ZULIA LA FAKI
NILIKIONA CHA MTO URITHI WA
BABU 34
ILIPOISHIA
“Mwenzako amekudanganya.
Amekwambia mimi ni mbaya kwa maana yake. Alikuleta huku ili akuue. Ile dawa
aliyokupa kwenye kikombe haikuwa dawa. Ilikuwa ni sumu. Kama ungekunywa ungekufa pale pale! Mimi ndiye
niliyekibeta kile kikombe”
Hapo ndipo nilipogutuka.
“Kumbe alikuwa ananipa sumu?”
“Alikuwa anakupa sumu akuue.
Ukishakufa alitaka anichukue mimi niwe
mke wake ili apate utajiri”
“Ndiyo maana aliniambia tuje huku shamba!”
“Sasa ndiyo ujue kuwa
ulichofanya kilikuwa ni upuuzi. Kwanini ulikuja kumueleza siri ya mimi na wewe?”
“Nilikuja kumtaka ushauri,
ndio akaniambia kuwa wewe ndiye uliyemuua babu yangu na utaniua na mimi. Kwa
hiyo alitaka akuondoe”
“Shiit…! Mimi nimuue babu
yako kwa kosa gani wakati nilimchunuka mwenyewe. Babu yako alikufa kwa sababu alikuwa mzee.
Angeendelea kuishi hadi lini?”
SASA ENDELEA
“Basi alinaimbia umemuua
wewe”
“Yale yalikuwa maneno ya
uchochezi yenye lengo la kutaka unichukie mimi na ukatae kunirithi” Maimun
aliniambia kwa huzuni kisha akaongeza.
“Ni mganga mwenye roho mbaya
sana. Kama mimi ni mbaya mbona alinitaka yeye?”
Nikanyamaza kimya nikifikiria
kwamba kama si mwanamke huyo ningekuwa nimeshauawa kwa sumu.
“Unajua hukupaswa kuwaeleza watu
kila kitu. Babu yako alikuwa msiri sana. Hakuwa na mtu
yeyote aliyejua kama alikuwa na mke jini. Hata yule mganga wake
hakumwambia”
“Ni kweli nilikosea”
“Sasa acha tabia ya kuwaeleza watu habari zangu. Utakuja
kuuawa bure”
“Yule mganga sitamuamini
tena”
“Kwani nani alikwambia kwamba
ataamka tena?”
Nikashituka.
“Hataamka tena?”
“Ile ndiyo safari. Nilikubeba
wewe kile kikombe kisha nikampiga kibao. Alijiona anapigwa lakini hajui anapigwa na nani. Hataamka tena. Ile ndiyo safari!”
“Niloimuona amekakamaa”
“Hivi ndivyo ninavyomfanya
mtu mpumbavu. Kama ni mganga kweli mwenye majini, mbona hawakunizuia nisimpige? Yule hawezi kunichukua
mimi. Mimi ni jini wa kweli kweli. Sio vijini vyake ochwara!”
Kikapita kimya cha
sekunde kadhaa nikiyawazia maneno ya Maimun.
“Sioni haja ya kusubiri
ujiandae au ufikirie. Unajiandaa kwa lipi au unafikiria nini? Leo utanirithi na ninakuwa mke wako. Sasa
twende madukani tukanunue nguo kwa ajili ya sherehe yetu ya usiku” Maimun
akaniambia ghafla.
“Tutakuwa na sherehe leo
usiku” nikamuuliza.
“Ndiyo, sherehe ya kuoana
kwetu”
“Itafanyika wapi?”
“Itafanyika nyumbani kwako
usiku”
“Itakuwa ni sherehe ya namna
gani?”
“Sherehe kama sherehe yoyote
ya ndoa. Nitawaalika wageni wangu kutoka kwetu lakini wewe usialike mtu.
Itakuwa sherehe ya majini”
“Kwani haitaki maandalizi?”
