Wednesday, November 8, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 23

HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 23
ILIPOISHIA
“Enhe ameambiwa anaitwa nani?”
“Latifa kama sikosei”
“Sasa aliuawa na nani?”
“Ndiyo haijajulikana”
“Basi ndio hivyo”
“Inaelekea hapo shuleni kwenu kuna matatizo”
“Matatizo kama yapi?’
“Kama wanafunzi wameanza kuanguka chooni na kufa, huoni kama ni matatizo?’
Sofia akanyamaza kimya.
“Baba yako ameshauri tukusimamishe masomo kwa muda mpaka hali itakapokuwa nzuri”
“Una maana hali ya pale shule?”
“Ndiyo”
“Baba ana wasiwasi kuwa naweza kufa?”
“Hatujui lakini inawezekana?”
“Kwani mnahisi ni kitu gani?”
SASA ENDELEA
“Ni kama miujiza tu ambayo haielweki kwa sababu tumeambiwa kwamba huyo mwanafunzi alifyonzwa damu”
“Sawa” Sofia akasema kwa sauti iliyonywea kisha akauliza.
“Kwa hiyo kuanzia kesho sitakwenda shule?”
“Hutakwenda?”
“Inabidi kuwe na taarifa”
“Taarifa itapelekwa”
“Sawa”
Siku iliyofuata Sofia akapelekwa kijijini kwa mama yake. Kwa mara nyingine tena aliendelea kuaguliwa na waganga mbali mbali na kuwekewa ulinzi mkali saa ishirini na nne. Hata baada ya waganga kumuhakikishia mama yake Sofia kuwa matatio ya Sofia yamekwisha, baba yake alitaka aendeleaa kukaa hapo kijijini ili kumtazamia hali yake.
                                 ****************
Maria rafiki yake Sofia alikuwa akiishi na kaka yake ambaye ni daktari eneo la sinza jijini Dar. Dk Deo alikuwa akimiliki hospitali yake mwenyewe eneo la Mikocheni ambayo ilikuwa maalum kwa kuunga mifupa iliyovunjika.
Deo alikuwa daktari bingwa wa mifupa ambaye alikuwa amejipatia sifa ndani na nje ya nchi kutokana na uwezo wake wa kuunga mifupa iliyoshindikana kuungika katika hospitali nyingine.
Awali alikuwa daktari wa jeshi, akaamua kuacha kazi na kufungua hospitali yake mwenyewe ambayo ilikuwa ikipokea wagonjwa wa mifupa kutoka mikoani na nje ya nchi.
Ilikuwa na idadi kubwa ya wagonjwa waliotoka Kenya, Uganda,Malawi. Congo DRC, Rwanda na Burundi.
Ilikuwa hospitali kubwa iliyokuwa na uwezo wa kulaza wagonjwa zaidi ya mia tatu. Mbali ya yeye Dk Deo, alikuwa ameajiri madakatari wengine kwa ajili ya kumsaidia kazi pamoja na kutibu magonjwa mengine.
Mke wa Dk Deo alikuwa ameshafariki dunia kwa ajali ya gari miaka kadhaa iliyopita. Hakuwahi kuoa tena na alikuwa akiishi na mdogo wake Maria pamoja na watumishi wawili wa nyumbani kwake.
Kulikuwa na kipindi ambapo Maria aliugua malaria akalazwa katika hospitali ya kaka yake. Wanafunzi wenzake mbali mbali walikuwa wanakwenda kumjulia hali.
Sofia aliporudishwa jijini baada ya kuaguliwa na waganga mbalimbali huko kijijini kwao, alipata habari kuwa Maria alikuwa amelazwa katika hospitali ya kaka yake iliyoko mikocheni.
Alimwambia mama yake na wakapanga kumtembelea pamoja na mheshimiwa Waziri Mkuu.
Ilikuwa siku ya jumapili, mara tu waliporudi nyumbani kutoka kanisani wakapanda gari moja kuelekea Mikocheni. Kwa heshima yake waziri mkuu na kwa cheo chake, alitanguliwa na gari la polisi kwa ajili ya kumuwekea ulinzi.
Gari la Waziri Mkuu lilipofika hospitali ya Dk Deo, Waziri Mkuu, mke wake na Sofia walishuka na kuingia katika lango la hospitali. Walikwenda moja kwa moja katika chumba alichokuwa amelazwa Maria. Muuguzi aliyewapeleka aliwafungulia mlango wakaingia ndani.
Maria alikuwa amelala kitandani akionekana kuwa taabani.
“Maria unajionaje?” Waziri Mkuu akamuuliza Maria.
Maria alikuwa akitazama lakini hakuweza kujibu.
“Hali yake bado si nzuri” muuguzi akamwambia Waziri Mkuu kisha akaongeza.
“Subiri nikamuite dokta ambaye ni kaka yake aje akupe maelezo”
“Nenda katuitie tunakusubiri” Waziri Mkuu alimwambia muuguzi huyo.
Wakati muuguzi anatoka, Sofia akamfuata. Muuguzi huyo alikwenda katika ofisi ya Dk Deo akafungua mlango na kuingia.
