Wednesday, November 1, 2017

RIWAYA, KAMA UNATAKA PESA ZA MAJINI SEHEMU YA 12

RIWAYA

KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI 12

ILIPOISHIA

Yule mzee akaingia ndani ya ile nyumba na kutoka  na kiti akaniwekea na kuniambia.

“Karibu ukae”

Nikakaa mbele ya yule maalim.

“Haya nieleze shida yako”

Nikaanza kumueleza mtu huyo matatizo yangu mwanzo mpaka mwisho.

“Nadhani kulikuwa na makosa yalifanyika kati ya marehemu Habib na baba yako” akaniambia.

“Makosa gani?”

“Huyo jini alimuhusu baba yako tu na hizo pesa zilimuhusu baba yako tu. Lakini bila shaka baba yako alikutaja wewe kama mrithi wake na ndio maana huyo jini alikufuata. Sasa kwa bahati mbaya mzee Habib ameshakufa”

“Nimeambiwa kuwa wewe ndiye mrithi wake. Nilitarajia kuwa ungeweza kunisaidia”

“Kwani usichotaka wewe ni kitu gani, ni pesa au jini?” akaniuliza.

“Silitaki hilo jini?”

“Na pesa je?”

SASA ENDELEA

“Kama zitakuwa na masharti pia sizitaki”

“Lakini si umeshazitumia?”

“Sijatumia hata senti moja”

“Nikikwambia uende ukazigawe pesa hizo uwape maskini mia moja utaweza?”

“Sitaweza. Kijijini kwetu siwezi kupata masikini mia moja”

“Unaweza kupata wangapi?”

“Labda kumi tu”

“Wewe mwenyewe unafanya kazi gani?”

“Mimi ni askari”

Maalim huyo akashituka.

“Ni askari gani?”

“Ni askari wa jeshi la ulinzi”

Maalim akanyamaza kimya. Baada ya sekunde chache hivi akaniambia.

“Kama nitamchukua huyo mnyama hutabaki na kitu chochote”

“Sijakuelewa, unamaanisha mnyama gani?” nikamuuliza.

“Huyo jini”

“Na umesema sitabaki na kitu chochote kivipi?”

“Yaani hizo pesa na kila kitu kilichonunuliwa kutokana na pesa hizo kitapotea hata kama ni nyumba”

“Sawa”

“Uko tayari?”

“Niko tayari”

“Sasa utalala hapa kwangu hadi kesho”

“Sawa”.

Yule maalim akamgeukia yule mzee niliyekwenda naye ambaye alikuwa amesimama muda wote.

“Shaali mtafutie mahali pa kulala hadi saa nane usiku utamleta” akamwambia.

“Haya inuka twende nikupeleke mahali utakapolala”

“Kwani hapa  karibu hakuna gesti?”

“Huwezi kwenda kulala mahali kwingine kwa sababu usiku nitakuhitaji” Maalim akaniambia.

“Sawa, nimekuelewa”

Yule mzee alinipeleka katika kibanda kingine kidogo akaniambia “Tutalala sote hapa”

Yalikuwa mazingira ya kutisha lakini kwa vile nilikuwa na shida ilibidi nikubali.

Ni vyema nikiri kuwa yule mzee alinishughulikia sana. Kabla ya kuingia ndani ya kibanda hicho, alinitayarishia maji nikaenda kuoga kwenye choo cha kienyeji.

Nilipotoka kuoga nilikuta amekoka moto nje ya kile kibanda kwa kutumia vipande vya miti akaniambia tukae tuote moto.

Wakati tumekaa tukiota moto huku tukipiga stori za hapa na pale aliinuka na kuniambia nimsubiri. Akaondoka na kuniacha peke yangu.

Baada ya muda kidogo alikuja akiwa ameshika sinia la chakula akaliweka chini mbele yangu. Harufu ya chakula hicho ikanipitia puani mwangu, ilikuwa ni pilau.

