Friday, June 9, 2017

SIMULIZI, NILIKONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 38

NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 38
 
ILIPOISHIA
 
Nikaenda nyuma ya gari na kulitoa lile shepe.
 
“Njoo hapa” akaniambia akiwa amesimama mahali fulani kando ya lile gari.
 
Nilipofika karibu yake akaniambia.
 
“Chimba mahali hapa”
 
Alinionesha pale aliposimama kisha akaondoka na kusimama kando yake.
 
Nikaanza kupachimba mahali hapo kwa kutumia lile shepe. Bahati nzuri mchanga ulikuwa laini, sikutumia nguvu nyingi. Niliendelea kuchimba  mpaka shimo likafikia urefu wa wastani wa futi mbili.
 
“Nichimbe hadi wapi?”
 
“Bado. Endelea kuchimba” Maimun akaniambia.
 
Nikaendelea kuchimba. Mwili wangu ukaanza kutoka jasho. Nikaacha kuchimba na kuvua shati.
 
“Lete nikushikie” Maimun akaniambia.
 
Nikampa lile shati na kuendelea kuchimba.
 
SASA ENDELEA
 
Niliendelea kuchimba lile shimo mpaka likanifikia usawa wa kifua. Nilikuwa nikimwaga mchanga juu ya shimo hilo. Ghafla nikaona  ninapiga kitu kama mwamba au jiwe lililokuwa chini ya ardhi.
 
“Sijui nimepiga nini hapa?” nikamuuliza Maimun kwa mshituko.
 
“Huo ni mwamba, upige tena” Maimun akaniambia.
 
Nikaupiga tena kwa shepe.
 
“Piga tena”
 
Nikaupiga kwa mara ya tatu. Ule mwamba ukapasuka.
 
“Umepasuka” nikamwambia Maimun.
 
“Hebu washa kitochi cha simu yako umulike hapo palipopasuka” Maimun akaniambia.
 
Nikajipapasa  mfukoni na kutoa simu yangu. Niliwasha kitochi nikamulika pale chini.
 
Mama yangu! Niliona  vipande vya madini yanayomeremeta vikiwa vimetawanyika!
 
“Nini hii?” nikamuuliza Maimun kwa mshituko.
 
“Kwani umeona  nini?”
 
“Sijui  ni madini haya. Huu mwaba ulikuwa na madini!”
 
“Ndiyo ni madini”
 
“Sijui  ni madini ya aina gani?”
 
“Ni Tanzanite, ni yale aliyokuwa akiuza babu yako”
 
“Niyachukue”
 
“Ndiyo yachukue”
 
Nikainama haraka na kuyachukua yale madini.
 
Vilikuwa vipande saba vya madini.
 
“Huu ni utajiri hasa! Nikajiambia kimoyomoyo kisha nikamshukuru Mungu.
 
“Mungu anipe nini tena!”
 
Yakiwa mikononi mwangu madini hayo yalikuwa yakiakisi rangi mbali mbali za dunia. Zile rangi zilikuwa kama zinazunguka. Ilikuwa ni furaha hata kuyatazama.
 
“Ni vipande vingapi?” Maimun akaniuliza.
 
“Viko saba”
 
“Haya sasa toka kwenye hili shimo”
 
“Ngoja niendelee kuupiga huu mwamba”
 
“Hapana, usirudie tena. Toka kwenye shimo” Maimun akanionya.
 
Nikayatia yale madini mifukoni mwangu kisha nikalitoa lile shepe na kuliweka juu ya shimo hilo.
 
“Lete mkono wako nikutoe” Maimun akaniambia.
 
Nikampa mkono wangu Maimun, akaushika na kunivuta. Mara moja  nikjioan niko juu ya lile shimo.
 
“Anza kulifukia haraka haraka”
 
Nikalichukua shepe hilo na kufukia lile shimo.
 
“Tutakuja lini tena kuchimba?” nikamuuliza Maimun kwa tamaa huku nikiendelea kufukia shimo hilo.
 
“Baada ya miezi sita”
 
“Ah kwanini! Mbona  mbali sana?”
 
“Ndiyo masharti yake. Haya madini yanakaliwa na majini. Huwezi kuja kienyeji tu na kuyachimba na hata ukija hutoyaona. Masharti yake ndiyo haya ninayokupa.  Kila baada ya miezi sita tunakuja kuchimba tena”
 
“Sawa”
 
Niliendelea kulifukia lile shimo mpaka nikaliweka sawa.
 
“Watu wengine hawatakuja kufukua?” nikamuuliza Maimun.
 
“Ni nani atakayethubutu?”
 
“Wanaweza kutokea watu wakaja kufukua”
 
“Hawatapata kitu chochote. Chukua shati lako tuondoke”
 
Nililichukua lile shati alilokuwa amelishika Maimun nikalivaa.
 
