Thursday, December 11, 2014

GAMBO ATOA AGIZO KWA WATENDAJI WA SERIKALI KUSAJILI KAYA 200 KILA MMOJA

Kumekucha blog

Korogwe, MKUU wa Wilaya ya Korogwe, Mrisho Gambo, amewataka wenyeviti   wa mitaa na vitongoji Wilayani humo ifikapo Julay mwakani kuhakikisha kila kijiji inasajili kaya 200 kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF).

Agizo hilo amelitoa jana wakati akifungua kituo cha zahanati kijiji cha Kalalani kata ya Kigwase Wilayani Korogwe kilichojengwa kwa msaada wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kusema kuwa kiongozi yoyote ambaye atashindwa kufanya hivyo  atawajibishwa.

Alisema agizo hilo limekuja baada ya kuonekana  wananchi wengi wanashindwa kumudu gharama za matibabu kufuatia  kupanda kwa maisha  hivyo kuwataka kutoa elimu ya nyumba kwa nyumba na kusajili wanachama ambao watapata  matibabu bure mwaka mzima kwa kuchangia shilingi elfu tano.

“Natoa agizo viongozi wote wa kijiji, mtaa na kitongoji kusajili kaya mia mbili kujiunga na mfuko wa bima ya afya---na ifikapo mwezi wa saba mwakani ambaye hajakamilisha kufanya hivyo bora aachie ngazi” alisema Gambo

“Wananchi hawana uelewa wa mifuko ya bima ya afya hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha munatoa elimu ya nyumba kwa nyumba ili kila mmoja atambue umuhimu wa mfuko huo na kuchangia kiasi kidogo cha pesa na kupata matibabu bure mwaka mzima” alisema

Mkuu huyo wa Wilaya aliwataka wajawazito vipindi vya kujifungua kwenda katika vituo vya zahanati na kuepuka kujifungulia katika sehemu ambazo sio salama ili kuepusha matatizo wakati wa kujifungua.

Alisema wajawazito wengi wamekuwa wakipata matatizo yakiwemo kupoteza damu nyingi na uhai wa mtoto  kwa kwenda sehemu ambazo sio salama na hivyo kuwataka vipindi vya ujauzito kuhudhuria vituo vya afya.

Awali akisoma risala fupi mbele ya mgeni rasmi, Mrisho Gambo,Meneja Ujirani Mwema Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Ahmed Mbugi,alisema  mradi huo hadi kukamilika kwake umetumia zaidi ya shilingi milioni 97 ambapo mchango wa wananchi ni milioni 19.

Alisema hifadhi ya Taifa ya Mkomazi  kwa kuthamini ushirikiano wa wananchi na hifadhi hiyo na kuona kero ya kufuata matibabu zaidi ya kilometa 30 ikaona ni vyema kuwajengea kituo cha afya ikiwa ni moja ya sera za hifadhi hiyo.

“Sera ya hifadhi ya taifa kwa wananchi walioko kandokando ni kuwapatia huduma muhimu zakiwemo za elimu na afya----kwa muda mrefu tulikuwa tunaumiza vichwa ni jambo gani muhimu tulifanye kwa wakazi hawa” alisema Mbugi

“Tuliwaita viongozi wa Serikali ya kijiji na Wilaya na tukapeleka wazo la kutaka kujenga kituo cha afya hapa Kalalani na kwa kweli tuliungwa mkono na wananchi nao wakalipokea kwa mikono miwili” alisema

Aliwataka kukitunza kituo hicho na kuwa msaada kwa wakazi wa eneo hilo na jirani na kuwataka kuwa na mashirikiano kwa jambo lolote na kusema kuwa Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi itashirikiana nao kwa hali na mali.

Alisema kituo hicho kitakuwa mkombozi wa mama wajawazito na wazee  na kuondokana na kero ya kufuata matibabu kwa zaidi kilometa 30 jambo ambalo baadhi ya vipindi wajawazito walikuwa wakijifungulia njiani.

                                   Mwisho

No comments:

Post a Comment