SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572 , 0655 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 17
ILIPOISHIA
Ndani ya moyo wangu nilishituka
lakini nilijifanya niko kawaida tu
"Unataka uonje kidogo?"
"Nitaonja siku nyingine"
"Ameshayaonja sana. Nimeshamtilia
kwenye mchuzi mara nyingi. Mwenyewe akausifia ule mchuzi akasema ni mtamu
kweli" mke wangu akasema.
Nikashituka tena
"Kumbe wewe pia unayo?"
nikamuuliza Chausiku kwa sauti tulivu ili wasione kuwa nilikuwa mpinzani wa
vitendo vyao
"Nilikuwa nayo, niliyamaliza
jana kwenye mchuzi"
Kumbe nalishwa vingi? niliwaza
kimoyo moyo
Kama vile bibi huyo aliyasoma mawazo
yangu aliangua kicheko kisha akanitazama, na mimi nikajifanya nacheka uongo
"Sasa kazi utaiweza tu.Usiwe na
wasi wasi na wala usiwe na haraka.Tunakwenda hatua kwa hatua. Hata mke wako
tulitoka naye mbali" bibi akaniambia baada ya kunitazama
Sikumjibu kitu. Moyo wangu ulikuwa
umesha fadhaika
"Subirini ninywe uji twende
chumbani"
SASA ENDELEA
"Tutakusubiri, kunywa tu
bibi.Sisi hatuna haraka" Chausiku akamwaambia bibi bila kujua jinsi
nilivyowachukia yeye na bibi yake
Baada ya bibi kumaliza kunywa uji
Chausiku alichukua kijungu na kifuu na kuvipeleka uani.Bibi mwenyewe alichukua
bakuli lake la mafuta na kuingia nalo chumbani mwake.Nikabaki peke yangu pale
ukumbini.
Baada ya muda kidogo mke wangu
akarudi.
"Bibi ameingia chumbani?"
akaniuliza
Nikamjibu kwa kichwa.Mdomo wangu
ulikuwa mzito kwa fadhaa
Chausiku naye akaingia mle chumbani.
Pakapita ukimya wa kama nusu saa. Baada ya muda huo bibi akaniita mle chumbani.
Nikanyanyuka na kuingia
Chumba hakikuwa na mwanga wa
kutosha.Kilijaa makorokoro na kilikuwa na harufu mbaya.Na ni lazima kiwe na
harufu isiyo ya kawaida kwani vitu vilivyokuwa humo ndani kama vile nyama za
maiti,mafuta ya miili ya binaadamu waliokufa, havikuwa vya kawaida.
Nilipoingia humo chumbani nilishituka sana. Bibi aliyeniita sikumuona.Nilimuona Chausiku amekaa kwenye kitanda cha bibi huku jipaka jeusi limesimama juu ya meza likiwa limenitolea macho.
"Bibi yuko wapi?' nikamuuliza
Chausiku
Yule paka akatoa sauti lakini
ilikuwa na maneno yaliosema "Niko hapaaa!"
Kwa kweli ingawa nilitaka mwenyewe
kuujua uchawi huo wa kugeuka paka lakini ilinishitua
"Sema unataka niniiii?"
lile paka aliendelea kulia huku akinitazama
"Jibu sasa!" mke wangu
akaniambia aliponiona nababaika
"Sitaki kitu" nikajibu kwa
sauti ya kitetemeshi
"Ebo hutaki kitu maana yake
nini? uliniambia nini jana kule shamba?"
"Sijakuambia kitu"
Chausiku akamtazama yule paka na
kumuambia "Anataka na yeye aweze kujigeuza paka kama wewe"
"Atakuwa pakaaa......leta zile
dawa zangu!" paka akamwaambia Chausiku
Chausiku alinyanyuka kwenye kitanda
akainama kwenye mvungu wa kitanda na kutoa pembe tatu ambazo sikuweza kujua
zilikuwa za wanyama gani.Zilikuwa zimefungwa fungwa kitambaa cheusi.
"Mimina dawa kwenye kiganja
chake" paka akasema
"Nyoosha mkono wako" Chausiku
akaniambia
"Lakini mimi sijasema kuwa
nataka nigeuke paka" nikasema kwa hofu.
