Monday, January 5, 2015

KISIWA CHA CHA HARISHI (26)

HADITHI
 
KISIWA CHA HARISHI (26)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
“Yasmin tumeepuka kifo cha aina moja, sasa tunakabiliwa na kifo cha aina nyingine” nikamwambia Yasmin.
 
“Kifo gani tena?”
 
“Tutaondokaje kwenye kisiwa hiki?”
 
“Usijali. Mungu mkubwa”
 
Tukarudi katika lile jumba. Tulipofika tulioga maji baridi. Yasmin alinitolea “Ni kwa nguo za kiume alizokuwa akiletewa na Harishi, akaniambia nivae.
 
Kwa vile kulikuwa kumeshakucha alipikauji aliouchanganya na asali, tukanywa. Kwa sababu moyo wangu ulikuwa umetulia nilikunywa vikombe vitatu.
 
Wakati nakunywa kikombe cha tatu Yasmin akaniambia.
 
“Leo umekunywa uji mwingi kuliko siku zote!”
 
sababu nina njaa na roho yangu imetulia”
 
“Yasmin akacheka.
 
“Jana hukutaka kula kabisa!” akaniambia.
 
“Ni kwa sababu ya yule mshenzi, alinisababishia hofu sana”
 
“Sijui ulipata wapi akili ya kufunga kile kizibo?”
 
“Niiona tu akili yangu ikinituma nikifunge nilipoona ule moshi”
 
“Pengine ni kwa sababu ya zile dua ulizokuwa ukiomba tangu juzi”
 
“Pengine”
 
SASA ENDELEA
 
Wakati tunajadiliana na Yasmin tulishituka tulipoona wazungu wawili wanaume namtu mweusi mmoja wakiingia ndani ya ile nyumba.
 
Nguo zao zilikuwa zimeroa maji. Walionekana walikuwa wamatoka baharini.
 
Tukapatwa na uoga kwa vile hakukuwa na watu waliokuwa wakifika katika kisiwa kile.
 
Tulikuwa tumekaa pale ukumbini Yasmin akanyanyuka na kuwauliza kwa Kiswahili.
 
“Nyinyi ni kina nani”
 
“Samahani jamani. Tumekuja kuomba msaada” Yule mtu mweusiakatuambia.
 
“Mnatoka wapi?”
 
“Tunatoka Zanzibar. Chombo chetu kilipigwa na dharuba kimepinduka. Tumeogelea hadi tumetokea katika kisiwa hiki”
 
“Nyinyi ni kina nani” Yasmin akawauliza tena.
 
“Hawa wenzangu ni watalii wanatoka Ufaransa. Mimi ni Mzanzibari. Nilikuwa nawatembeza kwa boti kwenye Bahari ya Hinndi ndio tukapatwa na ajali”
 
“Mimi pia najua Kifaransa, ngoja niwaulize” Yasmin akasema  na kuwageukia wale wazungu. Aliwauliza maswali kwa kutumia lugha ya Kifaransa. Wazungu hao walimjibu na kufurahi kuona Yasmin alikuwa akizungumza lugha yao.
 
“Karibuni make” Yasmin akawambia kwa Kifaransa.
 
Watu hao watatu wakakaa chini.
 
“Kwanza tunawapa pole sana kutokana na mkasa uliowafika. Mmesema kuwa mnaomba msaada, mtufahamishe mnaomba msaada gani?” Yasmin aliwauliza.
 
Msaada wowote tu unaostahili kwa binaadamu kwani tumezunguka sana katika kisiwa hiki hatukuona mtu yeyote. Tulichoona ni nyumba tupu na kwingine tulikuta mafuvu na mifupa ya bianaadamu” Mzanzibari alisema.
 
“Ni kweli” Yasmin alimjibu.
 
“Ni kwanini?”
 
“Kwanza mlitakiwa mshukuru kuwa mmefika katika kisiwa hiki katika muda mzuri, vinginevyo na nyinyi mngekuwa kama yale mafuvu mliyoyaona”
 
“Kwa niaba ya wenzangu nasema kuwa tumeshukuru lakini tuna shauku ya kutaka kujua kilichotokea mpaka mkabaki nyinyi peke yenu”
 
“Nitawaeleza”
 
Ndipo Yasmin alipoanza kuwaeleza kisa cha kisiwa hicho. Alianza kwa kujitambulisha kuwa yeye ni binti wa Rais wa Comoro na jina lake ni Yasmin. Akawambia kwamba alisoma elimu yake nchini Ufaransa na ndiyo sababu akawa anajua kuzungumza Kifaransa.
 
Akaeleza alivyoposwa na mwana wa mkuu wa majeshi nchini mwao lakini siku ile ya harusi akakumbwa na jini anayeitwa Harishi ambaye alimpeleka katika kisiwa hicho na kumgeuza mke wake.
 