Dk Deo hakuwemo.
Wakati muuguzi huyo anageuka ili atoke, Sofia naye akaingia mle ofisini. Macho yake yalikuwa yameshabadilika rangi na kuwa mekundu. Alimshika muuguzi huyo ambaye baada ya kushikwa na sofia alihisi mwili wake ukilegea.
Sofia alifungua mdomo wake na kukita meno yake kwenye shingo ya muuguzi huyo ambaye alifungua mdomo wake ili apige kelele lakini sauti haikutoka.
Sofia baada ya kumpiga meno alianza kumfyonza damu.
Katika chumba alichokuwa amelazwa Maria, dakika ziliendelea kupita. Waziri Mkuu alitazama saa yake na kuona zilikuwa zimeshapita dakika kumi na tano. Ingekuwa ni muuguzi peke yake wanayemsubiri, Waziri Mkuu asingepata wasiwasi lakini Sofia naye alikwenda huko huko.
Amekwenda wapi muda wote huo?
Na amefuata nini?
Waziri Mkuu akatoka. Mke wake naye akamfuata.
Wakati wanatoka, walimuona Dk Deo akitoka katika chumba kilichokuwa jirani na ofisi yake. Wakati huo huo wakamuona Sofia akitoka katika ofisi ya Dk Deo. Walikutana kando ya mlango. Sofia hakuonekana kumjali Dk Deo japokua walikuwa wakifahamiana. Alimpita kama vile hakumuona akaelekea kwenye mlango wa kutokea nje ya jengo hilo.
Dk Deo alisita, akawa anamtazama Sofia kwa nyuma huku uso wake ukionesha mshangao.
Alikuwa kama anajiuliza huyu ni Sofia binti wa Waziri Mkuu au siye. Na amefuata nini ofisini kwangu?
Dk Deo akaingia ofisini kwake. Sofia alikuwa ameuacha wazi mlango wa ofisi yake.
Dk Deo alipoingia ofisini humo alishituka alipomuona muuguzi wake yupo chini akiwa na jeraha linalovuja damu kwenye shingo yake.
Dk Deo alichutama na kumtazama muuguzi wake huyo.
“Mage Mage!” alimuita huku akimshika kichwa.
Mage alikuwa kimya. Macho yake yalikuwa wazi lakini hayakuwa yakiona chochote.
Waziri Mkuu na mke wake walikuwa wameshafika kwenye usawa wa mlango wa ofisi ya Dk Deo. Walimuona Dk Deo akichunguza lile jaraha kwenye shingo ya Mage.
Mara moja walimuona daktari huyo akiinuka kwa kasi. Waziri Mkuu na mke wake walijua kuwa alikuwa anamfuta Sofia aliyekuwa ametoka humo ofisini.
“Dokta unafanya nini?” waziri Mkuu akamuuliza kwa mshituko.
Hapo Ndipo Dk Deo alipoona kuwa kulikuwa na mheshimiwa mbele ya mlango.
“Kuna tatizo limetokea!” akasema kwa taharuki.
“Tatizo gani?”
“Huyu muuguzi wangu sijui amepatwa na tatizo gani. Ameanguka chini na ameshakufa lakini kwenye shingo yake ana jeraha la kung’atwa na meno na linatoa damu”
“Amefanya nini?” Waziri Mkuu akamuuliza kimtego.
“Sijajua ila kuna binti yako, rafiki wa mdogo angu nimemuona ametoka katika ofisi yangu katika hali ambayo si ya kawaida, amenitia wasiwasi sana”
“Unataka useme nini Dokta wakati tumekuona ulichofanya, wewe umemdhuru muuguzi wako halafu unataka kusingizia watu waliotembelea wagonjwa”
“Hapana, Sofia alitoka ofisini mwangu muda huu huu mwenyewe nikiwa sipo”
“Acha uongo! Tumeona kila kitu ulichofanya. Ulikuwa unamfyonza damu muuguzi wako!”
“Mhehimiwa siijafanya hivyo, nimemkuta muuguzi huyu tayari yuko katika hali hii na sijajua amepatwa na nini”
“Tafadhali simama hapo hapo!”
Waziri Mkuu alitoa simu yake ya mkononi akawapigia polisi waliokuwa katika gari la polisi lililokuwa linaongoza gari lake.
“Hebu njooni humu ndani mara moja! aliwambia.
Polisi hao walipofika aliwaaamuru wamkamate Dk Deo.
“Amemdhuru muuguzi wake mbele ya macho yetu, huyu ni dokta hatari kweli kweli”
Polisi hao walimkamata Dk Deo.
“Tokeni naye nje” akawambia kisha akapiga simu tena makao ya polisi.
Alimpigia Mkurugenzi wa Upelelezi akamtaka afike katika hospitali ile iliyokuwa Mikocheni.
“Kuna tukio limetokea”
“Tukio gani mheshimiwa?” Sauti ya Mkurugenzi wa upelelezi ikasikika kwenye simu.

ITAENDELEA kesho Usipitwe na uhondo huu hapoahapa kumekucha.com

No comments:

Post a Comment