Alipoweka ile sinia aliondoka tena. Baada ya muda kidogo alirudi tena akiwa na jagi la maji, bilauli na kisufuria. Akaninawisha mkono kisha na yeye akanawa.

“Karibu chakula” akaniambia.

Tukala pamoja pilau ile ambayo niliipenda sana kwani ilipikwa kipwani na kutiwa viungo mbalimbali vilivyotia ladha na hurufu ya kuvutia.

Baada ya kula tulinawa mkono. Mwenyeji wangu akanipa maji ya  kunywa, nikanywa na yeye akajitilia na kunywa.

Baada ya hapo aliinuka na kuondoa vyombo. Wakati nimebaki peke yangu, nilitoa simu yangu niliyokuwa nimeizima nikaiwasha.

Nilitega kama kulikuwa na meseji zozote zilizotumwa niweze kuzipata. Baada ya muda kidogo tu zikaingia meseji tatu kwa mfululizo.

Meseji zote hizo zilitoka kwa mke wangu ambaye ndiye niliyemzimia simu. Meseji aliyoituma kwanza alihoji kwanini sipatikani.

Meseji ya pili aliniuliza kwanini ninazima simu wakati nilimuahidi kumtumia nauli ya kuja korogwe?

Meseji ya tatu alinishutumu kwamba nilikuwa sitaki aje Korogwe kwa sababu nilikuwa na mwanamke lakini ameshakopa nauli na kesho yake asubuhi ataondoka Dodoma kuja Korogwe.

Wakati nazifikiria hizo meseji, tayari mke wangu alishagundua kuwa nimewasha simu kutokana na zile meseji alizotuma kurudisha majibu.

Hapo hapo akanipigia. Nikapokea simu yake.

“Sasa ndio umenifanyaje?” mke wangu akaniuliza kwa kufoka.

“Mbona umekuwa mkali?”

“Nisiwe mkali kwanini wakati unanifanyia mambo yasiyoeleweka. Umeahidi ungenitumia nauli tangu mchana. Mpaka huu usiku umezima simu. Una maana gani?”

“Wewe unakuwa mkali kwa sababu unadhani mimi nina mwanamke lakini amini usiamini mimi sina mwanamke zaidi yako wewe. Simu yangu ilizimika kwa sababu ilikuwa na hitilafu” nikasema uongo.

“Sasa kwanini hukunitumia hizo pesa za nauli tangu mchana?”’

“Ningekutumia kwa njia gani wakati simu yangu ilizima!”

“Huo ni ujanja wako tu lakini kama nilivyokwambia kwenye hizo meseji, ninakuja kesho. Naondoka hapa saa kumi na mbili asubuhi. Sasa kama ni simu imezimika au kuna kingine tutakuja kujuana huko huko”

“Kwanini usije kesho kutwa?” nikamuuliza.

Nilitaka aje hiyo kesho kutwa nikijua kuwa ningekuwa nimesharudi Korogwe na pengine lile tatizo lililonipeleka Pemba litakuwa limeshapatiwa ufumbuzi.

“Nakwambia ninakuja kesho, nimeshakata tikiti ya basi” mke wangu akasisitia.

“Sasa mimi nilikuja Dar mara moja, hutanikuta” nikatunga uongo mwingine.

“Lakini ni kwanini unasumbua akili yanngu!”

“Unajisumbua mwenyewe. Mimi nataka  tuelewane, uje kesho kutwa nitakuwa nimesharudi Korogwe”

“Huko Dar ulifuata nini na kwanini hukuniambia kama unakwenda Dar?”

“Niliitwa mara moja na mkuu wangu wa kazi”

“Mkuu wako wa kazi anakuita wakati uko likizo?”

Mke wangu aliponiona nimesita aliniuliza. “Mume wangu mbona unajichanganya?”

Sikuwa hata na la kumjibu. Nikamuona yule mwenyeji wangu anarudi. Sikutaka asikie yale maneno niliyokuwa nazungumza na mke wangu.