"Nyoosha mikono!" Chausiku
hakutaka kunisikiliza
Nikanyoosha
Chausiku akamimina unga unga mweusi
kwenye kiganja changu.Unga unga huo ulitoka kwenye zile pembe tatu.Baada ya
hapo akamwaambia yule paka "Tayari"
"Sasa lete hapa huo
mkonooo" ilikuwa sauti ya yule paka
Mke wangu akanisukuma hadi pale karibu na ile meza. Akakipeleka
kiganja changu kwenye mdomo wa yule paka. Paka huyo akaunguruma na kutoa
ulimi akairamba ile dawa na kuitosa mate yake.
"Sasa mpe arambee" paka akasema
Mke wangu akaniambia "Unaambiwa uirambe hii
dawa"
Nilishindwa kuiramba
"Unasita nini wee mwanaume! mbona mimi
ninaramba?"
Mke wangu akatoa ulimi na kuiramba kisha akameza
"Hebu ramba bwana!" akaniambia
"Usipo ramba utakufaa!" paka akaniambia.
"Wewe ulikubali kutii kila kitu"
"Unasikia unavyoambiwa?" mke wangu akaniuliza.
Mkono wangu ulianza kutetemeka.Chausiku akaukunja na kuusogeza kwenye mdomo
wangu
"Hebu ramba!" akaniambia
Nikatoa ulimi na kuiramba kidogo
"Ramba mpaka uimalize"
Nikatoa tena ulimi na kuiramba
"Ramba tena!"
Nikaramba tena hadi dawa ikaisha
"Ameshamaliza" Chausiku akamwaambia yule paka
"Sasa vueni nguo mcheze ngoma yangu" paka
akaunguruma
"Vua nguo" Chausiku akaniambia huku na yeye
akivua
Nilikuwa nimeduaa nikimuangalia Chausiku.Alimaliza kuvua
nguo na kubaki uchi wa mnyama.Alipoona sija vua akanivua yeye. Tukawa uchi
sote
"Sasa tucheze" akaniambia huku akinishika
mkono.Akaanza kucheza moja ya ngoma ambayo walinifundisha kule kiwanjani.
Nikajiona napandwa na mori wa kucheza.Tukacheza sana
Wakati tunacheza yule paka akaunguruma "Nuia
kugeuka paka kwa mdomo wako au kwenye moyo wako.Na pale unapotaka kuwa
mtu nuia tena kuwa mtu"
"Umesikia ulivyoambiwa" mke wangu akaniuliza
"Nimesikia" nikamjibu kwa sauti nzito
"Nuia sasa"
Nikanuia kimoyo moyo kutaka kuwa paka.Kabla sijamaliza
kunuia,nilishituka nilipoona tayari nimeshabadilika na kuwa paka wa rangi
mbili nyeusi na nyeupe
Mwili ulikuwa wa paka lakini akili yangu ilibaki kuwa ya
kibinaadamu.Hapo hapo nikamuona Chausiku naye amegeuka paka mweusi mwenye
bato jeupe kichwani
Yule paka aliyekuwa juu ya meza akashuka chini na
kutufuata
"Sasa umeshakuwa paka,usiku tutakwenda kuwanga"
paka huyo akaunguruma
Nikataka kumjibu lakini sauti yangu haikutoa maneno kama
ilivyokuwa yeye.Iliishia kuunguruma tu.
Lakini alinielewa nilichotaka kumuambia.Nilitaka
kumuambia
"Nimefurahi kujiona nimekuwa paka"
Akaniambia "Hutaweza kusema kama mimi lakini
nimekusikia.Unaonaje?"
"Nasikia furaha sana" nikaunguruma.Ingawa maneno
hayakutoka lakini alinielewa akanijibu.
"Hata mimi nasikia furaha sana.Kutoka hii leo ukitaka
kuwa paka utakuwa tu. Lakini usitokeze nje isipokuwa kwa usiku tu"
"Sawa" nikamjibu.Hata hivyo sauti yangu ilikuwa
ya kuunguruma tu.Sikuweza kusema
"Nitaweza kusema lini?" nikauliza kwa kuunguruma
"Bado kwanza,mpaka tukukate kilimi"
Tukasikia mlango wa mbele ukibishwa hodi.Sote tukashituka
na kutega masikio.
No comments:
Post a Comment