SIMULIZI
YALIYONIKUTA TANGA (2)
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
Maafisa hao waliokuwa na
nyuso zilizofadhaika walitabasamu walipoliona sanduku hilo
likiwa salama na limefungwa kwa funguo kama
lilivyokuwa lilipotoka benki.
Baada ya kulipakia kwenye
gari walilokuja nalo walinipa mikono ya pongezi na shukurani.
“Tunakushukuru sana kwa ujasiri wako, umefanya kazi nzuri sana” Afisa mmoja
akanimabia kwa furaha.
Polisi wanne waliofika hapo
waliniuliza kulikoni. Nikawaeleza mkasa uliotokea. Baada ya kupata maelezo
yangu walimtoa yule jambazi aliyekuwa amebanwa ndani ya lile gari
nililolipindua. Alikuwa hoi. Damu ilikuwa inamtoka puani na mdomoni.
Hapo tukagawanyana kazi.
Polisi wawili walisindikiza zile pesa kiwanda cha bia. Sisi wengine tulibaki
pale pale tukiwasiliana na maafisa wetu.
Dakika chache tu baadaye polisi
na makachero kutoka makao ya polisi walitinga katika eneo hilo.
Kila kachero na kila polisi
aliyefika hapo alinipongeza kwa kazi nzuri, kuwaua majambazi wanne na kuokoa
kiasi kikubwa cha pesa za mishahara ya wafanyakazi wa kiwanda cha bia. Baadye ilibainika
kuwa pesa hizo zilikuwa zaidi ya shilingi milioni mia tatu.
Majambazi niliowaua
walipelekwa katika chumba cha maiti cha hospitali ya Muhimbili pamoja na yule
polisi mwenzetu aliyeuawa. Jambazi aliyejeruhiwa baada ya kumpindua na gari naye
alipelekwa kutibiwa katika hospitali hiyo hiyo akiwa chini ya ulinzi mkali.
SASA ENDELEA
Siku ile ile niliitwa makao
ya polisi. Niliambiwa kutokana na ujasiri niliouonesha wa kupambana na
majambazi wanne na kuwaua na kuokoa pesa walizotaka kuzipora, nimehamishiwa
katika idara ya upelelezi ya makosa ya jinai. Hivyo sitatumia tena sare za
polisi bali nitakuwa nikivaa kiraia.
Mbali na kuhamishiwa katika
idara nyingine ya kazi nilihamishiwa pia katika kituo kingine cha kazi. Kutoka
kituo cha polisi Ilala nilipelekwa makao ya polisi.
Mabadiliko hayo yalinipa
furaha na faraja na kwa upande wangu yalikuwa kama
cheo kwani yalisogeza karibu na wakubwa.
Nikiwa katika idara hii ya
upelelezi makao ya polisi ndipo jeuri yangu ilipoanza.
Pale nilikutana na makachero
wenzangu vijana walionizidi kielimu. Tulikuwa tukivinjari katika mitaa ya jiji
la Dar mchana kutwa.
Tulikuwa katika vikundi
vikundi. Siku tunakuwa wawili, siku nyingine tunakuwa watatu.
Kilichonifurahishani kuwa kila mmoja wetu alikuwa amekabidhiwa bastolayake kwa
ajili ya kukabiliana na tukio lolote la kiusalama.
Nilipoanza kazi hii ya
ukachero makao ya polisi nilibadilisha mavazi nikawa napendelea sana kuvaa koti. Watu
wengi waliokuwa wananifahamu hawakujua ni kwanini nilikuwa sibandukani na koti.
Wengi walidhani ni mbwembwe zangu. Lakini ukweli ni kuwa nilikuwa navaa koti
ilikuficha bastola yangu na pia kupata urahisi wa kuitoa na kuitumia pale
inapohitajika.
Nilipata rafiki kachero
mwenzangu aliyeitwa Shaali Shazume. Alikuwa Mzanzibari aliyehamishiwa Dar kutoka
Unguja.
Mimi na Shaali tulikuwa na
tabia ya kutengeza kesi na kujipatia rushwa mara nyingi.
Lakini siku moja taarifa zetu
zikatua kwenye mez ya mkuu wetu. Akatuita na kutuambia kuwa alikuwa amepata
ushahidi juu ya tabia yetu ya kuwatengezea watu kesi na kula rushwa. Kutengeza
kesi kulimaanisha kumbambikia mtu kesi.
Mimi na Shaali tulizikana
tuhuma hizo na tukatolewa ushahidi ambao pia tuliukana kwa kudai kuwa ulikuwa
ushahidi wa uongo.
