Monday, June 5, 2017

SIMULIZI, NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU SEHEMU YA 36

NILIKIONA CHA MOTO URITHI WA BABU 36
 
ILIPOISHIA
 
“Nimekwambia hizo si za miradi. Hizo ni za kutumia tu. Pesa za miradi nitakupa baadaye”
“Sawa. Ngoja nichukue milioni moja”
 
“Chukua hata mbili”
 
Nikatia mkono na kuchukua burungutu moja ya zile noti za Kitanzania.
 
“Si unataka milioni mbili, chukua mawili”
 
Nikatia tena mkono na kuchukua burungutu jingine.
 
“Sasa funga hilo sanduku”
 
Nikalifunga. Maimun akanipa ufunguo wa sanduku hilo.
 
“Funguo utakaa nayo mwenyewe” akaniambia.
 
SASA ENDELEA
 
Aliponiambia hivyo, kwa bumbuwazi lililonipata kufuatia kuwa na pesa nyingi kiasi kile nikabaki nikimuangalia Maimun.
 
“Vipi mume wangu, mbona umetulia unaniangalia?”
 
“Unajua siamini macho yangu. Kwa hiyo pesa zote hizi nizitumie?”
 
 
Nilipomuuliza hivyo Maimun alitoa  kicheko laini akaniambia pesa zote zile zilikuwa zangu. Hivyo naweza kuzitumia kununua chochote nitakachotaka.
 
“Nakushukuru sana mke wangu”
 
Maimun aliachia tabasamu kabla ya kuniambia kuwa kulikuwa na jambo muhimu alinieleza.
 
“Sijui kama  unalikumbuka?”
 
“Nimesahau mke wangu ni jambo gani hilo?”
 
“Mume wangu jamani! Naona furaha yako imepita kiasi mpaka umesahau jambo muhimu nililokueleza. Kweli umesahau au unataka tu nikueleze tena?”
 
“Siyo hivyo mke wangu, ningekumbuka ningekwambia. Naomba unikumbushe maana umeniacha njia panda mwenzio”
 
SASA ENDELEA
 
“Haya njoo hapa kitandani nikueleze tena” Maimun akaniambia. Kidogo nilipatwa na wasiwasi. Nikamfuata.
 
“Mbona hujafunga kabati?” Maimun akaniuliza na kuongeza.
 
“Funga kabati kwanza ndio uje”
 
Nikarudi kunako kabati. Nikalifunga kisha nikaenda pale kitandani ambako  Maimun alikuwa ameketi.
 
Maimun akauzungusha mkono wake mmoja kwenye shingo yangu, mkono mwingine ukawa unapapasa kifua changu.
 
“Kassim una manyoya marefu kifuani!” akaniambia halafu akawa anacheka kama mtoto
 
Aliendelea kunipapapasa huku akiendelea kusema peke yake.
 
“Utadhani jini…!”
 
Aliposema hivyo aliangua kicheko kabisa.
 
“Hivi majini wanakuwa  na manyoya marefu?”  nikamuuliza.
 
“Hunioni mimi?” akaniambia huku akinionesha mikono yake ambayo ilikuwa na malaika marefu.
 
Akaendelea kunionesha miguu yake.
 
Ingawa alinionesha miguu na mikono lakini kifuani kwake kulikuwa na manyoya zaidi. Niliyaona usiku uliopita.
 
“Nilidhani ni wewe tu” nikamwambia.
 
“Hapana, hivi ndivyo tulivyo. Tena mimi ni mafupi lakini majini  wenzangu wana manyoya marefu sana”
 
“Kwa hiyo unapenda malaika marefu?”
 
“Sana”
 
Maimun aliposema neno ‘sana’ aliurudisha mkono wake kwenye kifua changu.
 
Mbona hujaniambia hilo jambo muhimu ulilotaka kunieleza”
 
“Ni kukukumbusha tu, nilishakwambia jana kwamba sitaki siri yangu uitoe nje. Hizi pesa  ninazokupa  ziwe siri yako na bado nitakupa  nyingi zaidi. Sitaki nikuone unamueleza mtu kwamba mke wako ni jini na anakupa  pesa. Umenielewa?”
 
“Nimekuelewa”
 
“Siku nikikusikia ukimwambia mtu habari zangu ujue umenivunjia mwiko wangu. Sawa”
 
“Sawa mke wangu. Sitamueleza mtu.  Kwanza nimueleze mtu ili iweje?”
 
