Saturday, May 7, 2016

HADITHI SEHEMU YA 12

HADITHI na Faki A Faki 0655 340572
Ilipoishia jana mume wa Chausiku baada ya kuona viroja kwa bibi kikongwe na kuruni nyumbani na kumueleza Chausiki visa vya bibi huyo huku Chausiku akicheka kana kwamba anajua kila kitu kilimshangaza mume wa Chausiku
Sasa Endelea
 
"Leo sijisikii vizuri" nikamwambia mke wangu.
 
"Hakuna. Usikwepe! Unatakiwa ukamilishe siku saba ndipo utaweza kutoa dharura ya kutokwenda”
 
Nikatikisa kichwa.
 
"Leo siendi. Bibi akikuuliza mwambie naumwa"
 
"Atajua umemdanganya"
 
"Kama sijisikii vizuri niende tu?"
 
"Mbona mimi nakuona ni mzima?"
 
"Ninayeumwa ni mimi, wewe huwezi kujua. Na pia nimeshakuona kuwa huna huruma na mimi"
 
"Sina huruma na wewe kwa sababu gani?"
 
"Basi tuyaache"
 
Nikajifanya nimekasirika ili mke wangu akubaliane na mimi.
 
"Kama unaumwa kweli lala. Mimi nilikwambia tu" Chausiku akaniambia aliponiona nimekasirika.
 
Usingizi ulipokuja kunichukua nililala moja kwa moja. Hata mke wangu alivyotoka usiku sikujua na wala yeye hakuniamsha kuniambia.Nilikuja kushituka usiku mwingi nikaona Chausiku hayupo kitandani. Nikajua ameshatoka. Mimi nikaendelea kulala.
 
Baada ya muda kidogo nilishitushwa na kelele zilizokuwa zikisikika nje ya dirisha la chumba changu. Nikatega masikio na kusikiliza. Nikagundua kuwa zilikuwa  kelele za lile kundi letu la wachawi. Kuna baadhi ya wachawi akiwemo mke wangu na yule bibi, waliamua kunifuata.
 
Kelele zao zilikuwa haziwezi kusikiwa na watu wengine katika ile nyumba zaidi yangu mimi kwa vile nilikuwa mchawi mwenzao.
 
Niliwasikia wakiimba nje ya dirisha langu na yule bibi kikongwe alipaza sauti yake kuniita.
 
"Toka! Toka! Tumekufuata wewe twende kazini, saa imefika"
 
Niliposikia sauti ya yule bibi nilijiuliza, Chausiku alikwenda kuwaeleza nini mpaka wakaamua kunifuata. Muda ule ule nikamuona mke wangu na mwanamke mmoja wameniibukia mle chumbani wakiwa uchi. Hawakupita kwenye mlango. Niliwashitukia tu wakiwa kando ya kitanda changu.
 
Mke wangu akanishika mkono na kuniondoa pale kitandani.
 
"Unaitwa na bibi. Amka"
 
"Si nilikuwa ninakuja?" nikajisemea kwa hofu.
 
Kwa vile sikuwa na nguo nilitafuta shuka nikajifunga kiunoni ili yule mwanamke mwingine asinione. Kama ni kuonana tuonane huko huko uchawini kwetu. Wakati nimemaliza kujifunga shuka mke wangu alinishika mkono mmoja, mwenzake akanishika mkono mwingine. Mara ile ile nikajikuta tumetoka nje ya chumba kwa kutumia uwazi mdogo uliokuwa kwenye dirisha.
 
Ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuona muujiza ule. Nilijikuta nimesimama mbele ya yule bibi.
 
"Leo tunakwenda na wewe kwa yule binti wa mwarabu tukamchawie"  Bibi huyo akaniambia.
 
Nikajua ataniuliza kwanini sikutoka ili nimjibu kuwa sijisikii vizuri. Lakini hakuniuliza na hivyo sikuweza kumweleza kitu.
 
Ghafla mmoja wa wanawake waliofika hapo akaja mbele yangu na kunipaka dawa kwenye uso wangu. Mwingine akanivua ile shuka na kunipachika mkia kwenye kiuno. Mke wangu naye alichukua ile shuka  akaipachika kwenye ukuta wa nyumba.
 
"Tutaikuta hapa hapa" akajisemea peke yake.
 
Baada ya hapo yule bibi akatuamuru tuondoke, tulikuwa wachawi saba. Mwanaume nilikuwa mimi peke yangu. Bila shaka kulikuwa na kundi jingine la wachawi lililokwenda mahali kwengine.
 
