MWANANCHI
Wakati dunia ikiwa na zaidi ya watu 34
milioni wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (VVU), madaktari nchini Hispania
wametangaza kugundua tiba ya ugonjwa huo wanayodai ni uhakika.
Kwa kutumia damu ya kupandikiza kutoka
kwenye kitovu mwana (umbilical cord) cha mtu ambaye ana vinasaba ambavyo
havipokei virusi hivyo vya Ukimwi, wataalamu hao wa tiba wa Hispania
wanaamini kuwa wanaweza kutibu ugonjwa huo baada ya mafanikio waliyopata
kwa mgonjwa mmoja.
Madaktari hao wa Kitengo cha Taifa cha
Upandikizaji (ONT) cha Hispania walichukua damu ya vitovu mwana vya watu
wenye vinasaba ambavyo havipokei VVU na kuipandikiza kwa mtu anayeishi
na virusi hivyo. Baada ya miezi mitatu, mgonjwa huyo alipimwa na
kuonekana hana virusi.
Daktari wa Programu ya Upandikizaji
kutoka Taasisi ya Tiba ya Catalan, Barcelona, Rafael Duarte alisema
mgonjwa aliyetibiwa kwa njia hiyo, Timothy Brown (37), alikuwa anaishi
na VVU tangu mwaka 2009 na madaktari hao walithibitisha kuwa amepona
baada ya kupandikizwa damu hiyo.
Mgonjwa mwingine aliyefanyiwa majaribio ya tiba hiyo alipona VVU, lakini miaka mitatu baadaye alifariki kwa ugonjwa wa saratani.
Timu ya madaktari wa Hispania ililiambia
gazeti la kila siku nchini humo la El Mundo kuwa wana uhakika kuwa
wameleta mapinduzi katika mapambano ya Ukimwi na magonjwa yanayofanana
na hayo.
Dk Duarte alisema mwaka 2015 umekuwa wa
kujivunia ugunduzi huo mkubwa duniani, ingawa alitahadharisha kuwa tiba
kamili haiwezi kupatikana katika siku za usoni.
Kaimu mkurugenzi wa mwitikio wa Taifa wa
Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids), Dk Morris Lekule alisema
utafiti kama huo hauna budi kufuata taratibu zote na kuthibitishwa na
Shirika la Afya Duniani (WHO) kabla ya kutangazwa kuwa ni tiba sahihi.
“Kila mara taarifa zinakuja zikisema
tiba ya Ukimwi imepatikana, lakini tiba kupata uthibitisho kwamba ni
sahihi, ni mchakato mrefu unaotakiwa kuhakikisha kama kweli dawa hiyo
inatibu na ni lazima WHO wathibitishe hilo,” alisema.
Alisema ni vizuri kama wataalamu hao
wakapata uhakika kutoka WHO badala ya kuwapa watu matumaini kuwa kuna
tiba na baadaye matumaini hayo yanapotea.
Daktari wa kitengo kinachoshughulika na
masuala ya Ukimwi cha WHO, Richard Banda alisema hana taarifa za tiba
hiyo. Tiba inavyofanya kazi Madaktari wa ONT walitumia damu ya mtu
mwenye vinasaba vya ‘CCR5Delta’ ambavyo seli zake haziathiriwi na virusi
hivyo vya Ukimwi.
Dk Duarte alisema kwanza huziua seli za
damu ya mgonjwa kwa kutumia mionzi halafu seli mpya (kutoka kwenye damu
ya mtu mwenye seli zisizoathiriwa na VVU hupandikizwa. Damu hiyo
ilipandikizwa kwa mgonjwa mwenye virusi hivyo na saratani ya damu.
Baada ya seli hizo kupandikizwa, Virusi
vya Ukimwi vilivyo kwenye damu ya mgonjwa hushindwa kujipenyeza katika
seli mpya zilizopandikizwa. “Siku 11 baada ya upandikizaji, mgonjwa wa
Barcelona alianza kupata nafuu na baada ya miezi mitatu, tulimpima na
kukuta hana VVU,” alisema.
HABARILEO
Rais John Magufuli amekutana na kufanya
mazungumzo na viongozi wanne wa taasisi nyeti tofauti kuhusu mambo
mbalimbali ya mustakabali wa Serikali yake ya awamu ya tano.
