Thursday, November 9, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONIO, SEHEMU YA 24

 
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 24
 
ILIPOISHIA
 
Waziri Mkuu akamueleza kwamba kuna muuguzi ameuawa  na daktari wake.
“Sawa mheshimiwa, tunakuja”
Waziri Mkuu alipomaliza kuzungumza na mkurugenzi wa upelelezi alitoka nje ya hospitali hiyo akiwa amefuatana na mke wake.
Walikuta Dk Deo amepakiwa katika gari la polisi huku mmoja wa polisi hao akiwasiliana kwa radio Call na polisi wenzake.
Wasiwasi wa Waziri Mkuu na mke wake ulikuwa kwa Sofia, hawakujua lipotoka katika ofisi ya Dk Deo alikwenda wapi.
Lakini walipokwenda kwenye gari lao walimkuta amejipakia katika siti ya nyuma na alikuwa amelala. Kwenye mdomo wake wa chini alikuwa na chembechembe za damu.
SASA ENDELEA
Mke wa Waziri Mkuu alifungua mlango wa gari akajipakia. Alifungua mkoba wake akatoa kitambaa na kuifuta midomo ya Sofia kisha alikikunja kitambaa hicho na kukirudisha kwenye mkoba.
Waziri Mkuu hakuingia kwenye gari. Alibaki nje ya gari akihaha huku na huku. Baadhi ya wauguzi na madaktari walikuwa wakitoka na kuingia ndani ya hospitali hali iliyoonesha taharuki.
Hakukuwa na yeyote miongoni mwao aliyefahamu nini kimetokea.
Muda usio mrefu, magari matatu ya polisi na makachero yakawasili. Gari la kwanza lilikuwa la mkurugenzi wa Upelelezi. Gari la pili lilikuwa na mchanganyiko wa makachero na polisi na gari la tatu lilitoka kituo kikuu cha polisi baada ya polisi walokuwa wakifuatana na Waziri Mkuu kuwapigia radio call.
Polisi na makachero hao waliokuwa zaidi ya kumi walishuka na kusogea alipokuwa amesimama Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alimueleza Mkurugenzi wa upelelezi kuhusu tukio lililokuwa limetokea akimuhusisha Dk Deo kumshambulia muuguzi wake.
“Polisi wamemkamata, yuko kwenye hili gari” alimwambia huku akimuonesha gari hilo.
Akaongeza. “Muuguzi aliyemfanyia unyama huo yuko ofisini kwake”
Mkurugenzi wa Upelelezi alisogea kwenye gari hilo akamtazama Dk Deo kisha alimwambia atoke kwenye gari. Alipotopka alimwambia.
“Twende ukatuoneshe huyo muuguzi wako”
“Lakini mimi sijamfanyia kitendo chochote kibaya, nilimkuta ofisini kwangfu akiwa ameshajeruhiwa” Dk Deo alijitetea.
“Muongo mkubwa. Nilimuona kwa macho yangu akimpopotoa” Waziri Mkuu alisema.
Mkurugenzi wa Upelelezi akampiga kibao Dk Deo kabla ya kumwambia.
“Twende ukatuoneshe huyo muuguzi wako”
Kabla ya Dk Deo kuinua hatua alitandikwa kibao kingine na kusukumwa. Mkurugenzi wa Upelelezi alikuwa amemshika kiunoni.
Wakati Dk Deo akiwapeleka ofisini kwake, Waziri Mkuu alifuata nyuma.
Walipofika ofisini humo, Waziri Mkuu aliwaonesha yule muuguzi aliyekuwa amelala chini. Ile damu iliyokuwa ikimvuja shingoni sasa ilikuwa imeganda.
“Huyo achukuliwe apelekwe hospitali ya Muhimbili kufanyiwa
uchunguzi” akawambia.
Baada ya polisi kumkagua na kumpiga picha, walimbeba na kutoka naye. Alipakiwa kwenye gari mojawapo la polisi. Dk Deo alipakiwa kwenye gari jingine.
Makachero kadhaa pamoja na polisi walibaki pale hospitali na kuanza kuwahoji madaktari wengine na wauguzi kuhusu kilichokuwa kimempata mwenzao.
Mwili wa muuguzi huyo ulipelekwa hospitali ya Muhimbili. Dk Deo alipelekwa kituo kikuu cha polisi. Waziri Mkuu, mke wake pamoja na Sofia waliondoka na kurudi nyumbani.
Walimuacha Sofia aende akalale chumbani mwake. Waziri Mkuu na mke wake wakakaa sebuleni.
“Kama nisingetumia mbinu ile ya kumsingizia yule dakatari, leo Sofia angebainika kuwa ndiye mfyonza damu na angekamatwa kutokana na ushahidi wa yule dokta” Waziri Mkuu alimwambia mke wake.
“Angekamatwa kwa sababu ingeonekana wazi kuwa ndiye aliyemfyonza damu. Aliondoka naye kule chumbani akangoja alipoingia mle ofisini akamshika…”
“Hili sasa limekuwa balaa!”
Mke wa Waziri Mkuu akatikisa kichwa.
“Sijui kama mwanangu atarejea katika hali yake ya kawaida!” alisema na kuongeza.
“Juhudi kubwa zimefanyika lakini bado hali inatia mashaka, sijui tufanye nini?’
“Sijui mke wangu, nimechanganyikiwa! Yaani nimelazimika kuokoa jahazi kwa kumbambikia yule daktari kosa la Sofia”
“Kwani atashitakiwa?’