 Tulikuwa tunaenda kwa miguu, nikaona tumekifikia kijiji cha Songe baada ya kupiga hatua chache tu. Kijiji hicho kilikuwa umbali wa karibu kilometa tano kutoka kijiji kile tulichokuwa tunaishi.
 
Hapo nikagundua kituko cha tatu cha uchawi. Cha kwanza kilikuwa kile cha mke wangu na mwenzake kujipenyeza chumbani nilimokuwa nimelala. Na cha pili ni jinsi walivyonitoa kupitia kwenye uwazi uliokuwa kwenye dirisha na cha tatu ni kile chakufika kijiji cha Songe kilichopo umbali wa kilometa tano kwa kupiga hatua chache tu.
 
Tulipokuwa tunatembea tulikuwa tunaonekana na kisha tunapotea machoni mwa mtu yeyote aliyebahatika kutuona.Tukafika katika ile nyumba tuliyokuwa tumeikusudia. Ilikuwa nyumba nzuri ya tofali iliyokuwa na mlango wa duka na ilikuwa inawaka taa ya umeme.
 
Pengine ile kuonekana ni nyumba nzuri yenye umeme ndicho kilichosababisha iandamwe na wachawi. Pia niliambiwa waarabu wenyewe walikuwa watu wenye uwezo kifedha, hali ambayo haikuweko kwa baadhi ya wanavijiji wa kijiji hicho.
 
Kwa hiyo uwezo wa waraabu hao ulikuwa ukiwakera baadhi ya wanavijiji akiwemo yule bibi kikongwe. Nilikuwa nimejifunza kwamba uchawi ulikuwa umeandamana na moyo wa uhusuda, yaani kuona gere maendeleo ya wengine na hivyo kutaka kuyaharibu.
 
Tulipofika barazani mwa nyumba huyo yule bibi alipiga pindu kwenye usawa wa mlango kisha akachutama na kumwaga kinyesi chake mbele ya mlango. Hapo hapo niliona ile taa iliyokuwa ikiwaka barazani ikizimika yenyewe na kuwa kiza.
 
Taa ilipozimika nilishuhudia vituko ambavyo sijawahi kuviona maishani mwangu. Mke wangu pamoja na wale wachawi wengine walikuwa wamecharukwa kucheza ngoma za ajabu ajabu wakionekana kama waliopagawa. Kama angetokea mtu na kutuona angekimbia.
 
Wakati wakicheza ile ngoma walikuwa wakifanya kama wanaitia misukuo ile nyumba. Wengine walisotea kwenye kuta na wengine waliing'ong'a. Sijawahi kuona ngoma kama ile hata siku moja.  Baada ya miujiza ile, bibi alitupeleka kwenye dirisha mojawapo la ile nyumba kisha akamwaambia Chausiku.
 
"Nitaingia mimi kisha utaingia wewe na mumeo"
 
Alipomwambia hivyo alinyoosha kidole kuelekea kwenye upenyo wa dirisha na mara ile ile akatoweka. Mke wangu akanishika mkono. Akanyoosha kidole chake kuelekea kwenye upenyo ule ule uliokuwa kwenye dirisha. Mara ile ile tukajikuta tumo ndani tukiwa tumeshikana mikono vilevile.
 
Tulitokea kando ya dirisha ndani ya chumba kidogo kilichokuwa na kitanda na kabati.Taa ilikuwa inawaka. Nikamuona msichana wa kiarabu aliyekuwa amelala usingizi kitandani. Bibi kikongwe alikuwa amemuinamia kitandani akimsemea maneno ya kichawi. Na sisi tukasogea pale penye kitanda.
 
Yule bibi alimkata sehemu ya nywele zake kwa kutumia kucha zake na kumuacha akiwa na vipachu kichwani. Kwa kutumia kucha zake hizo hizo aliendelea kumchanja kwenye kifua kisha akamgeuza na kumchanja kwenye mgongo.
 
Alipomaliza kumchanja, yule msichana alinyanyuka mwenyewe akiwa katika hali ya usingizi na kusimama mbele ya yule bibi.
 
"Wewe punda wangu inama unipakie twende!" Bibi akamwambia msichana huyo ambaye aliinama. Yule bibi akampandia mgongoni.
Usikose hadithi hii ya kusisimua kesho ni kitatokea nyumbani kwa Mwarabu je, wachawi hao pamoja na mume wa Chausiku watafanikiwa lengo lao
 
 

No comments:

Post a Comment