Mazungumzo hayo yaliyofanyika Ikulu
jijini Dar es Salaam, miongoni mwa viongozi aliokutana nao ni Mdhibiti
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Juma Assad
ambaye wamezungumzia kupunguza gharama za matumizi ya kuendesha serikali
na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Viongozi wengine ambao alikutana nao ni
Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), Biswalo Eutropius Mganga; Shehe
Mkuu, Mufti Abubakar Zuberi na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Bulembo.
Taarifa iliyotolewa na Ikulu jana,
ilisema pamoja na kutakiana heri ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli
alizungumzia mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa Serikali yake ya
awamu ya tano.
Akizungumzia yaliyojiri katika
mazungumzo hayo, CAG Assad alisema Rais Magufuli ametaka ofisi yake
ihakikishe Tanzania inaongeza ukusanyaji wa mapato kutoka asilimia 14 ya
Pato la Taifa (GDP) kwa mujibu wa hesabu zilizofanyika mwaka juzi.
“Hadi mwaka juzi Tanzania ilikuwa
inakusanya mapato kwa kiwango cha asilimia 14 ya Pato la Taifa
ikilinganishwa na Kenya ambayo ilikuwa ikikusanya asilimia 19 ya Pato la
Taifa, na hakuna sababu za msingi za kwa nini Tanzania iwe nyuma katika
ukusanyaji wa mapato hayo,” alisema Assad.
DPP Mganga alisema mazungumzo yao na
Rais Magufuli yalijikita katika suala la kupeana mikakati ya namna ofisi
yake inavyopaswa kufanya kazi kuendana na kauli mbiu ya serikali ya
awamu ya tano ya ‘Hapa Kazi Tu’.
Aidha Mganga alisema wamezungumzia
umuhimu wa kuhimiza Watanzania kufuata sheria, na kwamba ofisi yake
itatekeleza wajibu wake bila kumwonea mtu. Kiongozi mwingine aliyekutana
na Rais Magufuli ni Mufti Abubakar Zuber ambaye pamoja na kumpongeza
rais kwa juhudi kubwa alizoanza nazo katika uongozi wake, amesema
Waislamu wote nchini wanamuunga mkono na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu
aendelee na juhudi hizo.
“Na pia kwa niaba ya Waislamu tunataka
kumueleza kwamba kazi anayoifanya ni kazi ambayo tunairidhia na
tunamuomba aendelee kuifanya wala asiogope, na kauli yake ya Hapa Kazi
Tu iendelee, kwa sababu inaonesha kwamba sasa nchi yetu itakaa mahali
pazuri,” alisema Mufti.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Wazazi ya CCM, Bulembo, alimpongeza Rais kwa kasi nzuri aliyoanza nayo
katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015-2020 na kutaka
kasi hiyo iendelee. Alisema Jumuiya inaunga mkono kazi kubwa inayofanywa
na Rais Magufuli.
Bulembo alisema Rais amemhakikishia kuwa
ataendelea kufanya kazi hizo zaidi katika kutekeleza Ilani ya chama.
“Tunafurahi kwamba yapo mambo mengi ambayo Rais Magufuli ameanza
kuyatekeleza kwa haraka, mojawapo likiwa ni kufutwa kwa ada za shule, na
hivi sasa wanafunzi watakwenda shule pasipo kutozwa ada.” alisema
Bulembo.
HABARILEO
Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana,
Anthony Mavunde amevitoza faini ya zaidi ya Sh milioni 60 viwanda viwili
vya Lodhia Plastic Industries Limited na Sunflag (T) Ltd kwa kukiuka
taratibu za kazi na kudharau mamlaka ya usalama mahali pa kazi (Osha).
Mavunde alitoa adhabu hiyo jana jijini
hapa wakati alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye viwanda hivyo huku
akiongozana na wakuu wa idara ya kazi, idara ya uhamiaji na viongozi
kutoka Osha.
Awali alipokuwa katika kiwanda cha
Sunflag, alizungumza na baadhi ya wafanyakazi na kugundua kuwa baadhi
yao hawana mikataba ya ajira na wamefanya kazi zaidi ya mwaka mmoja
lakini pia hawana vifaa vya kutosha vya kuzuia pamba kuingia mwilini.
