Tuesday, October 31, 2017

RIWAYA, KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI SEHEMU YA 11

RIWAYA

KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI 11

ILIPOISHIA

Wengine walikuwa wakisema.

“Nahodha utatuua wewe, kuna watoto humu!”

“Alikuwa akivuta bangi, huyo hana akili!” Mwanamke mmoja alisema kwa hasira.

Pamoja na kelele zote hizo nahodha huyo hakumsikiliza mtu yeyote, aliendelea kukielekeza chombo hicho kwenye mawimbi. Ile dharuba iliyokuwa ikitupiga haikumtia hofu hata chembe.

Pale ndipo nilipogundua sababu ya baadhi ya manahodha kuvuta bangi, ni kutaka kupata uwezo wa kiakili wa kukabiliana na ile hali endapo itatokea.

Yule mtu alionekana kama mwehu. Wimbi linapokuja linatutosa. Na yeye alitota chapa chapa lakini hakuonesha kupata hofu wala kujali. Siku ile niliapa kuwa sitasafiri tena na jahazi na sikujua kama tungefika salama Pemba.

Yale mawazo ya kufa yakanifanya nimkumbuke mke wangu. Nikakumbuka kwamba nilimuahidi kumtumia nauli na nikahisi kwamba angenipigia simu kuniulizia tena.

Nikatoa simu yangu na kuizima ili akipiga simu asinipate.

SASA ENDELEA

Upande mmoja wa akili yangu ukaniambia kuwa hatua hiyo ingeweza kumzidishia wasiwasi mke wangu, jambo ambalo linaweza kufanya aamue kukopa pesa ya nauli ili aje anifumanie.

Kama atafanya hivyo, nilijiambia, akifika Korogwe hatanikuta na hivyo atawapa nafasi wale majini wamtoe kafara.

Kile nilichokuwa sikitaki ndicho kitakachotokea, nilijiambia.

Nikakumbuka pia nilikuwa nimewaacha na njaa wale viumbe kule kwenye pango na nikapata hofu kuwa wanaweza kufa.

Ilimradi nilijikuta nimesongwa na mawazo mengi lakini niliomba Mungu tufike salama ili nijue nitafanikiwaje kulitatua lile tatizo lililokuwa linanikabili.

Mungu si Athumani wala si Huseni. Pamoja na dharuba zilizotupiga baharini tulifika salama Pemba. Tatizo ni kuwa tulifika usiku.

Ikanibidi nitafute gesti. Mji huo haukuwa na gesti nyingi kama ilivyo huku bara. Hata hivyo nilifanikiwa kupata gesti moja katikati ya mji wa Chakechake Pemba. Nikalala hapo hadi asubuhi.

Kulipokucha ndipo nilipoulizia kwa wenyweji kilipo hicho Kisima cha Giningi.

“Kipo Kendwa” Kijana aliyenipokea pale gesti ndiye aliyenijibu. Kabla sijamuuliza huko Kendwa ni wapi akaendelea kuniuliza.

“Unataka kwenda Giningi?”

“Ndiyo nataka niende nikapaone”

“Wewe unataka ufike katika hicho kijiji au hapo kwenye kisima?”

“Nataka nifike hapo kwenye kisima”

“Magari yapo yanayokwenda huko”

“Nitayapata wapi?”

Kwa msaada wa yule kijana aliyegundua kuwa nilikuwa mgeni ninayetoka bara nikafanikiwa kupata daladala iliyonipeleka katika kijiji hicho kilichokuwa maeneo ya mashambani.

Nilipofika nilipata kijana mwingine aliyenichukua kwa baskeli ya bodaboda hadi kilipokuwa kisima hicho cha Giningi.

Kinapotajwa Kisima cha Giningi mtu angeweza kudhani kuwa kilikuwa kisima cha kisasa na kilichokuwa katika mazingira ya kupendeza. Lakini hakikuwa hivyo. Kisima chenyewe kilikuwa ni cha kale sana na kilionekana kama hakikuwa kikitumika tena.

Kwa mujibu wa mzee mmoja niliyemkuta hapo, kisima hicho ni cha kale sana na haikufahamika kilichimbwa katika enzi ipi. Lakini kilipata umaarufu kutokana na baadhi ya wenyeweji kuamini kuwa mahali hapo palikuwa na asili ya kimizimu na majini. Hivyo watu mbalimbali walikuwa wakifika mahali hapo kufanya matambiko na mambo mengine ya kiuganga.

