HADITHI
KISIWA CHA HARISHI
(24)
ILIPOISHIA TOLEO
LILILOPITA
Yasmin akaja kukaa
kando yangu.
“Unajua maisha?”
akaniuliza. Sikujua alikuwa na maana gani.
“Maisha ni nini?”
nikamuuliza.
“Maisha ya mwanaadamu
ni mtihani. Lolote linalokufika liwe zuri au baya ni mtihani kwako. Kama wewe
ni muumini unatakiwa ulijue hilo”
“Ndio ninalijua”
“Mungu hashindwi
kutuokoa sisi waja zake tunaomtegemea yeye ila anatupa mitihani kuona ni kwa
kiasi gani tunaweza kuweka matumaini kwake na kwa jinsi gani tunaweza
kumuomba kwa unyenyekevu katika siku hii ambayo mimi na wewe tunahitaji sana
msaada wake”
Ndani ya moyo wangu
nilikiri kuwa Yasmin alikuwa amenieleza maneno ya maana kuliko aliyowahi
kunieleza wakati wowote. Nilifarijika kuona juhudi zake za kunitia moyo
zilifanikiwa kwa kiasi kikubwa na kuamsha imani yangu.
Nikajiambia laiti kama
ningekuwa na mke kama Yasmin nisingeshindwa kimaisha hata itokee shida ya
kiasi gani.
SASA ENDELEA
Hatimaye jua
lilikuchwa. Giza lilianza kuingia. Yasmin aliwasha taa za nyumba nzima.
Alikuwa ameniacha mle chumbani mwake, akanifuata na kuniuliza. “Utakula
chakula?”
Nikatikisa kichwa.
“Sitakula”
“Hutakula hata kidogo”
Nikaendelea kutikisa
kichwa.
“Sitakula”
Yasmin akakaa karibu
yangu.
“Usiku ndio huu”
akaniambia.
“Kwani Harishi atakuja
muda huu?”
“Anaweza kuja wakati
wowote kutoka sasa hadi alfajiri”
“Anakujaje?”
nikamuuliza Yasmin huku nikiitazama ile chupa iliyokuwa juu ya kabati.
“Anakuja kama moshi.
Unajaa ndani ya ile chupa kisha unatoka. Unapotoka unabadilika na kuwa jini”
“Na ni kwanini anakuja
hivyo?”
Yasmin akabetua mabega
yake
“Sijui lakini ondoa
hofu. Mwisho wa mateso yetu utakuwa leo”
Sikusema kitu tena
nikanyamaza kimya. Tulikaa kimya kwa muda mrefu. Ile shauku ya kuzungumza
ilikuwa imetuishia. Tukaamua kukaa tu kusubiri muda wetu.
Tulikuwa tumekaa chini
tumeelekezana migongo. Kila mmoja alielekea upande wake. Yasmin alipochoka au
kuhisi kusinzia aliuegemeza mgongo wake kwenye mgongo wangu.
Kitu gani kilimfanya
Yasmin asipande kitandani na kulala?
Alikuwa amejitolea
kufa na mimi. Alikuwa ameamua akae na mimi pale chini hadi Harishi
atakapokuja.
Ilikuwa kama saa saba
usiku nywele zangu zilipoanza kunisisimka. Nikayapeleka macho yangu kwenye
ile chupa ya Harishi iliyokuwa juu ya kabati. Moyo wangu ulishituka
nilipoiona chupa inaingia moshi kwa ndani. Nikamgutusha Yasmin aliyekuwa
anasinzia.
“Yasmin!”
“Abee!” Yasmin
akaniitikia.
“Tazama ile chupa!”
Yasmin akageuza uso
wake na kuitazama chupa hiyo.
“Usimuogope kiumbe
aliyeghulukiwa kama wewe. Muogope aliyeghuluku” Ndilo neno aliloniambia
Yasmin.
Ule moshi uliendelea
kujaa ndani ya ile chupa. Kifiniko cha chupa hiyo kilikuwa pembeni. Moyo
haukunipa. Mara moja nikanyanyuka na kwenda kando ya lile kabati. Niisubiri
ule moshi ujae kabisa kisha nikakichukua kile kifiniko na kukifunga kwenye
mdomo wa ile chupa.
Baada ya sekunde
chache nilisikia sauti ya Harishi kutoka kwenye ile chupa.
“Nani amefunga
kizibo?”
Sote tukanyamaza
kimya.
Ile sauti ikasikika
tena.
“We Yasmin si
nilikwambia usifunge hiki kizibo?”
Tukaendelea kunyamaza
lakini moyo wangu ulikuwa ukienda mbio.
“Fungua sasa!” ile
sauti sasa ilifoka.
“Usifungue!” Yasmin
akaniambia huku akinifuata.
“Ahaa! kumbe uko na
hawara yako! Sasa mtanitambua”
“Sifungui!” Yasmin
akasema kwa jazba.
“Nimekwambia fungua,
nataka nitoke!” Sauti ikafoka.
“Toka mwenyewe!” Yasmin
akajibu.
“Yasmin umechoka
kuishi? Nakwambia nitakuua wewe na hawara yako!” Sauti ya Harishi iliendelea
kuunguruma kwa hasira.
“Ndio tunavyotaka
utuue. Tuue sasa hivi!” Yasmin aliendelea kujibu.
“Wewe kijana nani
amekuruhusu ufunge hiki kizibo, hujui kuwa hii ni nyumba yangu?” Sauti ya
Harishi ikaniuliza.
“Nimemruhusu mimi
akifunge. Nimeshachoka na wewe. Kama unaweza kutoka toka mwenyewe utuue. Sisi
tunasubiri kufa tu”
“Yasmin umeamua
kunigeuka leo?” Sauti ya Harishi sasa ilukuwa imerudi chini. “Nifungulie mke
wangu. Nimekuletea zawadi nzuri”
“Sitaki zawadi yako.
Njoo utuue!”
“Nani amekwambia kama
nataka kuwaua?”
“Si ndio kazi yako
kuua watu. Watu wote wa kisiwa hiki si umewamaliza wewe!”
“He he he!” Harishi
alitoa kicheko kilichoonesha wazi kuwa ni cha uongo. Kisha akauliza kwa
ukali.
“Sasa utakifungua
kizibo au hufungui?”
“Sifungui!” Yasmin
akamjibu.
“Wewe kijana fungua
kizibo hicho?’ Sauti ya Harishi ikanigeukia mimi.
“Usifungue. Mwache
atoke mwenyewe. Sisi tumeshajitolea, liwalo na liwe!” Yasmin akaniambia.
Wakati wote nilikuwa
najiuliza kama Harishi alikuwa hawezi kutoka mwenyewe kwenye ile chupa mpaka
atuombe sisi tufungue kizibo. Nikataka kupata uhakika kama kweli Harishi
alikuwa amenasa na asingeweza kutoka bila msaada wetu.
ITAENDELEA KESHO, USIKOSE NINI KITATOKEA
|
|
Friday, January 2, 2015
KISIWA HARISHI
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment