RIWAYA
KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI 15
ILIPOISHIA
“Umesikia, umeambiwa kama
unataka kuwakomboa mama yako na mwanao utoe ngo’ombe dume mweusi”
“Nimtoe wapi?” nikamuuliza.
“Umtoe hapa hapa” Ile sauti
ndiyo iliyojibu.
“Yaani utuletee ng’ombe
mweusi kabla hujarudi kwenu” Maalim akanifafanulia.
“Utanionesha wanapouzwa.
Nitanunua mmoja nimlete”
“Kama mmekubaliana mimi
naondoka” Ile sauti ikatuambia na hapo hapo kile kivuli kikatoweka.
“Basi twende zetu,
tumeshapata ufumbuzi” Maalim akaniambia.
Tukaondoka na Maalim.
Tulipofika kwa yule mtu mwingine Maalim alimwambia.
“Asubuhi utampeleka huyu mtu akanunue
ng’ombe dume mweusi, mje naye hapa”
“Sawa”
SASA ENDELEA
Baada ya hapo Maalim akaenda
zake na sisi tukarudi kwenye kile kibanda.
Kusema kweli ile nilioiona
kwenye ule mti ilikuwa miujiza mikubwa kwangu. Niliamini kweli pale mahali
palikuwa pa hatari.
Asubuhi kulipokucha
nilimuuliza yule mzee, ng’ombe anauzwa kiasi gani pale kijijini kwao.
“Hapa kijijini kwetu ng’ombe
wanauzwa kuanzia shilingi laki nne hadi laki tano. Ni ghali sana” Mzee huyo
akanijibu.
Nikanyamaza kidogo.
Nilinyamaza kufikiria kwamba mfukoni kwangu sikuwa na kiasi hicho cha fedha na
awali sikufikiria kama bei ya ngombe ingekuwa kubwa kiasi hicho kwa vile pale
palikuwa ni kijijini.
“Mbona umenyamza?” Yule mzee akaniuliza.
“Nilikuwa nafikiria. Pesa
nilizokuja nazo ni chache sana mpaka niende nikachukue benki”
“Hapa kijijini kwetu hakuna
benki mpaka uende mjini”
“Si kitu, nitakwenda mjini
kwenye ATM nikatoe”
“Kwa hiyo tukusubiri?’
“Ndiyo mnisubiri, sitachelewa
kurudi”
Nilifanikiwa kupata mahali
palipokuwa na ATM katika mji wa chake chake. Ilikuwa kwenye hoteli moja ya
kitalii ambako nilikuta wazungu wengi.
Kwa vile kadi yangu ya benki
nilikuwa nayo, nilitoa shlingi milioni moja ambayo ilikuwa akiba yangu
iliyokuwa benki. Baada ya kupata pesa hizo niliingia hotelini humo kupata
kifungua kinywa.
Wakati nakunywa chai,
nilijiambia nitakapomaliza shughuli nzima niliyoagizwa kule Kisima cha Giningi,
hapatakuwa na cha kuniweka tena pale Pemba.
Ilinibidi niharakishe kurudi
Tanga ili kumuepushia usumbufu mke wangu atakapokuja Korogwe.
Kwa upande mwingine
nilifurahi lile suala langu kupata ufumbuzi kwani licha ya kumuokoa mke wangu,
mama yangu na mwanangu watasalimika na kuwa wazima.
Nilijiambia nitakuwa na
furaha kumuona mama yangu na mwanangu wakiwa wazima.
“Najua watu watawashangaa kwa
sababu mama yangu na mwanangu walishakufa lakini nitawambia watu kuwa hawakuwa
wamekufa bali walichukuliwa msukule na sasa wamerudi” nikajiambia.
“Najua wako watakaoamini na
wako ambao hawataamini lakini jibu langu litakuwa hilo” niliendelea kujiambia.
Baada ya kumaliza kifungua
kinywa, nilitoka nikatafuta usafiri wa kunirudisha Kendwa. Muda wa saa moja
nikawa nimeshafika katika kijiji hicho. Kijana wa bodaboda akanipakia kwenye baskeli
na kunipeleka huko kilikokuwa Kisma cha Giningi.
Nilipokwenda katika kile
kibanda nikamkuta yule mzee.
“Umesharudi?” akaniuliza kwa
uchangamfu.
“Ndiyo mzee, nimerudi”
“Umefanikiwa kupata pesa?”
“Ndiyo nimepata, sasa twende
tukanunue huyo ng’ombe”
“Sawa. Twenzetu”
Tukaondoka na yule mzee kuelekea
katika kijiji kingine ambako aliniambia ng’ombe anayehitajika angeweza
kupatikana.
Tukiwa njiani tukitembea kwa miguu nilimwambia mzee
huyo kuwa nilitaka ile shughuli ikamilike mapema ili niwahi kurudi Korogwe.
“Unaharakisha nini?”
akaniuliza.
“Si nilikwambia mke wangu
atakuja Korogwe kutoka Dodoma.
Nilipendelea nisipishane naye sana”
“Sasa kuwahi kwako kurudi
itategemea kumalizika hii shughuli”
“Unadhani inaweza kuchukua
muda gani?”
“Siwezi kujua. Anayejua ni
Maalim mwenyewe”
“Kama
nitalazimika kulala tena huku itakuwa ni mtihani kwangu”
Nilipomwambia hivyo mzee huyo
alinitazama tu bila kuniambia kitu. Jambo lile lilinipa ishara kwamba huenda
shughuli iliyobaki ikawa ndefu kiasi cha kunilazimisha kulala tena Pemba.
Nikajiambia kama mke wangu atakuja
korogwe kama alivyoniambia, huenda akakutana
na matatio kwa vile yule jini aliyetaka kumtoa kafara mke wangu alikuwa bado
yuko nyumbani.
Nilipoona mzee amenyamaza na
mimi nikanyamaza. Tulipofika katika kijiji hicho tulifanikiwa kupata ng’ombe
dume mweusi kwa gharama ya shilingi laki
tano. Wakati natoa kile kitita cha noti niliona yule mzee amezikodolea macho
zile pesa huku macho yake yakimwekamweka.
Baada ya kumnunua ngombe huyo
tulimkabidhi kwa watu wanaoswaga ng,ombe ili waende naye katika kile kijiji
tulichotoka.
Mimi na yule mzee
tukatangulia kurudi kwa miguu. Tukiwa njiani nilimuuliza yule mzee kama ile kazi ingekuwa na gharama yoyote.
“Utamuuliza Maalim mwenyewe”
Mzee akanijibu.
Kwa vile alikuwa amechoka kwa
mwendo nilitoa noti mbili za shilingi elfu kumi kumi nikampa ili kumtia nguvu.
“Mzee na wewe chukua hizi,
umenisaidiaa sana”
Mee huyo alizipokea pesa hizo
na kunishukuru.
“Ondoa wasiwasi, utafanikiwa
tu” akaniambia.
“Unaamini kwamba matatizo yangu
yatakwisha kabisa?” nikamuuliza kwa matumaini.
“Yatakwisha tu. Yule jini
atarudishwa kwao na wewe utakuwa salama”
“Kwa hiyo mke wangu
hatadhurika?”
“Na mama yako pamoja na mtoto
wako pia watasalimika kwa vile umezikataa zile pesa za majini. Zile pesa zina
taabu lakini watu hawajui tu”
Tuliporudi pale kijijini
tulikwenda kwa Maalim na kumjulisha kuwa tumeshanunua huyo ng’ombe aliyetakiwa.
“Mmekuja naye?” Maalim
akatuuliza.
“Analetwa na mswagaji wa
ng’ombe” Mzee akamwambia.
Tukasubiri mpaka saa tisa, ng’ombe
huyo alipoletwa pale kijijini. Maalim alipomuona aliuliza.
“Ng’ombe mwenyewe ndiye
huyu?”
“Ndiye huyo” Mzee akamjibu.
“Haya. Sasa shika kamba yake
uende naye ukamfunge pale kwenye ule mti” Maalim akaniambia akinionesha ule mti
tuliokwenda usiku wa jana yake.
“Nimfunge tu kisha nimuache?” nikamuuliza.
“Mfunge umuache hapo hapo”
Nikaishika kamba ya ng’ombe
huyo na kuanza kumkokota kuelekea katika ule mti. Kwa vile sikuzoea kukokota
ng’ombe kazi hiyo haikuwa rahisi. Ng’ombe alikuwa mbishi na mara kwa mara
nililazimika kumvuta.
Nilipofika kwenye huo mti
nilimfunga ng’ombe huyo kwenye mti huo kisha nikarudi.
“Nimeshamfunga” nikamwambia
yule Maalim.
“Sasa unaweza kwenda zako”
akaniambia. Kwa kweli nilifurahi.
“Kwa hiyo nikifika nitawakuta
wale watu wameshakuwa wazima?” nikamuuliza nikimaanisha mama yangu na mwanangu.
“Umeshawafanyia kafara lao,
watakuwa wazima tu”
“Na mke wangu hatadhurika
tena?”
“Mke wako hawezi kupata
madhara”
“Nashukuru sana. Sasa je zile pesa nizipeleke wapi?”
Maalim alinipa jibu lililonishangaza.
“Wewe achana nazo na usitumie
hata senti moja. Watajua majini wenyewe. Na si pesa tu, kila kilichonunuliwa
kwa pesa hizo achana nacho. Si mali
yako tena”
“Mimi sijui ni kitu gani na
gani kimenunuliwa kwa pesa hizo”
“Ukirudi Korogwe utajua. Kile
ambacho kimenunuliwa kwa pesa za majini watakichukua wenyewe”
“Sawa. Ninachotaka mimi ni
mama yangu na mwanangu kuwa wazima”
“Hilo halina shaka, wamekuhakikishia wenyewe”
“Nitashukuru kama itakuwa
hivyo. Pia nataka kujua ninatozwa kiasi gani kwa kazi hii”
“Hapa hatutozi mtu gharama
ila chochote utakachopenda kunipa kitakuwa kama
sadaka yako”
“Sawa”
Nikatia mkono mfukoni na
kutoa shilingi laki moja nikampa. Maalim alinishukuru sana.
Baada ya hapo tukaagana
nikaondoka. Wakati niko njiani kwenda kupanda bodaboda nilikutana na watu
watatu, wawili wanaume, mmoja mwanamke. Nilishuku tu kuwa walikuwa wakielekea
kule Kisima cha Giningi.
Watu hao walioonekana kuwa
wageni walinisalimia na mmojawapo akaniuliza.
“Eti bwana, huku tunakoelekea
ndiko kilipo Kisima cha Giningi?”
“Ndiyo huko huko” nikamjibu.
No comments:
Post a Comment