Nilimsikiliza kwa makini yule mzee kabla ya kujitambulisha kwake na kumueleza kuwa nimetoka bara na nilikuwa na shida na mzee aliyekuwa anaitwa Habib Sultani.

“Ulikuwa unamtaka wa nini?” Mzee huyo akaniuliza.

“Nina shida naye”

“Shida gani?”

“Nilisikia huyo mzee anashughulika kuwapa watu majini ya kuwatajirisha”

“Ni kweli. Kwa hiyo wewe ulikuwa unataka upate utajiri?”

“Hapana. Nina tatizo jingine”

“Nataka nikufahamishe kuwa huyo mzee uliyemtaja ameshakufa”

Nikashituka na kumuuliza.

“Alikufa lini?”

“Ni muda sasa. Inafika miaka mitatu”

Nikatikisa kichwa changu kusikitika. Nikaona safari yangu ya kwenda Pemba ilikuwa ya bure.

“Ungenieleza mimi shida yako labda ningekusaidia”

“Kwani wewe pia unahusika na mahali hapa?”

“Mimi ndiye muangalizi wa eneo hili. Mimi ndiye ninayefagia hapa kila siku na kusaidia watu shida mbalimbali”

“Huyo Habib Sultani alikuwa ni nani?”

“Yeye alikuwa mganga na ndiye aliyeachiwa siri ya mahali hapa na babu yake”

“Sasa sijui utanisaidiaje mzee wangu…”?

“Niambie tu shida yako wala usihofu”

Nikamueleza yule mzee matatizo yangu mwanzo hadi mwisho.

Yule mzee hakushituka hata kidogo isipokuwa aliinama akafikiri kwa muda kidogo kabla ya kuniuliza.

“Una maana kuwa marehemu baba yako kabla ya kufa kwake hakuwa amekuarifu kuwa alikuwa na jini kutoka hapa Giningi linalompatia pesa?’

“Hakuniarifu. Nilizikuta zile pesa baada ya yeye kufa na yule jini alinifuata usiku akanifahamisha kuwa alinunuliwa na baba yangu kutoka hapa na akataka mimi nimrithi”

“Na wewe hukutaka?”

“ Sikutaka na sitaki!”

“Yule mke wake na yule mwanao waliotolewa kafara bado wapo?”

“Wale bado wapo hai lakini wakati wowote wanaweza kufa. Isitoshe nimeambiwa akifa mama, mke wangu naye atachukuliwa. Ndiyo maana nimeharakisha kuja huku”

“Tangu nianze kuwa msimamizi wa kisima hiki leo ndio mara ya kwanza kuona mtu anakataa pesa za majini ambazo watu wengi wamekuwa wakizitafuta”

“Mimi ni mtu tofauti sana, Najali utu wa watu, sijali pesa. Bora nife masikini kuliko kuwatoa muhanga binaadamu wenzangu”

“Basi usiseme maneno mengi, nataka nikuulize swali moja umeshatumia kiasi gani katika hizo pesa?”

“Sijatumia hata senti tano”

“Sasa mwanangu, mimi ni muangalizi tu wa eneo hili. Mimi sina uwezo wa kumpa mtu jini wala kumtoa jini na sijui kama jambo hilo unalolitaka linawezekana…”

“Mzee uliniahidi kuwa utanisaidia” nikamkatiza yule mzee.

“Msaada wangu utaupata. Nitakupeleka kwa mwana wa huyo Habib Sultani ambaye ameachiwa mikoba na huyo baba yake. Sasa msaada zaidi utaupata kwa huyo”

“Sawa, basi nipeleke kwa huyo aliyeachiwa hiyo mikoba”

“Lakini kuna mawili, anaweza akusaidie au asikusaidie”

“Mimi ninachotaka wachukue pesa zao pamoja na yule jini wao”

“Kwa sababu yeye siye aliyemtoa huyo jini, sina uhakika kuwa ataweza kulifanya jambo hilo lakini twende ukamsikilize mwenyewe’

Yule mzee akanipeleka katika nyumba moja iliyokuwa katika kitongoji kile kile cha Kendwa.

