Friday, January 2, 2015

WALALAMIKIA FUNZA KATIKA MIHOGO NA VIAZI



Kumekucha blog, Pemba

Pemba,WAKULIMA wa  kilimo cha Muhogo na viazi vitamu Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba wameilalamikia Serikali kushindwa kulipatia ufumbuzi ugonjwa ulioibuka wa funza kuharibu  zao hilo.

Wakizungumza katika kikao cha mwaka cha kujadili mbinmi na mikakati ya kilimo Wilayani humo leo,wakulima hao walisema kwa zaidi ya mwaka mmoja mdudu huyo amekuwa msumbufu na wakulima wengi wamekuwa wakikosa mazao.

Walisema mbali ya kufuata utaratibu wa kilimo kutoka kwa maofisa mashamba lakini wamekuwa wakishindwa kumdhibiti na hivyo kuitaka Serikali kutuma timu ya wataalamu ili kuweza kumtokomeza funza huyo.

“Ni misimu mitatu toka mdudu huyu aina ya funza ajitokeze katika mazao yetu---hatujui ni namna gani amekuwa akijipenyeza wakati maelekezo yote ya maofis kilimo tunayafuata” alisema Mwadini Fakihi

“Lakini cha kustajabisha ni kuwa mamlaka inayohusika na kilimo tumeshaitarifu ila hakuna kinachoendelea---kwa vile hatuna njia mbadala tunalima kwa matumaini umepata umekosa tunajishukuria” alisema Fakihi

Kwa upande wake mkazi wa Sizini, Ali Kondo amelalamikia wakulima kisiwani Pemba kutokuwa na soko la kuuzia mazao yao na badala yake wamekuwa wakiuza kwa kubahatisha.

Alisema wakulima wengi wamekuwa wakiendesha kilimo hicho kwa mazoea na sio kwa biashara kutokana na kutokuwa na masoko ya uhakika na kuwa sababu ya mashamba ya watu wengi kuwa pori.

“Pemba tatizo letu hatuna soko maalumu la kupeleka mazao yetu kama ilivyo kwa karafuu---ndio maana watu wengi wanalima kwa mahitaji ya mtu nyumbani kwake na ziada kutafuta riziki akipata asipate kwake ni kawaida” alisema Kondo

Alisema ili kumuwezesha mkulima wa kisiwani Pemba ni vyema Serikali ikawa na mkakati maalumu wa kukifanya kilimo kuwa ni zao la pili katika kuingiza pato badala ya karafuu .

Alisema kufanya hivyo itawa wepesi wakulima kisiwani humo na kuondokana na mazoea ya kusubiri msimu wa karafuu ambao kwa sasa soko lake limeanguka katika masoko ya nje.

                                        Mwisho

No comments:

Post a Comment