NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 38
ILIPOISHIA
Nikaenda nyuma ya gari na
kulitoa lile shepe.
“Njoo hapa” akaniambia akiwa
amesimama mahali fulani kando ya lile gari.
Nilipofika karibu yake
akaniambia.
“Chimba mahali hapa”
Alinionesha pale aliposimama
kisha akaondoka na kusimama kando yake.
Nikaanza kupachimba mahali
hapo kwa kutumia lile shepe. Bahati nzuri mchanga ulikuwa laini, sikutumia
nguvu nyingi. Niliendelea kuchimba mpaka
shimo likafikia urefu wa wastani wa futi mbili.
“Nichimbe hadi wapi?”
“Bado. Endelea kuchimba”
Maimun akaniambia.
Nikaendelea kuchimba. Mwili
wangu ukaanza kutoka jasho. Nikaacha kuchimba na kuvua shati.
“Lete nikushikie” Maimun
akaniambia.
Nikampa lile shati na kuendelea
kuchimba.
SASA ENDELEA
Niliendelea kuchimba lile
shimo mpaka likanifikia usawa wa kifua. Nilikuwa nikimwaga mchanga juu ya shimo
hilo. Ghafla nikaona ninapiga kitu kama
mwamba au jiwe lililokuwa chini ya ardhi.
“Sijui nimepiga nini hapa?” nikamuuliza
Maimun kwa mshituko.
“Huo ni mwamba, upige tena”
Maimun akaniambia.
Nikaupiga tena kwa shepe.
“Piga tena”
Nikaupiga kwa mara ya tatu.
Ule mwamba ukapasuka.
“Umepasuka” nikamwambia
Maimun.
“Hebu washa kitochi cha simu
yako umulike hapo palipopasuka” Maimun akaniambia.
Nikajipapasa mfukoni na kutoa simu yangu. Niliwasha
kitochi nikamulika pale chini.
Mama yangu! Niliona vipande vya madini yanayomeremeta vikiwa
vimetawanyika!
“Nini hii?” nikamuuliza
Maimun kwa mshituko.
“Kwani umeona nini?”
“Sijui ni madini haya. Huu mwaba ulikuwa na madini!”
“Ndiyo ni madini”
“Sijui ni madini ya aina gani?”
“Ni Tanzanite, ni yale
aliyokuwa akiuza babu yako”
“Niyachukue”
“Ndiyo yachukue”
Nikainama haraka na kuyachukua
yale madini.
Vilikuwa vipande saba vya
madini.
“Huu ni utajiri hasa!
Nikajiambia kimoyomoyo kisha nikamshukuru Mungu.
“Mungu anipe nini tena!”
Yakiwa mikononi mwangu madini
hayo yalikuwa yakiakisi rangi mbali mbali za dunia. Zile rangi zilikuwa kama
zinazunguka. Ilikuwa ni furaha hata kuyatazama.
“Ni vipande vingapi?” Maimun
akaniuliza.
“Viko saba”
“Haya sasa toka kwenye hili
shimo”
“Ngoja niendelee kuupiga huu
mwamba”
“Hapana, usirudie tena. Toka
kwenye shimo” Maimun akanionya.
Nikayatia yale madini
mifukoni mwangu kisha nikalitoa lile shepe na kuliweka juu ya shimo hilo.
“Lete mkono wako nikutoe”
Maimun akaniambia.
Nikampa mkono wangu Maimun,
akaushika na kunivuta. Mara moja
nikjioan niko juu ya lile shimo.
“Anza kulifukia haraka
haraka”
Nikalichukua shepe hilo na kufukia
lile shimo.
“Tutakuja lini tena
kuchimba?” nikamuuliza Maimun kwa tamaa huku nikiendelea kufukia shimo hilo.
“Baada ya miezi sita”
“Ah kwanini! Mbona mbali sana?”
“Ndiyo masharti yake. Haya
madini yanakaliwa na majini. Huwezi kuja kienyeji tu na kuyachimba na hata
ukija hutoyaona. Masharti yake ndiyo haya ninayokupa. Kila baada ya miezi sita tunakuja kuchimba
tena”
“Sawa”
Niliendelea kulifukia lile
shimo mpaka nikaliweka sawa.
“Watu wengine hawatakuja
kufukua?” nikamuuliza Maimun.
“Ni nani atakayethubutu?”
“Wanaweza kutokea watu wakaja
kufukua”
“Hawatapata kitu chochote.
Chukua shati lako tuondoke”
Nililichukua lile shati
alilokuwa amelishika Maimun nikalivaa.
“Twenzetu” akaniambia.
Nililiweka shepe nyuma ya
gari.
