Kumekucha blog
Korogwe, WAKULIMA na wafanyabiashara wa
matunda na mbogamboga Wilayani Korogwe Mkoani Tanga, wamelalamika kukosa soko
la kuuzia mazao yao na hivyo kulazika kuuza kwa bei ya hasara kwa hofu ya kuharibika majumbani.
Wakizungumza na Mwananchi jana, mji mdogo wa Mombo,
wafanyabiashara hao wamesema wanalazimika kuuza matunda yao kwa bei ya hasara
baada ya kutokuwepo kwa soko na hivyo kuwaomba matajiri na wawekezaji kujenga
kiwanda cha kusindika matunda Wilayani hapo.
Walisema wamekuwa wakiuza matunda yao kwa bei ya
hasara kwa hofu ya kuwaozea majumbani jambo ambalo linarudisha nyuma kasi ya
kilimo na baadhi ya wakulima kuacha kilimo hicho .
“Kama unavyoona hapa matunda ni mengi sana hadi
tunapatwa na hofu ya kutuozea mikononi----zikipitia siku mbili kama hujamaliza
mzigo jua yatakuharibikia mikononi na kuwa hasara” alisema Jumanne Ramadhani
“Tunalazimika kuuza kwa bei yoyote ile ---hatuna soko
rasmi la kuuzia matunda na tuko juu juu na kutokuwa na uhakika wa kuuza
kutegemea mteja mmoja mmoja sio biashara” alisema Ramadhani
Kwa upande wake mkulima wa mapeasi, Miraji Shemdoe,
alisema wakulima wengi wa matunda na mbogamboga wamepunguza kasi ya kilimo chao
na kuyaacha mashamba kuwa pori.
Ameitaka Serikali kukisikiza kilio chao baada ya
maombi ya muda mrefu na kupewa matumaini na kudai hadi muda huo hakuna matumaini na hivyo
kuwarejesha katika umasikini.
Alisema wakulima wa Lushoto na Korogwe wako na nafasi
nzuri ya kujikwamua na umasikini baada ya ardhi yao kuwa na rutba ya kilimo
ambacho hakitegemi mvua za misimu.
“Tumejaliwa kuwa na ardhi nzuri yenye rutba ya kilimo
cha aina yoyote lakini soko ndio shida----wakulima wengi wamebadilisha aina ya
kilimo na sio matunda tena” alisema Shemdoe
Alisema kuwepo kwa soko la uhakika wakazi wa ndani na nje ya Wilaya hiyo
wangeshawishika kulima kilimo hicho na Serikali kupata mapato yatakayosaidia
huduma za kijamii Wilayani humo.
No comments:
Post a Comment