HADITHI
SIMULIZI ZA FAKI A FAKI 0713 340572 , 0555 340572
SITASAHAU NILIVYOGEUZWA PAKA 13
ILIPOISHIA
Siku ile bibi alinipanga mimi na
wanawake wawili twende nyumbani kwa mwalimu mkuu wa ile shule anakouzia mbaazi
zake tukamchawie kwa sababu alimwambia yule bibi atamfukuza asipeleke tena
biashara yake kwa vile wanafunzi na walimu wanaokula mbaazi zake wanaharisha. Kauli
hiyo ilimuudhi yule bibi.
Mke wangu na wenzake wengine walitumwa
sehemu zingine.
Nyumbani kwa mwalimu mkuu hakukua
mbali sana na pale kwenye kiwanja chetu.Tukaenda.
Kama kawaida tulipofika wachawi
wenzangu wakapiga pindu kwenye mlango wa nyumba ya mwalimu mkuu
huyo.Wakaniambia na mimi nipige pindu nikapiga pindu.Kisha tukazunguuka duara
na kuanza kucheza ngoma ya kichawi barazani mwa ile nyumba.Zile pindu
tulizopiga zilikuwa na malengo ya kufanikisha ile kazi ya kichawi iliyotupeleka
hapo. Na ile ngoma ilikuwa ni ya kuwalaza usingizi watu wote waliokuwemo mle
ndani.
Tulipomaliza ikafuatia kazi ya
kujipenyeza kiuchawi ndani ya ile nyumba. Laiti ningejua ni kitu gani
kitatutokea humo ndani,mimi nisingekubali kuingia humo.
SASA ENDELEA
Alianza kujipenyeza mwanamke wa
kwanza kupitia kwenye upenyo wa dirisha.Mwanamke wa pili akanishika
mkono,nikapenya naye.Sote watatu tukawa ndani ya chumba kilichokuwa kiza. Mwanamke
aliyeingia kwanza alifyatua swichi,chumba kikajaa mwanga.Kwenye kitanda tukaona
watu wawili wakiwa wamelala.Walikuwa mwanaume na mwanamke.Mwanamke alilala
kichalichali na mwanaume alilala kifudifudi.
Yule mwanaume alikuwa ndiye mwalimu
mkuu wa shule ya msingi ya pale kijijini na mwanamke aliyekuwa naye alikuwa mke
wake.
Tulianza kuwachezea ngoma tukiwa
tumesimama kando ya kitanda walicholala.Baada ya mchezo huo mwanamke mmoja
aliwafunua shuka akaanza kumkatakata nywele yule mwanamke.Alimkata nywele
nyingi upande mmoja wa kichwa chake kwa kutumia kucha zake.
Mwanamke wa pili naye alipanda
kwenye kitanda na kumkalia mwalimu mkuu mgongoni. Alichokuwa anakifanya hapo ni
kumminya na kumuumiza mwalimu huyo mpaka akawa anaweweseka na kutoa sauti ya
kusikia maumivu.
Mbali ya kumshindilia kwenye kiuno
na mgongo aliipindisha mikono yake kama aliyetaka kuivunja akawa anarudia
kufanya hivyo mara nyingi.Baadaye aligeukia kwenye miguu,nayo akawa
anaipindisha.Mwalimu mkuu alikuwa akiendelea kuweweseka kwa maumivu.
Mwanamke huyo alipotosheka na mchezo
huo alishuka kwenye kitanda,akamchanja chale mwalimu huyo mgongoni kwa kutumia
kucha.Alimchanja sehemu tofautitofauti kisha akasema "Sasa tuwaache
twende zetu"
Mwanamke huyo akanishika mkono na
kulielekea dirisha.Alilinyooshea kidole ili tupenye katika dirisha hilo lakini
hatukuweza kuondoka mahali tulipokuwa tumesimama.
Mwanamke alijaribu tena lakini
hakuweza kuondoka, tena mwenzangu ndiyo alinata kabisa.Nikamuachia mkono na
kushikana na yule mwanamke mwingine.Na yeye nikamuona alikuwa kama
amelewa.Sikuweza kujipenyeza naye kwenye dirisha hilo.Wenzangu wote wawili sasa
walionekana kama mazezeta.Uwezo wa kutoka mle chumbani walikuwa hawana.Kila
mmoja akabaki amesimama hapohapo.
"Jamani mbona hatuendi?"
nikawauliza kwa hofu
"Siwezi kutoka!" mwanamke
wa kwanza akanijibu
"Na mimi pia nashindwa"
mwanamke wa pili naye akaniambia.
"Sasa tufanyeje?'
"Kuna zindiko humu ndani.Nenda
ukaliondoe" mwanamke aliyekwama kwanza akaniambia.
"Zindiko!"
nikang'aka "Hilo zindiko liko wapi?"
"Litafute"
"Sitaweza. Sina utaalamu huo"
"Basi hatutaweza kutoka!"
"Sasa itakuwaje?" nikawauliza
wanawake hao kwa hofu lakini hakukuwa na aliyenijibu.
"Basi tutoke kwa kutumia
milango" nikawaambia
"Hatuwezi kuondoka kabisa,mpaka
lile zindiko liondoke!"
Nikajaribu kwenda kwenye
mlango.Nikaona ninaweza kutembea.Nikaufungua mlango.
