Friday, November 10, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 26


MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 26
ILIPOISHIA
Sofia akatikisa kichwa kusikitika.
Pakapita ukimya wa sekunde kadhaa.
“Sasa wewe nenda zako kajisomee. Hao polisi wakifika utaitwa”
“Sawa baba. Watakuja muda huu?’
“Muda wowote kutoka sasa”
“Haya, mimi nakwenda”
Sofia akanyanyuka na kuondoka. Akili yake ilikuwa imeshachanganyikiwa. Tangu alipoanza kufyonza watu alikuwa akisikia harufu ya damu midomoni mwake mara tu anaporejewa na akili yake.
Alipomfyonza mpishi wa nyumbani kwao alisikia harufu ya damu midomoni mwake. Alipomfyonza dada yake alisikia harufu ya damu midomoni mwake. Alipomfyonza mwanafunzi mwenzake alisikia harufu ya damu midomoni mwake na alipomfyoza muuguzi wa hospitali ya Dk Deo pia alisikia harufu ya damu.
SASA ENDELEA
Ingawa hakuwa na kumbukumbu zozote kichwani mwake za kumfyonza mtu damu lakini hali ile ilimpa maswali mengi.
Alikuwa akijiuliza kwanini linapotokea tukio kama lile, yeye anasikia harufu ya damu midomoni mwake?
Mawazo yake yalikwenda mbali zaidi, akajiuliza ni kwanini alikatizwa masomo baada ya tukio la kufyonzwa damu kwa mwanafunzi mwenzake? Kwanini alipelekwa kijijini na kuaguliwa? Kwanini wakati fulani alipelekwa Nairobi kupimwa akili yake?
Maswali  yote hayo yalipitita akilini mwa Sofia bila kuwa na majibu.
Akaingia chumbani mwake na kuendelea kujisomea.
Baada ya saa moja makachero wawili wakawasili nyumbani kwa Waziri Mkuu.
Kachero Kembo na Inspekta Alex walikaribishwa sebuleni kwa Waziri Mkuu.
Wakaeleza dhumuni lao kuwa ni kupata maelezo kutoka kwa Waziri Mkuu, mke wake na mwanawe kuhusiana na tukio lililotokea katika hospitali ya Dk Deo, asubuhi ya siku ile.
Waziri Mkuu akawafahamisha kuwa walikuwa tayari kutoa maelezo.
Thabit Kembo alifungua jalada alilokuwa nalo mikononi akaandika tarehe ya siku ile kisha akaandika jina la Waziri Mkuu.
“Mheshimiwa tutaanza na wewe” kembo akamwambia baada ya kuandika.
“”Anza”
“Tunaomba utueleze nini kilitokea katika hospitali ya Dk Deo leo asubuhi”
“Sisi tulifika pale hospitali kumjulia hali rafiki wa mwanangu na mwanafunzi mwenzake ambaye anaumwa”
“Mwanao huyo anaitwa nani?” Kembo akamuuliza.
“Anaitwa Sofia”
“Na huyo mgonjwa mliyekwenda kumjulia hali ni nani?”
“Anaitwa Maria, ni mdogo wake Dk Deo”
“Dk Deo huyu ambaye amehusika na hili tukio?”
“Ndio”
“Endelea”
“Nataka uelewe kwamba tulikwenda pale kama raia wa kawaida kumjulia hali mgonjwa”
“Ndiyo”
Waziri Mkuu akaendelea kueleza jinsi walivyomuona mgonjwa huyo wakiongozwa na muuguzi mmoja wa hospitali hiyo ambaye hakuwa akimfahamu jina lake.
Akaendelea kueleza baada ya kumuona mgonjwa walihitaji kupata maelezo kutoka kwa daktari anayemtibu kwa vile mgonjwa mwenyewe bado hakuwa na hali nzuri na hakuweza kutoa maelezo.
“Muuguzi tuliyekuwa naye alitoka mle chumbani kwenda kumuita daktari lakini alichelea sana kurudi kiasi kwamba tuliamua kutoka kumfuata” Waziri Mkuu aliendelea kueleza.
“Wakati huo mlikuwa watu wanagapi?’
“Nilikuwa mimi, mke wangu na mwanangu Sofia”
“Endelea kueleza, baada ya kutoka nini kilitokea?”
“Tulipofika katika mlango wa ofisi ya Dk Deo, tuliukuta mlango ukiwa wazi. Tukamuona Dk Deo akiwa ndani ya ofisi yake amemshikilia yule muuguzi huku meno yake yakiwa kwenye shingo ya muuguzi huyo na pale shingoni palikuwa panatoka damu” Waziri Mkuu alieleza.
