ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA
BABU 37
ILIPOISHIA
Siku nilipogundua hilo
nilimuuliza.
“Hivi wewe Maimun hulali usiku?”
“Sisi majini hatulali, tunakuwa
macho tu” akanijibu.
“Kwaninini?”
“Ndiyo maumbile yetu”
“Kumbe usiku nalala peke yangu?”
“Ukilala mimi nakulinda”
Kuna siku moja aliniamsha saa
nane usiku akaniambia nichukue shepe kisha nitoe gari. Baada ya kulitia shepe
kwenye gari nililitoa gari. Maimun akajipakia na kukaa kando yangu.
“Twende Kigamboni”
akaniambia.
“Kuna nini?” nikamuuliza.
“Wewe twende tu”
Nilikwenda kukutana na
maajabu ambayo sitayasahau katika maisha yangu.
SASA ENDELEA
Tulifika Kigamboni kama saa
nane na nusu hivi. Ilielekea Maimun alikuwa akilijua vizuri eneo hilo kwani
aliniongoza hadi sehemu ambayo ilikuwa na pori.
Akaniambia niingize gari
katika pori hilo. Sikumuelewa halafu pia nilipata hofu kidogo. Nikafunga breki
na kumuuliza.
“Kwani tunakwenda wapi?”
“Wewe twende tu”
“Lakini huku unakoniambia
twende hakuna njia”
“Mimi pia nina macho, ninaona
kuwa hakuna njia. Ingiza gari hivyo hivyo”
“Unataka tutokee wapi?”
“Kassim mbona mbishi sana?”
“Mahali kuna pori, unaniambia
niende! Njoo uendeshe wewe”
“Kumbe huniamini?”
“Ninakuamini. Tatizo nini kuwa
siwezi kuendesha gari kwenye pori na pia sijui tunakwenda wapi”
“Kwahiyo turudi?”
“Tusirudi. Nimekwambia njoo
uendeshe wewe”
“Inaelekea wewe ni muoga
sana!”
Hapo sikumjibu. Nikanyamaza
kimya kwani ukweli ni kuwa uoga pia nilikuwa nao.
“Shuka unipishe hapo kwenye
sukani” Maimun akaniambia.
Nikafungua mlango na kushuka.
Kulikuwa na gari ambayo
ilikuwa nyuma yetu ikatupita na kusimama mbele yetu.
Wakati ule nafungua mlango
nikaona ninavamiwa na mtu mmoja miongoni mwa wanne waliotoka kwenye lile gari.
Mtu huyo alinishikia bastola na kunitia kabari kwa nyuma. Mtu mwingine
alifungua mlango wa upande aliokuwa Maimun akamwambia.
“Shuka haraka!”
Maimun akashuka kwenye gari.
“Mnataka nini?” Maimun
akiwauliza.
Mimi nilikuwa
nimeshadhibitiwa. Mkono ulionitia kabari ulikuwa ukinikaza na kunifanya
nisifurukute hata kidogo. Mdomo wa bastola ulikuwa ukitekenya shavu langu la
kulia.
Sikuweza kujua watu wale
walikuwa kina nani na walikuwa wanataka nini.
Kulikuwa na watu wengine
wawili ambao walikuwa wamefungua milango ya ile gari kama vile walikuwa
wakitafuta kitu.
“Mnakwenda wapi?” Yule mtu aliyemtoa
Maimun kwenye gari akamuuliza Maimun.
“Nyinyi ni majambazi sio?”
Maimun akawauliza.
Yule mtu alitaka kumpiga
Maimun kibao, bila shaka kwa vile alivyowambia ni majambazi. Maimun akatoweka
ghafla mbele yake. Kibao kikakata hewa.
Maimun akaibuka tena mahali pale pale. Nikamsikia akitoa mlio kama wa fataki
inayopaa juu huku na yeye akirefuka kwenda juu.
Wakati ule mmojawao, alikuwa
ameshajipakia kwenye gari kwenye siti ya dereva. Nikahisi walitaka kutupora
lile gari.
Lakini kitendo cha Maimun kurefuka
kiliwashitua. Maimun aliendelea kurefuka akafikia kimo cha mnazi!
Nikawasikia wale watu
wakisema kwa fadhaa. “Ha! Ha1 Ha!”
Yule aliyenitia kabari
aliniachia akakimbilia kwenye gari lao. Yule aliyetaka kuendesha lile gari letu
alitoka kwenye gari na kukimbia lakini yule aliyetaka kumpiga Maimun kibao
alinata pale pale.
Wale waliokimbilia kwenye
gari walikwama baada ya Maimun kupiga hatua moja na kutinga mbele ya gari hilo.
Mtu mmoja alianguka hapo hapo. Wengine wakakimbia kwingine na kuliacha gari.
Baada ya tukio hilo nikauona
mwili wa Maimun umerudi vile vile kama ulivyokuwa mwanzo.
Akaja kwenye gari letu upande
wa dereva na kuniambia.
“Ingia garini twende”
Nikazunguka kwenye mlango wa
upande wa pili na kujipakia. Yule mtu aliyenata alikuwa bado amesimama pale
pale, mkono wake mmoja akiwa ameunyoosha mbele kama vile anampiga mtu kibao.
Maimun alikuwa ameshaingia
kwenye gari akaliondoa na kuliingiza kwenye pori.
Kile kitendo cha Maimun kujirefusha,
hata mimi kilinishitua kwani katika maisha yangu sijawahi kuona mtu akirefuka
kwenda juu akafikia kimo cha mnazi.
Mpaka wakati ule nilikuwa
bado nikitweta.
“Umewaona wapumbavu wale?”
Maimun akaanza kuniambia akionekana alikuwa amekasirika.
“Nimewaona lakini sikujua
walikuwa ni kina nani”
“Wale ni majambazi, walitaka kulipora hili gari.
Walitufuata kuanzia mbali sana. Nilishawaona lakini sikukwambia”
“Kwa hiyo walitaka watuue?”
“Sasa kama walitutolea
bastola, unadhani walikuwa wana maana gani nyingine?”
“Lakini wametishika!”
“Walivyonuona ninakuwa mrefu
sio?”
“Ndiyo. Hata mimi
nimetishika”
“Wewe mume wangu pia
unatishika?”
“Sijawahi kukuona ukiwa
vile!”
“Acha vile naweza kujirefusha
mpaka ukawa hujui nimefikia wapi!”
“Sasa unafanyaje?”
“Ni namna yetu. Naweza pia
kujigeuza mnyama kama vile punda au joka kubwa”
“Lakini sitapenda ufanye
hivyo mbele yangu”
“Nikifanya mbele yako ndipo
utakaponizoea”
“Eh! Nitaogopa sana”
“Utazoea tu. Utaogopa mwanzo,
mwisho utakuwa huogopi tena”
“Sasa yule mtu aliyetaka
kukupiga kibao, ataendelea kubaki pale hadi lini?”
“Atajua mwenyewe, achana
naye”
Maimuna aliendesha gari huku akikata
kona ndani ya msitu hadi tukatokea mahali ambapo palikuwa na mawe makubwa sana
yaliyotokea ardhini.
Akalisimamisha gari na
kuniambia tushuke. Tukashuka. Palikuwa
ni mahali panapotisha usiku huo lakini kwa vile nilikuwa na Maimun sikuwa na
hofu sana. Nilijua kama kutatokea tatizo atanisaidia.
“Toa lile shepe nyuma ya
gari” akaniambia.
ITAENDELEA kesho hapahapa Usikose uhondo huu
No comments:
Post a Comment