“Mimi mwenyewe nitaandaa kila
kitu”
Nikabaki nimeduwaa.
Ningemjibu nini Maimun anayeua watu kwa vibao?
Ilibidi nimkubalie kila alichosema.
Nikampitisha katika maduka
makubwa ya nguo. Akanunua vitu pamoja na nguo zake na zangu. Alijaza masanduku
mawili ya nguo zenye thamani na kuyapakia kwenye gari. Pesa zilizomtoka zilikuwa karibu shilingi milioni
ishirini na tano!
Ile ‘shopping’ ilinitisha
hata mimi. Kununu nguo zenye thamani kubwa kiasi kile kwa wakati mmoja halikuwa jambo dogo. Niliamini kuwa
kweli yule mwanamke alikuwa na utajiri, si mchezo.
Tulirudi nyumbani kwangu na yale masanduku. Maimun
akaniambia siku ile nisiondoke kwenda popote. Nikatii agizo lake nikashinda
nyumbani hadi jioni lakini yeye aliondoka. Usiku nilitoka mara moja kwenda kula
chakula halafu nikarudi kulala.
Yapata saa nae usiku, mlango
wa chumba changu ukabishwa. Nikasikia
sauti za watu ukumbini. Sikupata hofu
kwa vile Maimun aliniambia sherehe zitafanyika usiku. Nikaamka na kwenda
kufungua mlango.
Niliona wasichana wawili
waliokuwa mbele ya mlango. Sikuwa na
shaka kwamba wasichana hao walikuwa majini kwani walikuwa wazuri sana.
“Wakati umewadia. Unatakiwa
uoge uvae joho lako alilokununulia dada, ujifunge na kilemba halafu ujitie
manukato” Mmoja wa wasichana hao wakaniambia.
Nikarudi chumbani na kuingia
bafuni. Nilioga na nilipomaliza nilitoka nikavaa ‘Panjabi’ aliyoninunulia Maimun kisha
nikajitia manukato.
Nikatoka bila kuvaa kilemba
kwani nilishindwa kukifunga. Nilikuwa nimekishika mkononi.
Wale wasichana wawili
walikuwa bado wako kando ya mlango kama maaskari. Waliponiona ninatoka, mmoja alinishika mkono akanirudisha
chumbani.
“Usitoke hivi hivi, dadada
atagomba” akaniambia na kunifunga kile kilemba.
Baada ya kufungwa kilemba
hicho nilijitazama kwenye kioo. Nilijiona nilikuwa kama ‘Mpakistani’ anayejiandaa
kwanda kuswalisha.
Nyumba yangu ilikuwa
imepambwa vilivyo. Mapazia yalikuwa yamewekwa mengine. Taa zilikuwa
zimebadilishwa na kuwekwa taa za rangi
mbalimbali na zisizo na mwanaga mkali.
Niliona watu mbalimbali, wake kwa waume,
wakishughulika. Maimun aliniambia mchana kuwa ataalika wageni kutoka kwao. Nikahisi
wageni wenyewe ndio wale niliowaona hapo.
Nikapelekwa sebuleni. Sebule
ilikuwa imebadilishwa. Makochi yangu yaliondolewa na kuwekwa makochi mengine ya
chini chini. Nilikuta watu wawili, mmoja akiwa mzee mwenye ndevu nyeupe ambaye
alikuwa amevaa joho na kilemba cheupe.
Pembeni yake palikuwa na
chetezo kilichokuwa kinafuka moshi
uliokuwa unanukia ubani uliochanganya na udi wa mawaridi, wengine huuita udi wa
Unguja.
Sebule nzima ilikuwa ikinukia
udi wa mawaridi.
“Kaa hapa” yule mzee
aliyekuwa amevaa joho akaniambia akinionesha sehemu iliyokuwa mbele yake.
Nilipokaa tu akaniambia.
“Lete mkono wako”
Nikampa mkono.
“Unaitwa nani?” akaniuliza.
ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu
No comments:
Post a Comment