Pia aliagiza menejimenti ya kiwanda
hicho, kuhakikisha inalipa mishahara ya wafanyakazi kwa kima cha
Serikali na si kuwalipa Sh 4,424 kwa siku. Aidha akiwa kiwandani hapo
aligundua kuwa kuna wafanyakazi raia wa kigeni 41 wanaofanya kazi katika
idara mbalimbali zinazopaswa kusimamiwa na raia wa Tanzania.
Akiwa katika kiwanda cha Lodhia, Mavunde
alifuta kibali cha mmoja wa wageni kutoka nje ya nchi kutokana na
kukiuka kibali cha kufanyakazi na kumwagiza Mkurugenzi wa Kiwanda hicho
Raju Sighn kupeleka vibali 38 vya raia wa kigeni ili vikaguliwe.
Kutokana na kasoro hizo Mavunde alitoza
faini ya jumla ya Sh milioni 22.9 kwa kiwanda cha Sunflag na kiwanda cha
Lodhia Plastic kilitozwa Sh milioni 10 kutokana na kukiuka masharti ya
uendeshaji viwanda na kutoa siku 14 faini hiyo iwe imelipwa.
“Ndani ya siku saba muwe mmepeleka
taarifa Osha na hivi vibali vya wageni kutoka nje ya nchi kwa ofisi za
kazi jijini Arusha. Maana mnasema mna vibali lakini nilivyoviona
havijaniridhisha, pelekeni ili waone na ikithibitika mmekidhi viwango
mtapunguziwa adhabu, ila heshimuni sheria za nchi,” alisisitiza.
HABARILEO
Serikali imenunua mashine mpya ya
CT-Scan kwa ajili ya kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa mbalimbali
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH). Mashine hiyo yenye thamani
ya Dola za Marekani milioni 1.7 (takribani Sh bilioni 3.6) imeelezwa
kwamba ni yenye uwezo wa hali ya juu.
Ununuzi wa mashine hiyo, umefanyika
baada ya agizo la Rais John Magufuli alilolitoa hivi karibuni akiutaka
uongozi wa MNH kuboresha huduma zake kwa kuhakikisha vifaa tiba na dawa
vinapatikana ili Watanzania wapate huduma bora ya matibabu.
Ununuzi wa mashine hiyo ulielezwa jana
na Mkuu wa Idara ya Mionzi, Dk Flora Lwakatare, wakati Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi
Kingwangalla alipofanya ziara katika hospitali hiyo kubwa zaidi nchini.
Dk Kigwangallah pia alitembelea Idara ya
Magonjwa ya Dharura, Idara ya Mionzi na sehemu mpya ya wagonjwa waliopo
chini ya uangalizi maalumu (ICU). Dk Lwakatare alisema kwamba CT-Scan
hiyo mpya imetengenezwa na kampuni ya Siemens na kwamba imefungwa siku
mbili zilizopita.
Alifafanua kwamba tayari wameshaanza
kuifanyia majaribio kwa wagonjwa 26 tangu ilipofungwa na kusaidia sana
uchunguzi. Dk Lwakatare alisema mashine ya uwezo huo iko moja tu nchini
na kwamba katika nchi za Afrika Mashariki, hospitali nyingine yenye
mashine kama hiyo ni Aga Khan ya nchini Kenya.
“Mashine hii inatoa huduma za hali ya
juu kwa magonjwa ya moyo, ubongo, tumbo na kifua na ina uwezo wa kupima
kifua na tumbo kwa sekunde sita tu,” alisema. Naibu Waziri Kigwangalla
alifafanua kwa waandishi wa habari kwamba mashine hiyo imenunuliwa kwa
fedha za serikali na sio mkopo.
“Tunatarajia kununua mashine pia kama
hii katika hospitali za Dodoma na Mwanza,” alisema Kigwangalla. Naye
Kaimu Mkurugenzi wa MNH, Profesa Laurence Maseru alisema mashine hiyo
ina sahani 128, mara mbili zaidi ikilinganishwa na iliyokuwepo.
Kuhusu mashine ya MRI, Profesa Maseru
alisema kwamba tangu ilipofanyiwa matengenezo makubwa Novemba 26 mwaka
jana, imeshahudumia wagonjwa 560 na inaendelea kufanya kazi.
Dk Kigwangalla pia alitembelea Idara ya
huduma za dharura na kuangalia jinsi huduma zinavyotolewa, ambapo
alielezwa na Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura, Dk Juma Mfinanga
kwamba wanahudumia wastani wa wagonjwa 300 hadi 400 kwa siku.