“Mimi nazijua tabia za binaadamu. Wengine wanapenda sifa sana. Na sifa haifai”
 
“Ni kweli lakini mimi sina tabia hiyo”
 
“Nataka nikukumbushe kitu kiingine kwamba usiwe  na mahusiano na mwanamke yeyote na kama ulikuwa naye umuache”
 
Hapo nikanyamaza kidogo. Nikamfikiria msichana wangu mmoja ambaye ndiye niliyekuwa nimepanga kuoana naye.
 
“Mbona umenyamaza?” Maimun akaniuliza.
 
“Sikufichi. Kuna msichana mmoja ambaye nilikuwa na uhusiano naye na tulikuwa tumepanga kuoana…”
 
Nilikuwa sijamaliza sentensi yangu,  nikauona uso wa Maimun ukiwa mwekundu mpaka niliogopa.
 
“Unasemaje?” akaniuliza huku akiwa amekunja  uso.
 
“Nilikuwa nataka kukueleza kwamba huyo msichana itabidi  niachane naye…”
 
Maimun akabaki kunitazama. Hata hivyo kwa vile nilikuwa nimeshamzoea nikamshika kiuno chake na kumvuta upande wangu. Wakati namvuta alikuwa laini kama si yeye aliyekuwa amekasirika.
 
“Unakasirika nini” nikapata ujasiri wa kumuuliza nikiwa nimemkumbatia.
 
“Sitaki shirika. Siku nikikufuma naye ujue ninamuua” akaniambia kwa sauti ya kudeka kama ya mtoto mdogo. Hasira zilikuwa zimeshamtoka.
 
“Hutonifuma naye ila itabidi nimueleze kuwa sitaoana  naye tena”
 
“Kwa hilo  ninakuruhusu”
 
“Yaani Maimun unafikiri mimi ni mjinga sana, nikupate wewe mrembo ambaye unanipa utajiri halafu nitafute mwanamke mwingine wa kunifilisi!”
 
Maneno hayo yakamfurahisha Maimun ambaye bado nilikuwa nimemkumbatia.
 
“Si kukupa utajiri tu, pia nakupa mapenzi adhimu” akaniambia kwa kunilegezea sauti.
 
“Ni kweli. Sasa baada ya hayo yote nitafute nini tena kwa mwanamke mwingine?”
 
Sikujua Maimun alipandwa na mori gani, akanipindua kitandani kisha akanikalia juu.
 
“Hutatoka humu chumbani leo. Nakwambia tutashinda humu humu nikuoneshe mahaba ya kijini” akaniambia.
 
Ni kweli siku ile siikutooka nje. Kumbe babu yangu alikuwa akifaidi! Majini wanajua mapenzi ya kweli. Kuoana na Maimun kuliniingiza katika enzi mpya katika maisha yangu, enzi ya mapenzi adhimu.
 
Mapenzi yetu hayakuwa chumbani tu, yalikuwa mahali popote, kwenye chakula, kwenye kuoga na hata kwenye mazungumzo.
 
Kitu ambacho niliokiona kilikuwa kero ni wivu wa mwanamke huyo.  Alikuwa na wivu wa kupindukia. Siku akiamua nisitoke nyumbani,  sitoki. Nitashinda naye chumbani mchana kutwa.
 
Siku ambayo ninapomuudhi anakasirika mchana kutwa. Anakuwa hataki kusema na mimi lakini siku akifurahi atakuenzi mpaka basi.
 
Saa moja asubuhi Maimun anakuwa ameshanitayarishia kifungua kinywa. Saa sita mchana ameshatayarisha chakula cha mchana.  Chakula cha  usiku kinakuwa tayari saa mbili.
 
Vyakula ambavyo Maimun alikuwa akivipenda ni uji uliochanganywa na nyama ya mbuzi, anauita ‘shurba’ Pia hupenda  chai ya maziwa, chapatti, mkate wa mchele, pilau ya kuku, biriani na wali kwa maziwa ya mgando.
 
 
Vitu ambavyo alipenda kuvinunua kila siku ni aina  za manukato. Kwenye kabati letu kulikuwa na chupa karibu ishirini za manukato tofauti tofauti.
 
Alikuwa akipenda kuoga. Mchana mmoja alioga karibu mara sita na akiingia bafuni huchukua muda mrefu kutoka. Ngozi yake ilikuwa safi na laini kama ngozi ya mtoto mchanga.
 
Kuna kitu kimoja nilikuja kukigundua kwamba Maimun alikuwa halali usingizi. Ninapolala naye usiku anafanya geresha tu.  Ninapopitiwa na usingizi mwenzangu anabaki macho akiwa na kazi ya kuniamgalia tu. Wakati mwingine hushuka kitandani na kwenda kukaa sebuleni usiku kucha.
ITAENDELEA kesho hapahapa usikose uhondo huu.

No comments:

Post a Comment