Tulimkuta mtu mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kiti cha uvivu akivuta tasbihi. Alikuwa amevaa kanzu nyeupe na kichwani alijifunga kilemba kikubwa.

“Maalim asalaam alaykum” Yule mzee akamsalimia. Na mimi pia  nikamsalimia.

“Waalaykum salaam” Mtu huyo akatujibu.

“Tumepata mgeni kutoka bara. Alikuwa na shida na marehemu Habib Sultani. Nimemwambia Sheikh Habib allishafariki kitambo lakini yuko mwanawe”

Yule mtu akanitazama na kuniambia.

“Karibu mgeni?”

“Huyo ndiye mwanawe  marehemu Shikh Habib Sultani na yeye pia anaitwa Sultani. Unaweza kumueleza shida yako” Yule mzee akaniambia.

Tangu nilipomuona mtu huyo sikutarajia kuwa angekuwa  ndiye huyo mwana wa Habib Sultani. Kwa vile niliambiwa ni mwana, nilitarajia kumuona kijana mdogo. lakini yeye hakuwa kijana mdogo. Alikuwa mtu mzima na kiumri alikuwa amenizidi hata mimi.

“Mtolee kiti” Mtu huyo akamwambia yule mzee niliyekwenda naye.

Yule mzee akaingia ndani ya ile nyumba na kutoka  na kiti akaniwekea na kuniambia.

“Karibu ukae”

Nikakaa mbele ya yule maalim.

“Haya nieleze shida yako”

Nikaanza kumueleza mtu huyo matatizo yangu mwanzo mpaka mwisho.

“Nadhani kulikuwa na makosa yalifanyika kati ya marehemu Habib na baba yako” akaniambia.

“Makosa gani?”

“Huyo jini alimuhusu baba yako tu na hizo pesa zilimuhusu baba yako tu. Lakini bila shaka baba yako alikutaja wewe kama mrithi wake na ndio maana huyo jini alikufuata. Sasa kwa bahati mbaya mzee Habib ameshakufa”

“Nimeambiwa kuwa wewe ndiye mrithi wake. Nilitarajia kuwa ungeweza kunisaidia”

“Kwani usichotaka wewe ni kitu gani, ni pesa au jini?” akaniuliza.

“Silitaki hilo jini?”

“Na pesa je?”

Je nini kitatokea? Tukutane kesho

1 comment:

  1. PESA ZA MAJINI PIA NDAGU YA MALI KWA (MASHARTI) NDANI YA MASAA 72(SIKU TATU) PAPO HAPO KIKUBWA UWE MWAMINIFU, JASILI NA UWE NA UTAYARI WA KUPOKEA MASHARTI YA KUTUNZA SIRI HII SIO MZAHA......

    (HUSITUME SMS PIGA SIMU KUHEPUKA MATAPELI)

    PUUZA UONGOFU WA KUWA MTU KUWA TAJIRI NI DHAMBI WAKATI AKUAMBIAE YEYE NI TAJIRI (Tumia ufahamu kujinasuaUTAJIRI WA

    NAITWA DR, MDIRO piga 0742162843. KAMA UNAITAJI PESA ZA MAJINI AU NDAGU YA MALI AU ULINZI KWA MALI YAKO

    MATIBABU MENGINEYO NI KAMA UTULIVU KATIKA NDOA, AU KUMVUTA UMPENDAE, KUONDOA MIKOSI, MABALAA, KUOSHA NYOTA, KUITAMBUA NYOTA YAKO NA ASILI YA KAZI YAKE.
    JINI MAHABA NA SHIDA YA UZAZI. NIPIGIE 0742162843. KIKUBWA NI KUSIKILIZA NA KUFATA MASHARTI. ANGALIZO USITUME SMS PIGA NA UWE NA NIA.

    (kuhusu utajiri au pesa) KABLA YA KUPIGA SIMU ZINGATIA YAFUATAYO
    1. uwe una umri wa miaka 18+
    2. uwe tayari kupokea masharti yote
    3.uwe na uwezo wa kutunza siri
    4. uwe jasiri wa kupokea taarifa yoyote
    KARIBU SANA KWA SHIDA NYINGINE PIA ULIYONAYO AMBAYO SIJATAJA INSHAALAH ITATATULIWA IKIWA NDANI YA UWEZO WANGU.

    ReplyDelete