Naibu Waziri huyo, mbali na kupongeza
maboresho yaliyofanyika na huduma nzuri inayotolewa kwa sasa, alitoa
maagizo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuboresha huduma zaidi kadri
inavyowezekana.
Aliutaka uongozi wa hospitali hiyo
kuhakikisha unawalipa wafanyakazi malipo ya ziada kwa wakati, kutumia
mfumo wa kompyuta sehemu zote, kupunguza msongamano wa wagonjwa na kuwa
wabunifu.
HABARILEO
Watu wanane akiwemo Msaidizi wa Mkuu wa
Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP), Gerald Ryoba pamoja na familia
yake, wamekufa maji baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na
maji katika mkondo mpana wa mto unaotenganisha Kibaigwa na Pandambili,
mkoani Dodoma.
Watu sita ni wa familia ya Ryoba
waliokuwa ndani ya gari lililosombwa na maji likijaribu kupita. Pia
miili ya watu wengine wawili ambao pia walikufa kutokana na kusombwa na
maji, ilipatikana baada ya maji kuisha.
Pamoja na msaidizi huyo wa IGP, wengine
waliokuwa kwenye gari hilo lililosombwa na maji, ni mkewe, Fidea Kiondo
ambaye ni Mwalimu katika Manispaa ya Temeke, jijini Dar es Salaam pamoja
na watoto wao, Gabriel (4) na Godwin; msaidizi wa kazi za ndani, Sarah
na dereva, Koplo Ramadhani.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma,
David Misime katika taarifa yake alisema kwamba Ryoba na familia yake
walikuwa wakitoka mkoani Geita kwenda Dar es Salaam. Mtendaji wa Kata ya
Kibaigwa, Gabriel Mganga alimwambia mwandishi wa habari hizi kwamba
maiti wawili ambao ni tofauti na waliokutwa kwenye gari, mmoja
hakutambulika lakini mwingine amebainika ni Ofisa Kilimo na Mifugo Kata
ya Lenjulu, wilayani Kongwa aliyetambulika kwa jina la Eudiji.
Kuopolewa kwa familia hiyo ndani ya gari
kuliwezeshwa usiku wa manane baada ya maji kupungua. Mganga alisema
kwamba walilazimika kukata kwa gesi gari lililokuwa limebeba familia ya
msaidizi wa IGP baada ya kusombwa na maji kwa ajili ya kutoa watu wawili
waliokuwa ndani.
Wengine waliokotwa nje na kutambuliwa
kutokana na vitambulisho vilivyokutwa katika gari. Alitaja gari hilo ni
aina ya RAV 4 yenye namba za usajili T 516 DEP. Kwa mujibu wa mtendaji
huyo aliyekuwa kwenye eneo la tukio, dereva huyo wa polisi alionywa
asiingie katika mkondo huo kutokana na wingi wa maji lakini
hakuwasikiliza.
Alisema baada ya kuingia kwenye mkondo,
maji yaliitoa gari barabarani na kuitupa katika korongo la mto kabla ya
kwenda kusimama katika eneo lenye bwawa. Alisema mkondo huo ambao wengi
hupaita Pasua, ni moja ya sehemu korofi na madereva wengi hushitukizwa
na maji kwa kuwa mkondo huo unatoka mbali.
Diwani wa Kata ya Kibaigwa, Kapinye
alisema eneo hilo linajulikana kuwa korofi na ni pana na maji yake huja
kwa kishindo. Ilielezwa kwamba maji hayo yaliyoanza kuingia barabarani
juzi saa 11.30, yalisababisha magari zaidi ya 400 kukwama kila upande
katika barabara hiyo kuu ya Dodoma-Morogoro.
Mafuriko hayo ni matokeo ya mvua
zilizonyesha katika Kata ya Njoge Kiteto, Hembahemba na bonde la
Ndurugumi wilayani Kiteto. Wakati huo huo, Kamanda Misime katika taarifa
yake pia alisema kwamba madaktari katika hospitali ya rufaa Dodoma
wanaandaa miili ya marehemu kwa ajili ya kusafirishwa ambapo familia ya
Ryoba itapelekwa Geita, mfanyakazi wa ndani atapelekwa Mbinga na dereva
mwili wake utapelekwa Lindi.