“Lazima ashitakiwe kwa mauaji, najua tutapambana sana mahakamani lakini nitatumia kila mbinu kuhakikisha haepuki ile tuhuma”
“Sasa Sofia tutampeleka wapi?”
“Tutamrudisha kijijini akae huko huko chini ya uangalizi. Tutakodi watu wa kuwa naye wakati wote kuhakikisha hafyonzi watu. Ile damu inaweza kumuua. Damu nyingine si salama”
Ili kumkandamiza zaidi Dk Deo, Waziri Mkuu alimpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani akamueleza kuhusu lile tukio akidai alimshuhudia kwa macho yake Dk Deo akimfyonza damu muuguzi wake hadi kumuua.
Baada ya kumpigia Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri Mkuu alimpigia Mkuu wa Jeshi la Polisi.
“Nimeshapata taarifa mheshimiwa na hivi sasa tunalifanyia uchunguzi tukio hilo” Mkuu wa Jeshi la Polisi alimwambia Waziri Mkuu mara tu alipomdokeza kuhusu tukio hilo.
“Kama mmeanza kufanya uchunguzi ni vizuri. Yule mtu ni katili sana”
“Kumekuwa na matukio ya ufyonzwaji damu hapa nchini, tutachunguza kuona kama ni yeye aliyehusika”
“Itakuwa ni yeye, wasomi wengine wanafanya kazi zao kwa kutegemea ushirikina”
“Hilo suala tunalifanyia kazi mheshimiwa”
“Tunataka haki itendeke na mhakikishe kwamba anapelekwa mahakamani mara tu uchunguzi wenu ukikamilika”
“Asante mheshimiwa”
Wakati huo hospitali ya Dk Deo ilikuwa imezingirwa na makachero na kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi. Mwili wa muuguzi aliyefyonzwa damu na Sofia ulifanyiwa uchunguzi haraka haraka katika hospitali ya Muhimbili na matokeo ya uchunguzi huo yalitolewa kwa polisi.
Uchunguzi huo mbali ya kuthibitisha kifo cha muuguzi huyo ulieleza kuwa kifo hicho kilitokana na marehemu kufyonzwa damu nyingi mwilini mwake kupitia katika jereha lililokuwa kwenye shingo yake ambalo lilitokana na kuumwa meno ya binaadamu.
Taarifa hiyo ya madaktari ndio iliowapa polisi taharuki. Ile dhana kwamba Dk Deo ndiye mfyonza damu za binaadamu iliwafanya polisi wamng’ng’anie kama ruba.
Mbali ya hospitali yake kuwekwa chini ya ulinzi wa polisi, makachero walianza kuwahoji madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo.
Madaktari na wauguzi wote waliohojiwa walieleza kuwa hawakuliona tukio hilo linalodaiwa kufanywa na Dk Deo.
Pia walieleza kwamba hawaamini kuwa Dk Deo anafyonza watu damu.
Baada ya kutoridhishwa na maelezo ya madaktari na wauguzi hao, makachero walianza kuwahoji wagonjwa waliokuwa wamelazwa katika hospitali hiyo.
Wagonjwa hao pia hawakuwa na maelezo ya kuwatosheleza polisi kuhusiana na tuhuma zilizokuwa zinamkabili Dk Deo. Mkurugenzi wa Upelelezi akaja na dhana nyingine. Aliwataka makachero hao kuifanyia upekuzi hospitali hiyo kwa hofu kwamba Dk Deo anaweza kuwa ananunua viungo vya binaadamu ambavyo anavitumia katika shughuli zake za kishirikina.
Upekuzi huo ulifanywa lakini hakukuwa na kiungo chochote kilichopatikana.
Dk Deo mwenyewe alihojiwa kwa saa kadhaa. Alichokuwa akikieleza kilikuwa hakikubaliwi na polisi ambao tayari walishajenga hisia kwamba Dk Deo ni mfyonza damu.
Dk Deo alieleza kwamba wakati tukio hilo linatokea hakuwepo ofisini. Lakini wakati anarudi ofisini mwake alimuona Sofia binti wa Waziri Mkuu akitoka ofisini mwake.
“Nilipoingia ofisini mwangu nikamuona muuguzi wangu akiwa chini huku akitokwa na damu shingoni. Nilipomchunguza vizuri nikagundua kuwa alikuwa na jeraha ambalo sikuweza kujua ni la kitu gani.
“Nikaondoka pale pale kumfuata yule msichana aliyetoka mle ofisini ili nimuulize nini kilitokea ndio hapo nilipomuona Waziri Mkuu na mke wake wamesimama mbele ya mlango wakinitazama. Waziri Mkuu akaanza kunishutumu kuwa nimemfyonza damu muuguzi wangu jambo ambalo si kweli”
“Sofia binti wa Waziri Mkuu alikuwa amefuata nini ofisini kwako?” Thabit kembo, mmoja wa makachero waliokuwa wakimhoji Dk Deo alimuuliza.
“Sijui”
“Je wewe ulikutana na Waziri Mkuu alipofika hospitalini kwako?’
“Sikukutana naye na wala sikuwa na taarifa kuwa waziri Mkuu anakuja hospitalini kwangu”
“Baada ya Waziri Mkuu kukwambia kwamba amekuona umemfyonza damu muuguzi wako, alichukua hatua gani?’
“Aliita polisi wanikamate na hakunipa nafasi ya kujitetea”
 
ITAENDELEA kesho hapa hapa kumekucha.com

No comments:

Post a Comment