“Sikujua nilivyofika katika kisiwa hiki. Nilijishitukia tu nikiwa ndani ya jumba hili nikiwa sijielewi” Akasema.
 
Watu hao watatu, wazungu wawili na Mzanzibari mmoja walishikwa na mshangao mkubwa kusikia habari ile.
 
Yasmin aliendelea kuwaeleza kuwa jini aliyemkumba ndiye aliyekuwa akiua watu katika kisiwa hicho kwa kuwafyonza damu na kula ubongo wao.
 
“Aliwamaliza watu wote waliokuwa katika kisiwa hiki na kuacha majumba yakiwa matupu. Niliishi peke yangu kwa karibu mwaka mzima” Yasmin alieleza.
 
Aliendelea kuwaeleza jinsi tulivyofika katika kisiwa hicho na kumkuta yeye ndani ya jumba hilo na jinsi tulivyoanza kuuawa na Harishi mmoja mmoja hadi nikabaki peke yangu.
 
Ni dhahiri kuwa maelezo ya Yasmin yalikuwa yamewatia hofu watu hao kwani nyuso zao zilizidi kupata fadhaa.
 
“Mungu ni mkubwa” Yasmin alisema kabla ya kueleza jinsi walivyofanikiwa kumfungia Harishi kwenye chupa na kwenda kuizamisha baharini asubuhi ile.
 
“Hiki ni kisa cha ajabu kweli kweli. Je tunaweza kwenda kuiona hiyo chupa? mzungu mmoja akauliza.
 
“Hatuwezi kujua tumeizamisha wapi lakini kwa sasa Harishi yuko chini ya Bahari”
 
“Je hao watu waliouawa tunaweza kuwaona?”
 
“Hao mnaweza kuwaona”
 
“Tunaomba mtupeleke tukawaone kama hamtajali”
 
Yasmin akanitazama.
 
“Umeridhika twende tukawaoneshe hawa wageni miili ya ndugu zako?” akaniuliza.
 
“Nimeridhika” nikamjibu.
 
Yasmin akawambia wale watu “Twendeni”
 
Tukaondoka sote watu wanne. Yasmin alianza kuwaonesha miili ya wenzetu waliouawa ambayo ilikuwa karibu na lile jumba. Walikuwa ni wale wenzangu waliouawa mwanzo mwanzo.
 
Yasmin alikuwa akieleza jinsi watu hao walivyokuwa wakiuawa kila siku mmoja baada ya mwingine.
 
Tukaenda mbali zaidi katika ile nyumba aliyouawa Haji. Wazungu hao pamoja na Mzanzibari waliyekuwa naye wakauona mwili wa Haji.
 
Mimi nilitakiwa kueleza alivyouawa Haji. Nikaeleza kwa Kiswahili huku Yasmin akitafsiri kwa kKifaransa.
 
Baada ya hapo tulikwenda katika nyumba aliyouawa Shazume.
Tuliwaonesha mwili wa Shazume na nikawaeleza jinsi Shazume alivyouawa.
 
“Hapa ndipo nilipokata tamaa kabisa. Nilijua na mimi ningeuawa leo” nilisema.
 
Yasmin akaeleza kuwa nay eye alikuwa ameshajitolea kufa kwa ajili yangu.
 
“Nilisema kama atauawa basi tuuawe sote” akasema na kuongeza.
 
“Niliona Hakuna haja ya kuendelea kujificha. Nilimwambia mwenzangu twende kule ninakoishi. Harishi akija atukute sote”
 
Wazungu hao walimsifu Yasmin kuwa alikuwa msichana jasiri na mwenye moyo.
 
“Kumbe na sisi tungekuja kufa!” Mzanzibari naye aling’aka.
 
“Ndiyo maana niliwambia mwanzo kuwa mshukuru kwa kufika katika kisiwa hiki katika kipindi cha usalama” Yasmin akawambia.
 
“Sasa kule nyumbani Comoro wanajua uko wapi?” Yule Mzanzibari alendelea kumuuliza Yasmin.
 
“Wao hawajui niko wapi na kwa sasa wanaamini kuwa nimeshakufa”
 
“Je wakikuona tena itakuwaje?”
 
“Itakuwa mshangao mkubwa. Wazazi wangu hawataamini”
 
“Ni mkasa wa kutisha kweli na unastahili kuandikwa katika historia ya Comoro”
 
“Hapo ni kama tutanusurika na nitarudi kwetu kwani kama niivyowambia mwanzo hapa hatutarajii kupata msaada wowote. Hatima yetu tumemwachia Mwenyezi Mungu”
 
ITAENDELEA KESHO,USIKOSE NINI KITAJIRI KATIKA SEHEMU IFUATAYO KESHO

No comments:

Post a Comment