“Huyu koplo ambaye alikuwa ni dereva
yeye ni mwenyeji wa Lindi na Mkaguzi (Ryoba) ni mtu wa Geita hivyo
tunatarajia kusafirisha mwili wake pamoja na wa mkewe na watoto wake
wawili, na msichana wa kazi atapelekwa Mbinga,”alisema Misime. Kaimu
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Ibenze Ernest
amethibitisha kupokea miili sita ya marehemu kutoka eneo la tukio.
HABARILEO
Licha ya Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kutoa huduma bure za afya kwa wajawazito, ni asilimia 12.4 tu
ya wanawake wanajifungulia katika hospitali za serikali.
Ofisa Mshauri Mwandamizi wa huduma za
uzazi salama, Hanuni Waziri Songoro alisema hayo wakati alipozungumza na
wafanyakazi wanaotoa huduma za uzazi kwa akinamama huko Mbweni mjini.
Songoro alisema kwa upande wa Pemba
asilimia ya wanawake 66 wanajifungulia majumbani kwa sababu mbali mbali
ikiwemo masafa ya kupata huduma hizo zaidi vijijini. Aidha kwa upande wa
Unguja asilimia 44 ya wanawake wanajifungulia majumbani kwa kupata
huduma kutoka kwa wakunga wa kienyeji.
“Utafiti uliofanywa wa wajawazito kuhusu
matumizi ya huduma za uzazi salama imebainika wengi bado hawajapata
mwamko wa kujifungulia katika hospitali zenye huduma sahihi zaidi,”
alisema.
Alisema kwa upande wa kisiwa cha Pemba,
moja ya matatizo makubwa linalowafanya wajawazito kujifungulia majumbani
ni umbali wa vituo vya afya. Aidha alisema bado baadhi ya wananchi
wamekuwa wakiendekeza itikadi na imani za jadi ambazo huwafanya kupenda
kujifungua majumbani kuliko hospitalini.
“Zipo sababu mbali mbali zinazowafanya
akinamama kujifungulia majumbani ikiwemo umbali wa kupata huduma za afya
zaidi vijijini. Lakini lipo tatizo la wanawake kuamini zaidi imani ya
itikadi,” alisema.
Mkazi wa Kilimahewa, Asha Saidi, alisema
baadhi ya wanawake wanagoma kujifungua katika hospitali kwa sababu ya
huduma zisizoridhisha kutoka kwa wauguzi.
Aliipongeza Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kwa kufuta ada mbali mbali walizokuwa wakitozwa akinamama
waliokuwa wakijifungulia katika hospitali za Serikali, lakini zaidi
alitaka kuimarishwa kwa huduma hizo kutoka kwa wauguzi.
“Mimi nimejifungua watoto wanne wote
katika hospitali ya Serikali lakini tatizo moja kubwa ni kwamba huduma
kutoka kwa wauguzi zinatakiwa ziimarishwe na kuwa bora zaidi kwani watu
wanaona bora kuwafuata wakunga wa kienyeji,” alisema.
Muuguzi katika hospitali ya Mnazi Mmoja
aliyejitambulisha kwa jina la Asia Juma, alisema wamejipanga kuhakikisha
kwamba wanatoa huduma bora zinazokwenda sambamba na maadili na viapo
vya kazi.
“Huduma zinazotolewa katika hospitali
zinazowahudumia wajawazito zimeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa lengo la
kuondosha malalamiko yote yaliyokuwa yakitolewa awali,” alisema.
NIPASHE
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameutaka
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha wakulima wa
mahindi wanapatiwa magunia ya kuhifadhia mazao yao.
Agizo hilo alilitoa jana katika ziara
yake ya siku tatu ya kikazi mkoani Ruvuma na kwamba anatekeleza agizo
la Rais John Magufuli kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa njaa.
Majaliwa alisema wafanyabiashara
wamekuwa wakipatiwa magunia na NFRA kwa ajili ya kununulia mahindi
lakini wakulima wanapoomba kupatiwa imekuwa ni tatizo kwao kuyapata kwa
urahisi.
Alionyesha kusikitishwa na vitendo hivyo
vinavyofanywa na wafanyabiashara wajanja, ambao wamekuwa wakipita
vijijini kuwarubuni wakulima na kununua mahindi kwa bei ndogo ambayo
hailingani na uzalishaji wa zao hilo.