Kukana kwetu kulitusaidia
tusifukuzwe kazi lakini mimi na Shaali tukatenganishwa. Mimi nilihamishiwa mkoa
wa Tanga na Shaali akapelekwa Tanga.
Sikuwahi kufika katika mkoa
huo kabla ya hapo isipokuwa nilikuwa nikiusikia sifa zake. Na nilipoambiwa
ninakwenda Tanga nilifurahi.
Nilifanya kazi Tanga kwa
takribani mwaka mmoja. Nikagundua kuwa mkoa huo ulikuwa na watu wakarimu sana na pia ulikuwa na wasichana warembo sana.
Haukuwa mkoa wenye hekaheka kama ilivyo mikoa mengine ambapo polisin wanakuwa na
mchakamchaka mchana wakati wote. Kusema kweli nilipokuwa Tanga nilitulia.
Kwenye kituo nilichokuwa
nafanya kazi kulikuwa na sajenti mmoja ambaye alikuwa mtu wa nyumbani. Alisoma
na kaka yangu Kagera.
Alikuwa ni sajenti Erick.
Kachero huyo licha ya kunipenda alinichukulia kama
mdogo wake. Mara nyingi alikuwa akinipa upendeleo wa kikazi. Siku za mapumziko
nilikuwa namtembelea nyumbani kwake ambapo huzungumza na kukumbushana matukio
ya kwetu Kagera.
Sikuwa nikijua kuwa nilikuwa
namtengeza Shaali mwingine badala ya yule niliyekuwa naye Dar kwani baada ya
miezi michache tu yalitufika makubwa.
Kuna siku nilikuwa kwenye
mizunguko yangu ya kikazi. Sajenti Erick akanipigia simu. Nilishituka
nilipoonanamba yake kwa sababu hakuwa na kawaida ya kunipigia simu.
“Shikamoo afande” nilimuamkia
,mara tu nilipopokea simu yake.
“Marahaba Martin. Uko wapi
muda huu?” akaniuliza kwenye simu. Martin ndio jina langu. Jina langu kamili ni
Martin Philip Lazaro.
“Niko eneo la stendi ya
mabasi” nikamjibu.
“Kuna nini huko?”
“Naangaza kwenye mabasi
yanayotoka Mombasa.
Naweza kushika mirungi”
“Sasa umefanikiwa?”
“Hakuna kitu, nataka kurudi
kituoni”
“Hebu njoo hapa hoteli ya
Mtendele”
Mtendele ni hoteli moja
maarufu iliyoko eneo la Chuda.
“Wewe uko hapo?”
Sikutaka kumuuliza kuna nini.
Nilikodi bodaboda ikanipeleka Mtendele. Nilipoingia nilimkuta Erick akinywa
bia.
Kiumri alikuwa amenizidi kwa
miaka isiyopungua minane.
“Kaa hapo” akaniambia
akinionesha kiti kilichokuwa kwenye meza aliyoketi.
“Najua huna pesa, nataka
nikupe kazi lakini uwe ngangari” akaniambia mara tu nilipoketi kwenye kiti hicho
“Sawa”
“Nimepata taarifa moja, kuna
mama mmoja na binti yake wana duka la vitu vya dhahabu na mapambo ya wanawake
pale barabara ya nane kwa barabara ya jamaa”
“Ana nini huyo mama?”
nikamuuliza.
“Nataka twende tukapekue
nyumbani kwake, nimesikia anajishughulisha na biashara ya madawa ya kulevya.
Lile duka ni danganya toto tu”
“Sawa. Twende tukafanye hiyo
kazi”
“Ngoja nimalize bia yangu
twende”
“Si itabidi twende kituoni
tukaandike hati ya upekuzi”
“Hapana, twende hivi hivi tu.
Si kila kitu kinahitaji hati ya upekuzi. Kwanza
watu wenyewe ni wanawake, hawajui sheria yoyote”
“Sawa”
Erick akamaliza bia yake na
kuinuka.
“Twenzetu”
Tulitoka hapo hotelini. Erick
alikodi teksi ikatupeleka barabara ya nane katika hiyo nyumba.
Ilikuwa nyumba ya kizamani
iliyojengwa kwa mawe lakini ilipigwa lipu na kupakwa chokaa. Ilikuwa na mlango
mmoja wa duka lakini kwa muda ule tuliokwenda duka hilo lilikuwa limefungwa.
Je nini kitatokea? Usikose
kuendelea na simulizi hii kesho.
No comments:
Post a Comment