“Ulihisi alikuwa anamfanya nini?”
“Nilihisi kama alikuwa anamfyonza damu”
“Baada ya hapo nini kilitokea?’
“Yule muuguzi alianguka chini, ndipo nilipomuuliza Dk Deo unafanya nini? Akaanza kubabaika. Hakujua kuwa kulikuwa na watu wanamuona?”
“Baada ya kumuuliza hivyo na kubabaika, ulichukua hatua gani?’
“Nilipiga simu polisi, polisi wakafika na kumchukua”
Kembo alimaliza kuandika maelezo ya Waziri Mkuu kisha alimwambia.
“Dk Deo baada ya kuhojiwa alitupa maelezo tofauti”
“Aliwambia uongo gani?” Waziri Mkuu akamuuliza huku macho yake yakimeta kwa taharuki.
“Alitueleza kwamba, yeye hakuwako ofisini kwake lakini wakati anarudi ofisini kwake alimkuta Sofia akitoka mle ofisini…”
“Huo ni uongo mtupu, Sofia tulikuwa naye sisi” Waziri Mkuu akadakia.
“Alitueleza kwamba licha ya kwamba yeye na Sofia walikua wanajuana lakini Sofia hakumsemesha chochote, alimpita kama vile alikuwa hamjui. Alipoingia ofisini kwake ndipo alipomkuta yule muuguzi amelala chini huku damu ikitoka kwenye shingo yake…”
“Yule dakatari ni muongo sana tena hafai kabisa. Sisi tumemuona waziwazi akifanya unyama wake halafu anamsingizia mwanangu! Mwanangu alifuata nini ofisini kwake wakati tulikuwa naye sisi?” Waziri Mkuu alifoka.
“Sawa. Tutachukua pia maelezo kutoka kwa Sofia lakini kabla ya yeye ni vizuri pia tupate maelezo ya mama yake kwa vile alikuwepo katika tukio”
“Sawa”
Kembo akamgeukia mke wa waziri Mkuu.
“Tupe maelezo yako, nini ulikishuhudia hapo hospitali asubuhi”
Mke wa Waziri mkuu alieleza kama alivyoeleza mume wake. Kembo baada ya kumaliza kuandika alitaka aitwe Sofia.
Mama yake ndiye aliyekwenda kumuita. Alimkuta Sofia amepitiwa na usingizi. Akamuamsha na kumwambia kuwa maafisa wa upelelkezi wameshafika kuchukua maelezo ya tukio lililotokea katika hospitali ya Dk Deo.
“Haya mama nakuja” sofia akamwambia.
Mke wa Waziri Mkuu aliporudi sebuleni Sofia alikuwa nyuma yake.
“Kaa kwenye kochi” Waziri Mkuu alimwambia.
Sofia akakaa.
“Hujambo?” Kembo akamsalimia.
“Sijambo, habari ya kazi?’
“Nzuri, za masomo?’
“Pia ni nzuri”
“Sawa. Sisi ni maafisa wa idara ya polisi ya upelelezi. Tunahitaji maelezo yako kuhusiana na tukio lililotokea leo asubuhi kwenye hospitali ya Dk Deo. Uko tayari kutueleza nini kilitokea?’
“Niko tayari”
“Sawa, anza kutueleza”
“Kuna rafiki yangu ambaye amelazwa pale hospitali akiugua malaria. Leo asubuhi tulikwenda kumsalimia…”
“Mlikwenda nani na nani?’
“Mimi, baba na mama”
“Mlipofika mlimuona huyo mgonjwa?”
“Ndio tulimuona”
“Alikuwa na hali gani?”
“Kwa kweli hali yake haikuwa nzuri, alikuwa hawezi hata kuzungumza”
“Endelea kueleza”
“Yule muuguzi aliyetupeleka alikwenda kumuita daktari ili atupe maelezo kuhusu mgonjwa”
“Ndiyo”
Hapo Sofia alisita akawa anafikiria alivyofundishwa na baba yake.
Kitendo hicho kilimuudhi Waziri Mkuu akamkazia macho Sofia.
“Eleza kilichotokea baada ya hapo” akamwambia.
“Ndio naeleza baba. Yule muuguzi hakurudi tena” Sofia akasema huku akiendelea kufikiri.
“Mlichukua hatua gani?” Kembo akamuuliza.
“Na sisi tukatoka kumfuata daktari”
“Mlimfuata wapi?”
“Ofisini kwake”
“Je mlimkuta?”

ITAENDELEA kesho Usikose Uhondo huu hapahapa kumekucha.com

No comments:

Post a Comment