Monday, December 22, 2014

MTOTO WA MIAKA 7 ATUMBUKIA KISIMANI NA KUFA

Kumekucha blog

Muheza,MTOTO wa darasa la pili Asha Mussa (7) mkazi wa kijiji cha Darajani kata ya Potwe Wilayani Muheza Mkoani Tanga  amekufa baada ya kutumbukia katika kisima wakati mama yake akifua nguo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Freisser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 9 jioni wakati mama huyo Mariam Bakari akifua nguo.

Alisema wakati akifua nguo Asha alikuwa akicheza  na mwenzake kilipo karibu  kisima  na wakati anakimbia alitumbukia na kufariki baada ya kunywa maji mengi.

“Yule mtoto alikufa mara tu ya kutumbukia katika kisima baada ya kunywa maji mengi---wakati anacheza na mwenzake alikimbia na kuteleza katika kisima ambacho kilikuwa karibu” alisema

“Mama mtoto hakuwa makini mazingira ya pale katika kisima kwani  hayaruhusu kucheza mchezo wowote kwanza kulikuwa na utelezi na kisima chenyewe hakikuwa na ukingo wa kuzuia endapo mtu ameteleza” alisema Kashai

Katika tukio jengine mkazi wa kijiji cha  Kichemba tarafa ya Ngomeni Muheza, Ismail Baraka, amekufa baada ya kugongwa na bodaboda wakati akikatisha barabara.

Alisema uchunguzi wa awali wa kipolisi umeonyesha kuwa marehemu aligongwa na pikipiki wakati akikatisha barabara sehemu ambayo haina alama za barabarani na hivyo dereva wa bodaboda akiwa mwendo kasi.

Alisema marehemu alifariki papo hapo baada ya kugongwa sehemu ya ubavu na kuangukia kichwa na kusababisha kutokwa na damu nyingi na wakati akipelekwa hospitali alikuwa ameshafariki.

“Kwa sasa tunamsaka dereva wa bodaboda kwani ilipomgonga tu marehemu alinyanyua pikipiki yake na kukimbia----tunaendelea kumsaka ili kumfikisha mahakamani” alisema Kashai

Akitoa wito kwa watumiaji wa barabara, kamanda Kashai aliwataka wananchi kuzingatia alama za barabarani ili kuepusha ajali za kujitakia na kuwashauri kujifunza alama zake pamoja na wenye vyombo vya moto wakiwemo madereva wa pikipiki.

                                   Mwisho

No comments:

Post a Comment