RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
13
ILIPOISHIA
Kichwa changu kilikuwa
kimeshavurugika. Nilijiambia kama mke
wangu atakwenda Korogwe, anaweza kupata madhara kwa vile sikuwa nikijua lile tatizo
langu lingekwishaje usiku ule.
Kwa vile sikutaka yule mzee
ajue kuwa nilikuwa nimefadhaika, tukaanza kuzunguma.
Tulizungumza mengi kuhusu
kile kisima cha Giningi. Aliniambia yeye alizaliwa wakati wa utawala wa sultani
na hicho kisima allikikuta hivyo hivyo.
“Haijulikani ni nani alikichimba
na kilichimbwa wakati gani” aliniambia.
“Huenda kilichimbwa miaka
mingi iliyopita. Baba yangu aliniambia alikikuta hivyo hivyo” akaongeza.
“Unadhani hapo kilipochimbwa
kilichimbwa kwa madhumiuni gani?” nikamuuliza ili kupata undani wa kisima hicho.
“Nafikiri kilichimbwa na
wenyeji wa wakati huo ili kupata maji ya kutumia”
“Mpaka hii leo watu wanateka
maji?”
“Hivi sasa hakitumiki tena”
SASA ENDELEA
“Sasa imekuwaje mahali hapa
pakawa panatumika katika mambo haya?”
Hapo nilikusudia mambo yale
ya uchawi na majini.
“Tangu sisi tunainukia
tulikuta watu wakifanya matambiko na mambo mengine ya kijadi”
“Unafikri ni kwanini?”
“Hiki kisima ni cha miaka
mingi. Kitakuwa kinakaliwa na majini na kuna miujiza mengi iliyowahi kutokea
mahali hapa.
“Kama ipi?”
“Kulikuwa na watu waliokuwa
wakionekana nyakati za usiku wakikusanyika mahali hapa. Watu hao walikuwa ni
majini. Wakati mwingine huonekana moto
lakini haijulikani ni nani aliyeuwasha. Hizi zote ni ishara kuwa hili eneo lina
wenyewe”
“Sasa tukirudi kwenye hii
shughuli yangu, unadhani itafanikiwa?”
“Tutamsikiliza mwenyewe
maalim atakapotuita usiku”
“Kwani inaweza
ikashindikana?”
“Kwa vile amekwambia
atakushughulikia usiku, nafikiri itawezekana. Kushindikana si aghalabu sana”
Mzee akaniambia na kunipa chembe ya
matumaini.
“Mzee sitakuficha, hofu yangu
kubwa ni kwa mke wangu. Hivi sasa yuko Dodoma lakini amesema kesho atanifuata
Korogwe na mimi sikumwambia kuwa ninakuja huku”
“Kwanini hukumwambia?”
“Sikumwambia kwa sababu
niliogopa kumtia waiwasi. Yule jini aliniambia mama yangu atakufa hivi karibuni
na mke wangu ndiye atakayechukua nafasi yake. Sasa sikutaka aje pale Korogwe
mpaka hili suala nilipatie ufumbuzi”
Nilipomwambia hivyo yule mzee
hakunijibu kitu, alinitazama tu kama vile aliniona nilikuwa mgeni sana katika
mambo yale ya mtu kutolewa kafara wakati yeye aliona yalikuwa ya kawaida.
Tukaendelea kuzungumza lakini
ghafla niliona mwenzangu akianza
kusinzia.
Alipogutuka akaniambia twende
tukalale. Tukaingia ndani ya kile kibanda na kulala. Mimi nililala na nguo
zangu hivyo hivyo.
Kusema kweli sikulala
usingizi. Muda wote nilikuwa nikiwaza tu na niliyekuwa nikimuwazia sana alikuwa
mke wangu. Hofu yangu ilikuwa kwenye ile safari yake ya kwenda Korogwe.
Niliwaza kwamba anaweza
kufika Korogwe kabla ya mimi na hivyo akahatarisha maisha yake.
“Yule jini anaweza kumchukua”
nilikuwa nikijiambia.
Wakati nikiendelea kuwaza,
muda nao ulikuwa ukienda. Sikutambua kama ulikuwa usiku mwingi niliposikia
hatua za mtu zikisogea pale kwenye kibanda tulichokuwemo. Moyo wangu ukashituka,
nikatega masikio yangu kusikiliza.
Ghafla nilisikia mlango wa
kibanda hicho ukibishwa.
“Bwana Hanzuruni…Bwana Hanzuruni….”
Nikaisikia sauti ya yule maalim ikiita.
Nikainuka na kukaa.
“Bwana Hanzuruni!” Sauti
ikaendelea kuita.
Nilitaka nimuamshe yule mzee
aliyekuwa amelala lakini akawahi kuamka mwenyewe.
“Labeka maalim” akasema huku
akiinuka.
Alinishika mguu kisha
akanitazama.
“Alah! Kumbe umeshaamka!”
akaniambia.
“Mimi nimeshaamka, nilikuwa
nataka kukuamsha wewe”
“Maalim huyo ameshakuja”
“Nilifikiri sisi ndio
tutakwenda kwake”
“Amekuja mwenyewe kutuamsha
labda alijua tumepitiwa na usingizi”
Nikaitazama saa yangu na kuona ilikuwa saa nane ikikaribia kuwa na
nusu.
Tukanyanyuka na kutoka kwenye
kile kibanda.
“Wakati umewadia twendeni”
Maalim huyo akatuambia. Alikuwa ameshika tochi mkononi.