Alisema kumekuwa na mianya ya rushwa
inayofanywa na wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na baadhi ya maofisa
wa NFRA kwa lengo la kujinufaisha watu wachache huku mkulima wa kawaida
akiendelea kuteseka na mazao yake shambani.
“Magunia yanayonunuliwa na serikali kwa
ajili ya kuhifadhia zao hili, ninazo taarifa za kutosha kwamba
hayamfikii mkulima kule kijijini, badala yake yanaishia kwa watu
wachache”, alisema Waziri Mkuu.
Alisema serikali ina wajibu wa kuhifadhi
chakula katika mazingira yanayokubalika ili kisiharibiwe na wadudu
waharibifu, hivyo ameitaka NFRA Kanda ya Songea kuhakikisha mahindi
yaliyohifadhiwa chini ya ardhi yanatafutiwa sehemu nyingine ili
yasiharibike.
Alifafanua kuwa uhifadhi wa aina hiyo,
usalama wake ni mdogo na kwamba mlundikano huo wa magunia yaliyosheheni
mahindi katika hifadhi unasababishwa na wakala kuwa na upungufu mkubwa
wa maghala.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alihoji kuwepo kwa msongamano wa malori kandokando ya barabara ya Songea – Mbinga.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha
malalamiko kutoka kwa wasafirishaji kuwa magari yanayoingia kupakia
mahindi, NFRA huwapatia watu wanaojulikana kwanza, ndipo huruhusu
wengine kitendo kinachoonyesha kuwepo upendeleo.
Awali, Mbunge wa Songea Mjini, Leonidas
Gama, alisema tatizo la soko la mahindi katika mkoa huo ni kubwa, hivyo
ameiomba serikali ya awamu ya tano, iangalie namna ya kutafuta masoko
ili wakulima wadogo wapate fursa ya kuuza mazao yao.
NIPASHE
Wafanyakazi 350 wa kiwanda cha Sukari
Mahonda wapo katika hatari ya kupoteza ajira baada ya shamba la miwa la
kiwanda hicho kuchomwa moto kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha siku
tano, mkoa wa Kaskazini Unguja.
Hayo yalisemwa na meneja wa kiwanda
hicho, Tushar Mehta, wakati Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi
Seif Ali Iddi, alipofanya ziara ya kukagua mashamba yaliyochomwa moto ya
wawekezaji hao.
Alisema kitendo cha kuendelea kuhujumiwa
mashamba yao ya miwa kinaweza kusababisha uongozi wa kiwanda hicho
kuzuia ajira mpya 450 baada ya kukamilika kwa matengenezo makubwa na
kuanza tena uzalishaji wa sukari.
Alisema watu wasiofahamika waliingia
katika shamba hilo na kuwasha moto kwa mara ya pili baada ya tukio kama
hilo Disemba 30, mwaka jana.
“Moto uliwashwa katikati ya shamba la
miwa juzi, kabla ya waliofanya kitendo hicho kuwasha moto huo waliweka
kizuizi kwa makusudi ili vikosi vya uokozi vishindwe kuuzima haraka,”
alisema.
Mehta alisema hadi sasa eka 200
zimeteketezwa kwa moto kwenye matukio yote mawili katika kipindi cha
siku tano na kusababisha hasara ya dola za Marekani 1,176,234.28 sawa
na Sh. bilioni 2.3.
Akizungumza baada ya kupatiwa taarifa
hiyo, Balozi Seif alisema vitendo hivyo vya hujuma haviitakii mema
Zanzibar katika harakati zake za kukuza uchumi na kufanikisha mpango wa
kukuza uchumi na kupunguza umasikini kwa wananchi wake.
Alisema watu wanaofanya vitendo hivyo
wanafanya dhambi kubwa na pia wanawavunja moyo wawekezaji walioamua
kuwekeza miradi yao ya kiuchumi Zanzibar kwa lengo la kuisaidia
serikali pamoja na wananachi kupata maendeleo.
Alisema fikra za baadhi ya watu kwamba
hujuma hizo zitatoa fursa kwao kutumia maeneo ya mashamba hayo ya miwa
kuendeleza kilimo na mifugo inafaa kuachwa mara moja kwa vile
yataendelea kuwa katika mipango ya serikali ya kuhudumia sekta ya
viwanda.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa Tangakumekuchablog
No comments:
Post a Comment