Tuesday, November 14, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI

HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI
ILIPOISHIA
Mke wa Waziri Mkuu alishaanza kushituka.
“Tukio gani tena hilo?”
“Linamuhusu yeye”
“Ndiyo ni tukio gani. Hebu nieleze”
Maria akamueleza mkasa mzima uliotokea tangu alivyomuona Sofia akimfyonza damu mwanafunzi mwenzao ndani ya choo cha shule mpaka polisi walivyofika.
“Mama yangu wee!” Mke wa Waziri Mkuu akamaka.
“Yaani mimi nilishangaa sana, sijui Sofia amepatwa na nini!”
“Huyo mwanafunzi amekufa?”
“Amekufa lakini mwili wake bado uko hospitali”
“Yesu wangu, sasa ikawaje?’
SASA ENDELEA
“Baada ya kile kitendo Sofia alipotoka chooni alikwenda kukaa chini ya mti nyuma ya shule, nikamuuliza Sofia una nini. Akaniambia anasikia kichwa kinamuuma lakini kile kitendo alichokifanya alikuwa hakijui kabisa”
Mke wa waziri Mkuu alikuwa akiguna tu.
“Wakati nazungumza naye, yule mwanafunzi aligunduliwa kule chooni. Walimu wakaenda kumuona. Mkuu wa shule akapiga simu polisi. Polisi wakafika”
“Enhe..?”
“Wanafunzi tukaulizwa nani anayejua kilichompata mwenzetu, kila mmoja akasema hajui lakini mimi sikusema kitu. Nilinyamaza kimya. Wanafunzi wanne waliokuwa wamekaa na Sofia kabla ya tukio hilo wakachukuliwa polisi pamoja na mkuu wa shule”
“Walichukuliwa kama washukiwa au…?’
“Walichukuliwa kwenda kuandikisha maelezo kisha walirudishwa”
“Sofia mwenyewe hakuulizwa kitu?’
“Hakuulizwa kwa sababu hakuonekana, niliyemuona ni mimi peke yangu na sikumwambia mtu”
“Asante sana mwanangu, ngoja nimuite baba yake naye umueleze”
Mke wa Waziri Mkuu aliondoka akaingia ndani. Baadaye kidogo alirudi akiwa amefuatana na mheshimiwa Waziri Mkuu.
“Hujambo Maria?” Waziri Mkuu akamsalimia Maria huku akiketi.
“Sijambo, shikamoo”
“Marahaba. Habari za nyumbani?’
“Nzuri”
“Wazazi hawajambo?”
“Hawajambo”
“Kumetokea nini huko shule?”
“Kumetokea mambo ya ajabu sana?’
“Enhe…hebu nieleze”
Maria akamueleza.
Uso wa Waziri Mkuu ulionesha wazi kutaharuki.
“Mbona sisi hatukupata taarifa yoyote kuhusu Sofia?” akamuuliza Maria.
“Haikufahamika kwamba Sofia ndiye aliyefanya kile kitendo. Nilimuona peke yangu na sikumwambia mwalimu yeyote”
“Huyo mwanafunzi amekufa?’
“Amekufa”
Waziri Mkuu akatikisa kichwa kusikitika.
“Una hakika kwamba uliyemuona akifanya hivyo ni Sofia?”
“Ni Sofia. Baadaye nilimuuliza lakini alionekana kama hajui alichokitenda”
“Labda amepatwa na malaria iliyompanda kichwani”
“Inawezekana kwa sababu alisema kichwa kinamuuma”
Kimoyo moyo Waziri Mkuu alikuwa akijiambia ile juhudi yote iliyofanyika usiku wa jana yake kijijini kwao ambako ngo’ombe watatu walichinjwa kwenye mzimu, hazikuwa na manufaa yoyote.
“Mwanangu umefanya jambo zuri kulifanya jambo hilo kuwa ni siri. Hakuna mtu yeyote uliyemueleza?’ mke wa Waziri Mkuu akamuuliza.
Maria akatikisa kichwa.
“Sikumueleza mtu yeyote. Nimekuja kuwaeleza nyinyi ili mjue kuwa Sofia ana matatizo”
