka kulala na mimi.
Nilimsihi sana
arudi lakini aligoma kabisa, tena alitaka alale na mimi chumba kimoja.
Aliniambia ananipenda” Yasmin akatueleza.
“Masudi ni kaka yetu lakini
ana matatizo sana”
Shazume akadakia.
“Sasa ikawaje?” na mimi
nikauliza kwa pupa.
“Nilimuachia alale. Yule ni
mwanaume nisingeweza kumzuia”
“Ulilala naye chumba kimoja?”
nikamuuliza.
“Nilimuomba sana akalale chumba kingine kwa usalama wake.
Nilimwambia Harishi akija na kukukuta atakuua. Akakubali kwenda kulala chumba
kingine”
“Sasa nini kimetokea?”
Shazume akauliza.
“Harishi alikuja muda ule ule
akamkuta ukumbini anazungukazunguka, akashikwa”
Alipofikia hapo Yasmin
alianza kulia.
“Sasa ameuliwa?’ nikamuuliza.
“Harishi aliacha mtu siku
gani?” Yasmin akaniuliza.
Mimi na Haji na Shazume
tulitazamana tukiwa tumeacha midomo wazi.
“Aliyataka mwenyewe!” Yasmin
akasema.
“Ni kweli aliyataka mwenyewe,
kifo kilikuwa kinamuita” nikamuunga mkono.
“Angekuja kulala na wenzake
pengine angenusurika” Yasmin aliendelea kutuambia.
“Mbona hukuja mapema
kutuambia?” nikamuuliza.
“Harishi ameondoka sasa hivi.
Jana usiku alipokuja alikuwa amelewa na alipomuua Masudi hakuondoka tena hadi
hii asubuhi”
“Kumbe majini pia wanalewa?”
“Wanalewa kama watu. Harishi
analewa sana”
“Hiyo pombe anaipata wapi?”
“Sijui mwenyewe”
“Na anapokuta mtu mle ndani
anakuuliza ni nani?”
“Anaua kwanza halafu ndio
anauliza. Mimi humwambia kwamba ni wavuvi wameingia kwa bahati mbaya. Lakini
kama angenikuta nimelala naye angejua ni mwanaume wangu”
“Angekuua?”
“Sijui ingekuwaje?”
Pakapita kimya cha sekunde
kadhaa. Sote tulikuwa tunamkumbuka kaka yetu Masidi.
“Mtanisamehe sikuwaletea
chai. Nilikuwa nimetaharuki sana”
Yasmin akatuambia baadaye.
“Misiba kama hii. Kila siku
anakufa mtu. Hamu ya kula pia inapotea” nikamwambia.
“Nyinyi mtabaki huku huku
mjaribu bahati zenu. Mnaweza kusalimika”
ITAENDELEA KESHO NINI KITAJITOKEZA, USIKOSE MTU WANGU
No comments:
Post a Comment