“Utaendesha wewe?” Maimun akaniambia.
“Sawa” nikamjibu haraka
haraka na kwenda kufungua mlango wa gari wa upande wa dereva.
Maimun alifungua mlango wa
upande wa pili wa dereva na kujipakia.
“Washa gari tuondoke. Muda
umekwenda sana”
Nikaliwsha gari na kuliondoa.
Nilipokuja na Maimun mahali hapo nilikuwa nimefadhaika lakini wakati tunaondoka
moyo wangu ulikuwa na furaha iliyopita kiasi.
“Hivi babu yangu ulikuwa
unakuja naye hapa hapa kuchimba haya madini?”
“Ninajua mimi kama tulikuwa
tunakuja hapa au mahali pengine”
“Hutaki kuniiambia”
“Si lazima kila kitu ukijue
kwa sasa Kasim”
“Sawa mke wangu”
Nikabaki kimya mpaka
tulipotokea pale mahali ambapo majambazi walitaka kulipora gari langu. Yule mtu
aliyenata huku mkono wake mmoja ukipiga ngumi kwenye hewa alikuwa bado amenata
vile vile na yule aliyeaguka alikuwa bado yuko chini. Lile gari lao pia lilikuwa pale pale.
“Kumbe hawa watu bado
wapo?”nikamuuliza Maimun.
“Si uwaache tu. Majambazi
wanakuhusu nini?”
“Nilikuwa nasema tu”
“Sema maneno yenye maana.
Achana na watu hao”
“Inaonekana walikuudhi sana”
ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 39
ILIPOISHIA
Maimun hakunijibu chochote na
mimi nikanyamaza. Mawazo yalikuwa yakipita akilini mwangu
Niliwaza si muda mrefu
nitakuwa mmoja wa matajiri wakubwa hapa
nchini. Nitakuwa ninazungka kwa ndege katika nchi mbalimbali kama alivyokuwa babu yangu.
Huku nikiliendesha gari kwa mbwembwe, nilijiambia fedha
itakaponikubali sawasawa, nitamshawishi Maimun ninunue jumba jingine la
kifahari eneo la Masaki ambalo nilikuwa
niikitamani sana kuishi.
Pia nilitaka ninunue
gari jingine la gharama kutoka Ulaya.
Ikiwezekana magari mawili la Maimun na la
kwangu.
Tulipofika nyumbani Maimun
aliniambia niyatoe yale madini. Nikayatoa mifukoni.
Aliyashika shika na
kuyaangalia kisha aliniambia.
“Kuwa makini sana, wewe bado
ni kijana mdogo. Nakuomba uwe msikivu. Ujue
kuwa ukifanya papara utakwenda na maji”
“Kwanini?”
“Si lazima kila kitu
nikwambie, unapaswa kutumia akili yako. Mimi sitaki uwe mtu wa papara”
SASA ENDELEA
“Kwani umenionaje mke wangu?”
nikamuuliza Maimun baada ya kutomuelewa.
“Nimekuona una papara. Jicho
limekutoka kwenye haya madini. Unajiona tayari umeshakuwa tajiri. Nataka
nikukumbushe kuwa hii mali yote ni yangu mimi. Wewe ninakupa uimiliki tu,
wakati wowote utakapovunja masharti yangu nninaichukua mwenyewe”
“Sitavunja masharti yako,
wewe acha tu niimiliki. Kila mara unapenda kunituhumu lakini mimi sina tatizo”
“Sasa sikiliza. Tafuta
wanunuzi wa haya madini hapa hapa nchini. Sitaki uende nje ya nchi kama alivyokuwa
babu yako. Na pia huwezi kuyauza madini yote kwa pamoja. Uza moja moja”
“Kwanini hutaki niende
nikayauze nchi za nje wakati huko nitapata bei nzuri kuliko ya hapa?”
nikamuuliza.
“Uhitajji kupata pesa nyingi.
Pesa yoyote utakayopata itakutosha kwa sababu kila baada ya miezi sita utapata
madini mingine, una wasiwasi gani?”
“Mimi nilitaka niende nje
lakini kama unataka tuyauze hapa hapa, sawa”
“Wewe unajua jiwe moja
litakupatia kiasi gani?”
Pesa nyingi sana. Naweza hata
kujenga jumba moja la ghorofa”
“Sasa kiherehere chako ni cha
nini?”
Nikacheka kidogo kisha
nikamwambia.
“Sina kiherehere. Sasa
nitakwenda kuyauza lini haya madini?’
