ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 35
ILIPOISHIA
Nikamtajia jina langu.
“Nikilitaja jina lako utaitikia
labeka”
“Sawa”
Mzee huyo akaniita.
Nikamuitikia “labeka”
“Ninakuozesha Maimun binti
Hashhash kwa mahari mliyokubaliana. Unakubali?”
“Nimekubali”
“Sema nimekubali kumuoa Maimun
binti Hashhash kwa mahari
tuliyokubaliana”
Nikasema kama vile
alivyonifundisha. Akarudi kunaimbia hivyo mara tatu.
Hapo hapo nikasikia sauti za
wanawake waliokuwa wamekaa ukumbini
ziking’ara kwa vifijo.
Yule mtu aliyekuwa
amenichukua kutoka mlango wa chumbani kwangu, akaniambia niinuke. Nilipoinuka
akanirudisha chumbani kwangu. Nilipoingia nilikuta chumba hicho kimebadilishwa.
SASA ENDELEA
Hakikuwa kile chumba changu
kabisa. Kitanda kilikuwa kimewekwa kingine. Kabati lilikuwa jingine na mapazia pia
yalikuwa mengine. Kwa kweli kilikuwa kimependeza sana. Hata taa zizokuwa
zinawaka zilikuwa ni za rangi mbali
mbali.
Nikamkuta Maimun binti
Hashhash amekaa kwenye kitanda. Pale
kwenye kitannda palikuwa pametandazwa maua ya mawarisi, asmini, vilua, mlangilangi na vitu vingine
ambavyo vilikuwa vikitoa harufu nzuri
mle chumbani.
Maimun alikuwa amepambwa na
kupendeza kama malkia wa Habesh. Alikuwa akinukia manukato ya kila aina. Mwili
wake ulikuwa umejaa mapambo ya dhahabu. Kuanzia kwenye shingo yake ambapo
palikuwa na mkufu mzito wa thamani. Masikioni mwake alikuwa amewekwa vipuli
vilivyokuwa vikimeremeta. Kwenye mikono yake alikuwa amevaa aina ya bangili za
dhahabu.
Kadhalika katika mguu wake wa
kulia alikuwa amefungwa mkufu mwembamba uliokuwa ukimeremeta.
Kwa kweli alikuwa amependeza
na kutamanisha.
Alikuwa amefunikwa mtandio
uliokuwa unaonya. Hivyo niliweza kuyaona macho yake yaliyokuwa yamepakwa wanja
mzito mweusi huku yakiwa na kope ndefu mithili ya kope za bandia.
Nyusi zake pia zilikuwa zimeongezewa
msitari wa wanja uliopinda juu ya macho yake mithili ya pindi za mvua.
Aliniomba nimfunue ule
mtandio, nikaushika kwa uoga na kuufunua. Akaniambia.
“Asalaam alaykum mume wangu” Wakati
akinipa salaam hiyo alikuwa akinipa mkono.
“Wa alayka salaam” nikamjibu
na kushikana naye mkono.
Mkono wake ulichorwa maua kwa
kutumia piku na hina. Ulikuwa umeota malaika marefu yasiyo ya kawaida.
“Salaam yako ina kasoro,
sikuipenda” Maimun akaniambia wakati tumeshikana.
“Kwanini?” nikamuuliza.
“Nimekusalimia asalaam
alaykum mume wangu. Ulipaswa kujibu wa alayka salaam mke wangu”
“Samahani. Ni kweli nimekosea”
“Sasa nijibu kwa usahihi”
“Wa alayka salaam mke wangu”
Maimun akakibusu kiganja cha
mkono wangu kisha akaniambia.
“Karibu chumbani”
“Asante” nikamjibu.
Kusema kweli nilikuwa
nimenywea kama vile kile chumba hakikuwa changu.
Yule mtu aliyenisindikiza mle
chumbani akaniambia.
“Kama umeshaonana na mke
wako, mimi nakwenda zangu”
“Wewe nenda, muache” Maimun
akanijibia.
Yule mtu alipotoka Maimun
akajilaza kitandani na kuniambia.
“Huu ni wakati wako. Karibu
tujipumzishe…..”
Mkono wenye ngozi laini kama
ya mtoto mchanga uliokuwa ukipapasa kifua changu ndio ulioniamsha kutoka usingizini.
Nikafumbua macho yangu na kuisikia sauti ya Maimun ikiniambia.
“Amka mume wangu, kumekucha”
Maimun alikuwa amesimama
kando ya kitanda mkono wake ukiwa kwenye kifua
changu. Sikuweza kujua alikuwa ameondoka muda gani hapo kitandani lakini
wakati ule ananiamsha kulikuwa kumeshakucha.
“Amka ukaoge,
nimeshakuandalia kifungua kinywa” akaniambia.
Nikaitenga shuka na kushuka
kitandani.
“Utaoga maji ya moto?” Maimun
akaniuliza.
“Hapana, ninaoga maji baridi
tu”
Niliingia naye bafuni tukaoga
pamoja. Baada ya kuoga Maimun akanikaribisha mezani nipate kifungua kinywa
alichokuwa ameniamndalia. Ile vurugu pale nyumbani haikuwepo tena.
Nyumba ilikuwa kimya na
hakukuwa na mgeni yeyote aliyekuwa amebaki. Sikuweza kujua wageni wale
waliokuwepo usiku waliondoka saa ngapi.
Kitu kilichoonesha kuwa usiku
uliopita kulikuwa na sherehe ni mapambo yaliyopambwa mle ndani ambayo bado
yalikuwepo.
Baada ya kupata kifungua
kinywa pamoja na Maimun tulirudi chumbani ambapo Maimun alifungua kabati. Hilo
kabati lilikuwa moja ya vitu vilivyoletwa usiku uliopita. Halikuwa lile kabati
langu.
Maimun alipolifungua kabati
hilo, upende mmoja ulikuwa umepangwa
nguo zake, upande mwingine ulipangwa nguo zangu.
Katika sehemu ya chini ya
kabati hilo kulikuwa na sanduku la chuma. Maimun akanipa funguo na kuniambia nilifungue
sanduku hilo. Nikalifungua na
kupatwa na mshituko.
Sanduku hilo lilikuwa na
tabaka tatu. Tabaka ya kwanza ilikuwa imepangwa maburungutu ya noti nyekundu za
Kitanzania. Zilikuwa noti nyingi na mpya zilizozonesha kama zilitoka benki
kwani bado zilikuwa zimefungwa mfungo ule
ule wa kibenki.
Tabaka la pili lilikuwa
limejaa mapambo ya dhahabu, mikufu, bangili, vipuli na vitu vngine.
Tabaka la tatu lilikuwa na maburubgutu ya noti lakini hazikuwa za Kitanzania.
Zilikuwa ni dola za Kimarekani.
Nikamtazama Maimun kwa
mshangao.
“Hizo ni za kutumia hapa
nyumbani. Zikiisha ninaweka zingine” Maimun akaniambia.
Nikageuza tena uso wangu na
kuzitazama zile noti nilizoambiwa kuwa ni za kutumia.
“Bado kuna pesa za miradi
ambazo nitakupa” Manuna aliendelea kuniambia.
Akilini mwangu niljiambia
kuwa nimeshakuwa tajiri.
“Chukua kiasi unachotaka
uweke mfukoni mwako”
“Nichukue dola au hizi za Kitanzania?’
“Chukua unazotaka”
“Kuna miradi mingi ambayo
ninataka kuianzisha”
No comments:
Post a Comment