“Mke wangu si unazijua kazi za uaskari, ni kazi za amri tu” nikamwambia baada ya kimya kifupi.

“Sasa mimi nakwambia uwe Dar, uwe Korogwe ninakuja. Nitalala hata kwa majirani”

Mke wangu aliponiambia hivyo akakata simu. Kwa upande mwingine nilishukuru alipokata simu ingawa aliikata kwa hasira. Yule mwenyeji wangu alikuwa ameshafika.

“Ulikuwa unazungumza na nani?” akaniulia huku akiketi.

“Nilikuwa nazungumza na mke wangu. Alikuwa ananiuliza kama nimefika salama”

“Sasa tuote moto halafu twende tukalale” akaniambia.

Kichwa changu kilikuwa kimeshavurugika. Nilijiambia  kama mke wangu atakwenda Korogwe, anaweza kupata madhara kwa vile sikuwa nikijua lile tatizo langu lingekwishaje usiku ule.

Kwa vile sikutaka yule mzee ajue kuwa nilikuwa nimefadhaika, tukaanza kuzunguma.

Tulizungumza mengi kuhusu kile kisima cha Giningi. Aliniambia yeye alizaliwa wakati wa utawala wa sultani na hicho kisima allikikuta hivyo hivyo.

“Haijulikani ni nani alikichimba na kilichimbwa wakati gani” aliniambia.

“Huenda kilichimbwa miaka mingi iliyopita. Baba yangu aliniambia alikikuta hivyo hivyo” akaongeza.

“Unadhani hapo kilipochimbwa kilichimbwa kwa madhumiuni gani?” nikamuuliza ili kupata undani wa kisima  hicho.

“Nafikiri kilichimbwa na wenyeji wa wakati huo ili kupata maji ya kutumia”

“Mpaka hii leo watu wanateka maji?”

“Hivi sasa hakitumiki tena”

Itaendelea kesho hapa hapa kumekucha.com

1 comment:

  1. NDAGU YA MALI KWA (MASHARTI) NDANI YA MASAA 72(SIKU TATU) PAPO HAPO KIKUBWA UWE MWAMINIFU, JASILI NA UWE NA UTAYARI WA KUPOKEA MASHARTI YA KUTUNZA SIRI HII SIO MZAHA......

    (HUSITUME SMS PIGA SIMU KUHEPUKA MATAPELI)

    PUUZA UONGOFU WA KUWA MTU KUWA TAJIRI NI DHAMBI WAKATI AKUAMBIAE YEYE NI TAJIRI (Tumia ufahamu kujinasuaUTAJIRI WA

    NAITWA DR, MDIRO piga 0742162843. KAMA UNAITAJI PESA ZA MAJINI AU NDAGU YA MALI AU ULINZI KWA MALI YAKO

    MATIBABU MENGINEYO NI KAMA UTULIVU KATIKA NDOA, AU KUMVUTA UMPENDAE, KUONDOA MIKOSI, MABALAA, KUOSHA NYOTA, KUITAMBUA NYOTA YAKO NA ASILI YA KAZI YAKE.
    JINI MAHABA NA SHIDA YA UZAZI. NIPIGIE 0742162843. KIKUBWA NI KUSIKILIZA NA KUFATA MASHARTI. ANGALIZO USITUME SMS PIGA NA UWE NA NIA.

    (kuhusu utajiri au pesa) KABLA YA KUPIGA SIMU ZINGATIA YAFUATAYO
    1. uwe una umri wa miaka 18+
    2. uwe tayari kupokea masharti yote
    3.uwe na uwezo wa kutunza siri
    4. uwe jasiri wa kupokea taarifa yoyote
    KARIBU SANA KWA SHIDA NYINGINE PIA ULIYONAYO AMBAYO SIJATAJA INSHAALAH ITATATULIWA IKIWA NDANI YA UWEZO WANGU.

    ReplyDelete