“Ni wewe tu”
Basi kesho nitaanza kufanya utafiti wa wateja”
“Sawa”
Naam, hivyo ndiyo nilivyoanza
kutajirika. Nilifanikiwa kuviuza vipande vyote saba. Nikapata kiasi kikubwa cha
pesa. Maimun aliniambia pesa hizo nisiziweke benki, niziache pale pale nyumbani
atazilinda mwenyewe.
Badala ya sanduku moja la
pesa tulilokuwa nalo kabatini, tukawa na masanduku mawili. Kila baada ya miezi
sita nilienda na Maimun kuchimba madini mengine ambayo niliyauza. Nikapata
utajiri mkubwa.
Maimun aliniruhusu ninunue
nyumba jingine Masaki. Nikanunua jumba la kifahari ambalo alikuwa akiishi
mzungu mmoja. Nililinunua kwa bilioni tatu.
Nikaagiza magari mawili
kutoka Uingereza aina ya Benz. Moja
nilitaka nimpe Maimun lakini akaniambia hataki kuwa na gari la peke yake ila
tuyatumie yote mawili kwa pamoja.
Pia nilifungua miradi mbali
mbali ya kibiashara. Nikawa mmoja wa watu maarufu katika jiji la Dar na pia nikawa mmoja wa matijiri wakubwa Afrika.
Baada ya kuishi na Maimun kwa
miaka mitatu aliniambia yale madini
yamekwisha, kwa hiyo tutumie fedha tulizonazo na kwamba atakapoona inafaa
atanionesha mahali pengine pa kuchimba madini mengine ya Tanzanite.
Siku za mwanzo mwanzo nilizoanza kuishi na Maimun nilikuwa
nikimuogopa lakini kidogo dogo nikaanza kumzoea na kumuona wa kawaida. Ilifikia
mahali nilikuwa ninabishana naye kupinga maamuzi yake na kumwambia kwamba mimi ndiye
mume, kwa hiyo anapaswa kunisikiliza mimi.
“Nimekupa mali sasa imekulewesha” alikuwa akiniambia baada ya kuona sitaki kumsikiliza.
“Sio hivyo Maimun, amri zako nyingine
zinanikera”
“Mimi najua kinachokupa
kiburi ni huu utajiri lakini ujue kwamba ninaweza kuufyeka kwa siku moja tu”
“Hapana, usifanye hivyo Maimun. Nipe uhuru wa kushauriana na wewe.
Kwanini ninapokushauri kitu unatishia kuchukua mali yako?”
“Ni kwa sababu ninataka
unitii mimi”
“Basi yaishe. Naogopa kurudi
katika umasikini”
Hivyo ndivyo nilivyokuwa
ninaishi na Maimun. Alikuwa na wivu mwingi pamoja na kufuatilia mambo yangu kwa
karibu. Wakati mwingine nilikuwa nachukia.
Kwa maisha ya nyumbani,
Maimun alikuwa mke wa kweli aliyenionesha upendo na alinipa mamlaka ya
kuimiliki nyumba vile ninavyotaka mimi.
Wakati mwingine nilimtolea ukali, Maimun akaniomba msamaha kwa kuwa nilikuwa
mume wake.
Jamani huu ndio mkasa wa urithi wa babu yangu. Nilikiona cha
moto lakini mwishoni nikaja kupata mke wa kijini na kupata utajiri ambao sikuutarajia.
Kilichokuwa kinanipa uchungu
ni kuwa Maimun alipata ujauzito wangu
mara tatu lakini alikwenda kujifungulia kwao. Wale watoto alikuwa akiwaleta
nyumbani usiku. Inapofika alfajiri anawarudisha kwao.
Nilipomuuliza ni kwanini
anafanya hivyo aliniambia anataka watoto
hao wawe majini kama yeye. Hakutaka wazoeane na watu na kwamba watoto hao hawataenda
shule ila watasomea huko huko ujinini.
“Watakapokuwa wakubwa
watakuja kukusaidia, watakuwa kama
binaadamu na utaweza kuwatuma popote” Maimun aliniambia.
Mtoto wangu wa kwanza
niliyemzaa na Maimun, hivi sasa ana miaka
saba. Wa pili ana miaka minne na wa tatu
bado ni mchanga. Nilikuwa kiona jinsi anavyonyonyeshwa na mama yake
ifikapo usiku anapokuja naye nyumbani
pamoja na wale watoto wengine.
Sijui nitakapokufa Maimun
atakwenda kwa nani kwani sikuwa na
mrithi. Huenda atakwenda kwa mtu mwingine atakayemchunuka.
Hadi hii leo niko na Maimun
huko nyumbani kwangu Masaki lakini wageni ni marufuku nyumbani kwangu.
MWISHO