“Asante sana. Imekuwa vyema umemuona wewe rafiki yake, je kama angekuwa mtu mwingine ingekuwaje?” Waziri Mkuu akamuuliza.
“Angesema”
“Ingekuwa ni tatizo”
“Sasa huko alikokwenda sijui itakuwaje?” mke wa waziri Mkuu akauliza kama aliyekuwa akijiuliza mwenyewe.
Hakukuwa na aliyemjibu.
“Alipokuja hapa sisi tulimuona yuko sawa tu” Waziri Mkuu akasema na kuongeza.
“Kama tungegundua kuwa ana tatizo tusingemruhusu kuondoka”
“Tumuombee tu, atarudi salama” Maria akawambia.
“Ametutia wasiwasi sana lakini tunakushukuru wewe kwa kuja kutufahamisha hilo. Kwa hiyo kutoka sasa tutakuwa na tahadhari naye” Waziri Mkuu akasema.
“Sasa mwanangu nakusisitiza sana kuwa endelea kumfichia siri rafiki yako. Usimueleze mtu yoyote. Ujue ukimueleza mtu rafiki yako atakamatwa” Mke wa waziri mkuu akamwambia Maria.
“Sitamueleza mtu yeyote”
“Huyo aliyekufa amekufa kwa sababu muda wake ulikuwa umeshawadia” waziri Mkuu akasema.
“Ni kweli. Kila mtu anakufa kwa wakati wake”
Waziri mkuu alitia mkono ndani ya mfuko wa ndani wa koti lake akatoa kitita cha noti. Alihesabu shilingi laki moja akampa Maria.
“Mwanangu chukua hizi pesa, ni zawadi yako”
“Asante sana, nashukuru”
“Akirudi tutamwambia kuwa rafiki yako alikutembelea lakini hakukukuta”
“Ndio, mumpe salamu zangu”
“Na tutamshughulikia kumpatia matibabu”
“Itakuwa vizuri kwani ile hali inatisha”
Waziri Mkuu alitoa gari lake la binafsi pamoja na dereva wake kumrudisha maria nyumbani kwao Sinza.
Mara tu maria alipoondoka Waziri Mkuu alimwambia mke wake.
“Ule uganga aliofanyiwa haukusaidia kitu”
“Ni hasara tupu”
“Sasa tatizo linakuwa kubwa. Ameanza kufyonza wanafunzi wenzake shuleni. Atasoma vipi?”
“Itabidi tumsimamishe masomo”
“Atakubali?’
“Tutamlazimisha”
“Sawa. Sasa kesho utamzuia mwanano asiende shule hadi hapo tutakapomruhusu. Na mimi nitamtuma msaidizi wangu aende shuleni kuwapa taarifa ya kumsimamisha masomo Sofia kwa ajili ya matibabu ya afya yake” Waziri Mkuu alimwambia mke wake.
“Wakiambiwa kwamba tunamsimamisha masomo kwa ajili ya afya yake watahoji ana matatizo gani”
“Sasa tuwaambieje?”
“Waambiwe tu kuwa tunamsimamisha masomo kwa muda. Unadhani kuna atakayekuhoji?”
“Sidhani”
“Basi iwe hivyo”
Wakati wa magharibi ulikuwa umeshaingia, Sofia aliporudi nyumbani. Alimkuta mama yake sebuleni.
“Mama nimerudi” alimwambia.
“Ma mdogo wako hajambo?”
“Hajambo, anawasalimia”
Sofia akaketi kando ya mama yake.
“Sofia nataka kukuuliza, hivi shuleni kwenu kulitokea nini leo?”
“Hata sijapatiliza, niliona polisi tu. Mkuu wa shule alichukuliwa na polisi pamoja na wanafunzi watano”
 Walipelekwa wapi?”
“Walikwenda kuandikisha maelezo kisha walirudishwa”
“Walikwenda kuandkisha maelezo ya nini?”
“Nilisikia kuna mwanafunzi aliyefia chooni lakini simjui. Mwenyewe kichwa kilikuwa kinaniuma, sikupatiliza”
“Huyo mwananfunzi alikufaje?’
Sofia akabetua mabega yake.
“Sijui mama. Kwani wewe umejuaje?’
“Nimeambiwa”
“Umeambiwa na nani?”
“Baba yako alipigiwa simu akaelezwa”

itaendelea kesho hapahapa Usikose uhondo huu

No comments:

Post a Comment