“Twenzetu” akaniambia.
 
Nililiweka shepe nyuma ya gari.
 
“Utaendesha wewe?” Maimun akaniambia.
 
“Sawa” nikamjibu haraka haraka na kwenda kufungua mlango wa gari wa upande wa dereva.
 
Maimun alifungua mlango wa upande wa pili wa dereva na kujipakia.
 
“Washa gari tuondoke. Muda umekwenda sana”
 
Nikaliwsha gari na kuliondoa. Nilipokuja na Maimun mahali hapo nilikuwa nimefadhaika lakini wakati tunaondoka moyo wangu ulikuwa na furaha iliyopita kiasi.
 
“Hivi babu yangu ulikuwa unakuja naye hapa hapa kuchimba haya madini?”
 
“Ninajua mimi kama tulikuwa tunakuja hapa au mahali pengine”
 
“Hutaki kuniiambia”
 
“Si lazima kila kitu ukijue kwa sasa Kasim”
 
“Sawa mke wangu”
 
Nikabaki kimya mpaka tulipotokea pale mahali ambapo majambazi walitaka kulipora gari langu. Yule mtu aliyenata huku mkono wake mmoja ukipiga ngumi kwenye hewa alikuwa bado amenata vile vile na yule aliyeaguka alikuwa bado yuko chini. Lile  gari lao pia lilikuwa pale pale.
 
“Kumbe hawa watu bado wapo?”nikamuuliza Maimun.
 
“Si uwaache tu. Majambazi wanakuhusu nini?”
 
“Nilikuwa nasema tu”
 
“Sema maneno yenye maana. Achana  na watu hao”
 
“Inaonekana walikuudhi sana”
 
 
 
 
 
 
 
 
ZULIA LA FAKI
 
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 39
 
ILIPOISHIA
 
Maimun hakunijibu chochote na mimi nikanyamaza. Mawazo yalikuwa yakipita akilini mwangu
 
Niliwaza si muda mrefu nitakuwa mmoja  wa matajiri wakubwa hapa nchini. Nitakuwa ninazungka kwa ndege katika nchi  mbalimbali kama alivyokuwa babu yangu.
 
Huku nikiliendesha  gari kwa mbwembwe, nilijiambia fedha itakaponikubali sawasawa, nitamshawishi Maimun ninunue jumba jingine la kifahari eneo la Masaki ambalo  nilikuwa niikitamani sana kuishi.
 
Pia nilitaka ninunue gari  jingine la gharama kutoka Ulaya. Ikiwezekana magari mawili la Maimun na la  kwangu.
 
Tulipofika nyumbani Maimun aliniambia niyatoe yale madini. Nikayatoa mifukoni.
 
Aliyashika shika na kuyaangalia kisha aliniambia.
 
“Kuwa makini sana, wewe bado ni kijana mdogo. Nakuomba uwe msikivu.  Ujue kuwa ukifanya papara utakwenda na maji”
 
“Kwanini?”
 
“Si lazima kila kitu nikwambie, unapaswa kutumia akili yako. Mimi sitaki uwe mtu wa papara”
 
SASA ENDELEA
 
“Kwani umenionaje mke wangu?” nikamuuliza Maimun baada ya kutomuelewa.
 
“Nimekuona una papara. Jicho limekutoka kwenye haya madini. Unajiona tayari umeshakuwa tajiri. Nataka nikukumbushe kuwa hii mali yote ni yangu mimi. Wewe ninakupa uimiliki tu, wakati wowote utakapovunja masharti yangu nninaichukua mwenyewe”
 
“Sitavunja masharti yako, wewe acha tu niimiliki. Kila mara unapenda kunituhumu lakini mimi sina  tatizo”
 
“Sasa sikiliza. Tafuta wanunuzi wa haya madini hapa hapa nchini. Sitaki uende nje ya nchi kama alivyokuwa babu yako. Na pia huwezi kuyauza madini yote kwa pamoja. Uza moja moja”
 
“Kwanini hutaki niende nikayauze nchi za nje wakati huko nitapata bei nzuri kuliko ya hapa?” nikamuuliza.
 
“Uhitajji kupata pesa nyingi. Pesa yoyote utakayopata itakutosha kwa sababu kila baada ya miezi sita utapata madini mingine, una wasiwasi gani?”
 
“Mimi nilitaka niende nje lakini kama unataka tuyauze hapa hapa, sawa”
 
“Wewe unajua jiwe moja litakupatia kiasi gani?”
 
Pesa nyingi sana. Naweza hata kujenga jumba moja la ghorofa”
 
“Sasa kiherehere chako ni cha nini?”
 
Nikacheka kidogo kisha nikamwambia.
 
“Sina kiherehere. Sasa nitakwenda kuyauza lini haya madini?’
 