Tulikwenda kando ya kile
kisima. Maalim akaniambia.
“Unaouna ule mti” Alinionesha
mti wa mkuyu uliokuwa mbali kidogo na sisi.
“Nauona” nikamjibu.
“Sasa nenda chini ya mti ule
utaje jina la baba yako na jina lako halafu umuite Maimuna binti Ibilisi.
Umuite mara tatu. Kuna kivuli kitakuja pale utakiambia shida yako. Hicho kivuli
ni cha jini aliyemiliki kisima hiki. Umenielewa?” Maalim aliniambia haraka
haraka.
“Yaani niende peke yangu?”
nikamuuliza kwa hofu kwani mahali penyewe palikuwa mbali kidogo na palikuwa
panatisha usiku ule. Isitoshe pia nilitishika kukutana na hicho kivuli
nilichoambiwa ni cha jini aliyemiliki kisima kile.
“Unataka uende na nani?
Mwenye shida ni wewe au sisi?” Maalim akaniuliza.
“Ni mimi”
“Basi wewe ndiye unayetakiwa
kwenda hata baba yako alikwenda pale pale muda kama huu, ndio akapewa huyo jini,
sasa na wewe unatakiwa uende pale pale”
“lakini sitapata tatizo
lolote?”
“Tatizo kama lipi?”
Hapo nikashindwa kujibu.
Badala yake nikatoa hoja nyingine.
“Mzee hawezi kunisindikiza
mpaka pale karibu karibu?” nikamwambia yule mzee.
Maalim akaja juu.
“Unajua tumeacha usingizi
wetu kwa ajili yako wewe!”
“Sawa. Sasa nilikuwa na swali
moja”
“Swali gani?”
“Nikishasema shida yangu ndio
itakuwaje”
“Atakupa jibu, utakuja
kutuambia”
“Kwa hiyo nieleze kwamba mimi
sitaki zile pesa nilizorithi kwa baba yangu na pia simtaki yule jini…”
“Wewe zungumza utakavyoweza.
Eleza kama ulivyotueleza sisi. Useme kwamba hizo pesa zirejee hapa pamoja na
huyo jini aliyekuwa mke wa baba yako”
Nikashusha pumzi ndefu kabla
ya kuyapeleka tena macho yangu kweye ule mti. Bado nilikuwa nikiushauri moyo
wangu niende mahali pale nikazungumze na kivuli ambacho sikujua kilikuwa
kikoje.
Nilihisi huo ulikuwa ni
mtihani mwingine uliokuwa umenikabili. Lakini nilipowaza kuwa matatizo
yaliyokuwa yakinikabili mimi mwenyewe, mke wangu, mwanangu na mama yangu
waliokuwa kwenye pango, nilijikuta nikipiga hatua za kiaskari kuelekea kwenye
mti huo.
“Kitakachotokea na kitokee,
potelea mbali!” nikajiambia kimoyomoyo.
Kwa vile bahari haikuwa mbali
sana na mahali hapo, upepo wa baridi ulikuwa ukinipulizia lakini niliendelea
kutembea kwa hatua za ukakamavu kuelekea kwenye mti huo.
Kama sijakosea ulikuwa kama
mwendo wa hatua mia moja hivi hadi nilipokifikia kivuli cha mti huo. Chini ya
mti palikuwa na kichaka lakini hakikuwa kikubwa. Juu ya mti huo kunguru walikuwa
wakirukaruka na kupiga kelele.
Kwa mbali nilisikia sauti ya
bundi anayelia. Nilipofika hapo ilibidi nitazame nyuma ili niwaone wale watu.
Walikuwa wamesimama mbali kidogo wakinitazama.
Sikutaka kuingia kwenye kile
kichaka usiku ule kwa sababu sikujua kama palikuwa salama. Nikasimama mwanzo wa
kichaka hicho na kuusemea ule mti.
Kwa vile yule Maalim
aliniambia niseme shida yangu, nikazungumza kwa sauti ya kusikika kile
kilichokuwa moyoni mwangu. Nilieleza kwamba baba yangu ambaye kwa wakati ule ni
marehemu alifika mahali hapo na kutaka apate pesa za majini.
Nikaendelea kueleza kwamba
marehemu alipatiwa mke wa kijini na alipata utajiri kama alivyotaka lakini inasemekana
alinitaja mimi kama mrithi wake bila kunishauri mwenyewe.
“Sasa baba mwenyewe amekufa,
yule jini pamoja na zile pesa za majini vimekuja kwangu. Kilichonileta hapa ni
kuwa mimi sizitaki zile pesa kwa sababu siye niliyeziomba na pia simtaki yule mke
wa kijini, nataka arudi kwao” nikasema.
Lakini sikuishia hapo tu,
niliendelea kuzungumza kuwa baba alimtoa kafara mke wake pamoja na mjukuu wake
ambaye ni mwanangu mimi ili kutimiza masharti ya kupata utajiri.
“Sasa nataka mama yangu
pamoja na mwanangu wawe wazima kama zamani. Na pia yule jini ameniambia kuwa
mke wangu naye atatolewa kafara. Mimi sitaki atolewe kafara kwa sababu sitaki
utajiri wa pesa zile” nikasema.
Nikamalizia kwa kueleza.
“Kwa hiyo nataka yule jini
arudi kwao na zile pesa zirudi huku huku na mama yangu na mwanangu wawe wazima”
Nilipomaliza nilisubiri kwa
dakika moja, sikuona kitu chochote. Nikageka na kurudi kwa wale watu.
No comments:
Post a Comment