Friday, January 1, 2016

RC APIGA MARUFUKU MCHEZO WA POOL WAKATI WA KAZI



Tangakumekuchablog
Tanga, MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, amewataka wananchi kujiwekea chakula cha akiba majumbani kwa madai kuwa ni kukabiliana na kitisho cha njaa inayoinyemelea Wilaya za Korogwe  Handeni na Kilindi.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mahiza alisema kuna kitisho cha kuzuka kwa janga la njaa na hivyo kuwataka wakulima kujiwekea chakula ndani na pia kuwataka  wafanyabiashara kuacha kuwalangua wakulima kwa kutumia mtaji wa uhaba wa chakula.
Alisema ofisi yake inafanya mawasiliano na ofisi ya Waziri Mkuu kuomba msaada wa chakula ili kuweza kukabiliana na uhaba huo baada ya  mvua  kuacha kunyesha hivyo wakulima kukosa mavuno ya kutosha.
“Ndugu zangu waandishi wa habari mbali ya kutoa salama za kuingia mwaka mpya ila nifikishieni salamu zangu nyengine kwa wananchi kuwa kukosekana kwa mvua za kutosha kuna hatari ya mkoa wetu kukumbwa na janga la njaa” alisema Mhiza na kuongeza
“Niwatake wananchi na wakulima  kipindi hiki tusiwe na tamaa ya kujipatia pesa kwa kuuza mazao yetu yote  kwani dalili zote za kuzuka  janga la njaa liko karibu, sababu ni uhaba wa mvua za kutosha” alisema
Pia  Mkuu huyo wa Mkoa amepiga marufuku mchezo wa Pool wakati wa kazi kwa madai kuwa magenge hayo ni vituo vikuu vya kuuzia bangi na unga na kulitaka jeshi la polisi na viongozi wa Serikali za mitaa na vijiji kwa pamoja kushirikiana.
Alisema mchezo huo umekuwa ukizalisha wavutaji na wauzaji unga pamoja na kupoteza nguvu kazi za vijana katika kujiletea maendeleo  na hivyo kusema kuwa mchezo huo uchezwe baada ya kazi nyakati za jioni.
“Napiga marufuku mchezo wa pool kuchezwa wakati wa kazi, mchezo huu uko na vishawishi vingi vikiwemo kujihusisha na matumizi ya madawa ya kulevya na njama za uporaji” alisema Mahiza
Alisema zoezi la kupiga marufuku uchezaji wa mchezo wa poll wakati wa kazi ofisi yake inaanza operesheni mtaa hadi mtaa na hivyo kuwataka wamiliki wa mabanda poll kujiwekea utaratibu ili kuepuka mkono wa sheria.
                                                       Mwisho



 Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kuukaribisha Mwaka Mpya pamoja na kupiga marufuku mchezo wa Poll wakati wa kazi na kuwataka wamiliki wa michezo hiyo kutii amri hiyo, kushoto ni Katibu Tawala Mkoa, Salim Mohammed Chima na kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Abdullah Lutavi.

No comments:

Post a Comment