“Ni wewe tu”
 
Basi kesho  nitaanza kufanya utafiti wa wateja”
 
“Sawa”
 
Naam, hivyo ndiyo nilivyoanza kutajirika. Nilifanikiwa kuviuza vipande vyote saba. Nikapata kiasi kikubwa cha pesa. Maimun aliniambia pesa hizo nisiziweke benki, niziache pale pale nyumbani atazilinda mwenyewe.
 
Badala ya sanduku moja la pesa tulilokuwa nalo kabatini, tukawa na masanduku mawili. Kila baada ya miezi sita nilienda na Maimun kuchimba madini mengine ambayo niliyauza. Nikapata utajiri mkubwa.
 
Maimun aliniruhusu ninunue nyumba jingine Masaki. Nikanunua jumba la kifahari ambalo alikuwa akiishi mzungu mmoja. Nililinunua kwa bilioni tatu.
 
Nikaagiza magari mawili kutoka  Uingereza aina ya Benz. Moja nilitaka nimpe Maimun lakini akaniambia hataki kuwa na gari la peke yake ila tuyatumie yote mawili kwa pamoja.
 
Pia nilifungua miradi mbali mbali ya kibiashara. Nikawa mmoja wa watu maarufu katika jiji la  Dar na pia nikawa mmoja wa matijiri  wakubwa Afrika.
 
Baada ya kuishi na Maimun kwa miaka  mitatu aliniambia yale madini yamekwisha, kwa hiyo tutumie fedha tulizonazo na kwamba atakapoona inafaa atanionesha mahali pengine pa kuchimba madini mengine ya Tanzanite.
 
Siku za mwanzo mwanzo  nilizoanza kuishi na Maimun nilikuwa nikimuogopa lakini kidogo dogo nikaanza kumzoea na kumuona wa kawaida. Ilifikia mahali nilikuwa ninabishana naye kupinga maamuzi yake na kumwambia kwamba mimi ndiye mume, kwa hiyo anapaswa kunisikiliza mimi.
 
“Nimekupa  mali sasa imekulewesha”  alikuwa akiniambia baada ya kuona sitaki kumsikiliza.
 
“Sio hivyo Maimun, amri zako nyingine zinanikera”
 
“Mimi najua kinachokupa kiburi ni huu utajiri lakini ujue kwamba ninaweza kuufyeka kwa siku moja tu”
 
“Hapana, usifanye hivyo  Maimun. Nipe uhuru wa kushauriana na wewe. Kwanini ninapokushauri kitu unatishia kuchukua mali yako?”
 
“Ni kwa sababu ninataka unitii mimi”
 
“Basi yaishe. Naogopa kurudi katika umasikini”
 
Hivyo ndivyo nilivyokuwa ninaishi na Maimun. Alikuwa na wivu mwingi pamoja na kufuatilia mambo yangu kwa karibu. Wakati mwingine nilikuwa nachukia.
 
Kwa maisha ya nyumbani, Maimun alikuwa mke wa kweli aliyenionesha upendo na alinipa mamlaka ya kuimiliki nyumba  vile ninavyotaka mimi. Wakati mwingine nilimtolea ukali, Maimun akaniomba msamaha kwa kuwa nilikuwa mume wake.
 
Jamani huu ndio  mkasa wa urithi wa babu yangu. Nilikiona cha moto lakini mwishoni nikaja kupata mke wa kijini na kupata  utajiri ambao sikuutarajia.
 
Kilichokuwa kinanipa uchungu ni kuwa Maimun alipata ujauzito  wangu mara tatu lakini alikwenda kujifungulia kwao. Wale watoto alikuwa akiwaleta nyumbani usiku. Inapofika alfajiri anawarudisha kwao.
 
Nilipomuuliza ni kwanini anafanya hivyo aliniambia anataka  watoto hao wawe majini kama yeye. Hakutaka wazoeane na watu na kwamba watoto hao hawataenda shule ila  watasomea huko  huko ujinini.
 
“Watakapokuwa wakubwa watakuja kukusaidia, watakuwa kama  binaadamu na utaweza kuwatuma popote” Maimun aliniambia.
 
Mtoto wangu wa kwanza niliyemzaa na Maimun, hivi  sasa ana miaka saba. Wa pili ana miaka  minne na wa tatu bado ni mchanga. Nilikuwa kiona jinsi anavyonyonyeshwa na mama yake ifikapo  usiku anapokuja naye nyumbani pamoja na wale watoto wengine.
 
Sijui nitakapokufa Maimun atakwenda kwa nani kwani sikuwa  na mrithi. Huenda atakwenda kwa mtu mwingine atakayemchunuka.
 
Hadi hii leo niko na Maimun huko nyumbani kwangu Masaki lakini wageni ni marufuku nyumbani kwangu.
 
MWISHO

No comments:

Post a Comment