"Njooni twende
jamani.Tutakutwa!"
"Njoo utuondoe.Hatuwezi
kuondoka"mwanamke mmoja akanimbia
"Kwanini,mbona mimi
ninaweza?"
Hakukuwa na aliyenijibu.
Nikaenda na kumshika mkono mwanamke
wa kwanza ili nimvute lakini alikuwa amenasa kama aliyeshikwa na umeme,hali
ambayo ilinishitua. Sikutaka hata kumshika yule mwanamke mwingine kwa kujua
hali itakuwa ileile. Nikakimbilia kwenye mlango.Nikaufungua na kutoka.Ukumbini
palikuwa giza.Lakini nilijua mlango wa mbele ulikuwa upande wa kulia.Nikaelekea
upande wa kulia.Kwa sababu nilikuwa sioni kutokana na giza Nilikumba ndoo ya
maji ikaanguka,maji yakamwagika chini.
Nikasikia sauti kutoka chumba
kingine ikauliza
"Wewe nani?'"
Sikujibu kitu, nikaamua kukimbia.
Sikufika mbali nikateleza kutokana
na yale maji yaliyomwagika.Nikapiga mweleka kwa kishindo.
"Wewe nani uliye hapo
ukumbini?'' ile sauti ikauliza tena
Nikanyanyuka haraka na kupapasa
ukuta, nikawa naenda huku nimeshikilia ukuta.Mbele tena nikakumbana na
meza.Niliikumba ikatoa mlio wa kuburuzika.
"Wewe nani? mbona ukiulizwa
husemi?"
Sasa ilikuwa sauti ya mwanamke
iliyotoka chumba kingine.
Nilikuwa nikitetemeka kwa hofu
nikijua kuwa arobaini zangu zilikuwa zimekaribia.
Niliipita ile meza nikakumba ndoo
nyingine lakini hii ilikuwa tupu. Nikaendelea kwenda sasa kwa harakaharaka ili
nifike kwenye mlango.
"Baba Rama, hebu amka. Naona
kumeingia mtu hapo ukumbini!" ile sauti ya kike ikasikika tena.
Mara nikasikia sauti ya mwanaume
ikiuliza "Unasemaje?"
"Hebu amka.Kuna mtu ameingia
ukumbini. Kuna vitu vyetu visije vikaibiwa!"
"Unasema kumeingia mtu?'
"Ndiyo, yupo ukumbini. Anakumba
ndoo, akiulizwa wewe nani hasemi"
Sauti hizo ziliingia moyoni mwangu
kwa ukali kama mmweko wa radi.Nilijua sasa maisha yangu yalikuwa yamekwisha.
Niliufikia mlango lakini kufika
kwenye mlango hakukutosha. Mlango ulikuwa umefungwa na sikujua
umefungwaje.Nikawa naupapasapapasa kutafuta vifungulio.Moyo ulikuwa ukinienda
mbio kama uliotaka kutoka na nilikuwa nikihema kwa nguvu kama mwizi aliyekuwa
anafukuzwa.Sekunde zilikuwa zinapita.Nikahisi watu watatoka vyumbani mwao
na kunikuta pale kwenye ule mlango.
Akili yangu ilikuwa imeshataharuki
na sikuwa na maarifa zaidi ya kutumia nguvu.Nikaukumba ule mlango lakini
haukufunguka isipokuwa ulitoa kishindo kikubwa.Nikaukumba kwa mara ya
pili
"Kweli kuna mwizi!"
nikasikia ile sauti ya kiume ikinong'ona na kisha ikauliza " Lile
panga langu liko wapi?"
Moyo ukanishituka.Nilikaribia
kuzirai kwa hofu.Akili yangu iliunda picha ya mwizi anayefukuzwa na kuzingirwa
na watu ambao wanamtandika mawe na marungu na kumsaga kabisa.
Nilijiambia,wakati wowote kutoka
muda ule picha niliyoiwaza itanitokea kama sitatuliza akili yangu na kuweza
kufungua ule mlango.
Wakati nikijiambia hivyo mkono wangu
ulikishika kifungulio cha mlango kilichokuwa juu,nikakifungua.Nikajua milango
mingi inakuwa na vifungio vitatu.Kama kuna cha juu kutakuwa na cha
katikati na cha chini.Sikukosea,nilipopapasa nilikipata kifunguo cha
katikati.Nikakifungua kisha nikaujaribu mlango.Mlango ulikuwa bado
haufunguki.Nikainama na kupapasa sehemu ya chini ya mlango. Vile ninainama tu
nikaisikia sauti ya mwalimu mkuu na mke wake wakipiga makelele.
"Jamani tumeingiliwa na watu
chumbani,wako uchi.Njooni njooni jamani!" ilikuwa suti ya mke wa mwalimu
mkuu.
"Nyinyi ni akina nani?"
sauti ya mwalimu mkuu nayo ilisikika ikiuliza
"Nawauliza nyinyi ni akina
nani?" sauti ya mwalimu mkuu huyo iliendelea kusikika wakati mke wake
aliendelea kupiga kelele
Sasa hali haikuwa nzuri hata
chembe.Wenzangu wameshaonekana na walikuwa wamenasa,bado mimi.Tumbo lilikuwa
likiniunguruma.Vile nilivyoinama kama nisinge ikaza, haja kubwa ingenitoka
palepale.
No comments:
Post a Comment