Friday, December 12, 2014

HADITHI KISIWA HARISHI



HADITHI

KISIWA CHA HARISHI (9)

ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA

Mwenzetu aliishiwa na nguvu kabisa. Akawa amemkodolea macho Harishi.

“Mimi nasikia harufu zenu tangu jana”

Mwenzetu kimya. Sasa mwili wake ulikuwa ukitetemeka waziwazi.

“Sheikh nisamehe sana…” Sauti yake ikasikika kwa mbali ikiomba.

“Chombo chetu kiliharibika jana”

Harisha alikuwa akimtazama kama vile alikuwa hamuelewi.

“Wasemaje?”

“Nisamehe sana…nakuomba” jamaa alikuwa analia.

“Kwani wewe huna damu?. Ngoja nione”

Hapo hapo Harishi akamuinua juu mwenzetu huyo kwa mkono mmoja tu. Akamgeuza kichwa chini.

Kiasi cha kufumba na kufumbua tu alishamtoboa utosi kwa ncha ya upanga wake.

Yasmin alipoona hivyo alikimbilia nje. Akatuona tumeinamia dirisha.

“Jamani balaa gani hili?” akajisemea peke yake.

SASA ENDELEA

Idadi yetu sasa tulikuwa watu watano, wenzetu wawili walikuwa wameshauawa. Na sisi pia hatukuwa na matumaini kuwa tungebaki.

Tulijua kuwa kama hatutakufa kwa njaa, tutauliwa na lile jini la Yasmin. Kila mmoja wetu alikuwa ameshikwa na hofu na fadhaa. Tulitamani angalau kipite chombo kituokoe kuliko vile tulivyokuwa matumatu tukisubiri kufa.

Tulitamani tusifike tena katika lile jumba la Yasmin lakini tungekula nini, wakati kwa Yasmin ndiko tunakotarajia kupata riziki yetu. Kusema kweli tulichanganyikiwa na hatukujua la kufanya.

Tulikaa pale chini ya mti kwa karibu saa mbili. Ghafla tuliona mwanamke akiambaa na ufukwe wa bahari akija  upande wetu. Mkono mmoja alikuwa ameshika kapu.

“Jamani ni nani yule?” Mwenzetu mmoja akauliza.

“Naona ni kama Yasmin” nikajibu.

Mjadala ukaanza.

“Ni Yasmin kweli!”

“Amefuata nini huku?”

“Labda anatutafuta sisi”

“Mmoja wetu atokeze ili atuone au aende akampokee lile kapu. Labda anatuletea chakula”

“Hatujui Harishi yuko wapi. Unaweza kujitokeza ukajikuta unakamatwa!”

“Bila shaka Harishi ameshaondoka, Yasmin asingeweza kuja huku. Ngoja nimfuate” Mimi ndiye niliyesema hivyo. Nikanyanyuka na kuanza mwendo kuelekea upande ule aliotokea Yasmin.

Yasmin akaniona.

“Nawatafuta nyinyi, mko wapi?” akaniuliza tangu akiwa mbali.

“Tuko huku chini ya mti. Tumekuona tangu ukiwa mbali”

“Nimewaletea chakula”

Nilikuwa nimeshamfikia. Nikampokea lile kapu.

Tukawa tunatembea pamoja kuelekea kule waliko wenzetu

“Lile shetani limeshaondoka, ndio maana nimeweza kutoka” Yasmin akaniambia’

“Halitarudi tena kwa leo?”

“Halitarudi labda kwa kesho”

“Yule mwenzetu ndio ameuawa?”

“Ndio aliuawa. Si mliona wenyewe akikamatwa”

Nikatikisa kichwa changu kusikitika.

“Wakati anabisha mlango niliona ile chupa ya Harishi inajaa moshi. Nikajua kuwa Harishi anakuja. Nikawahi kutoka ili niwambie muondoke. Wakati nasemeshana na yule mwenzenu, Harishi akasikia akawahi kutoka na kumkamata” Yasmin aliendelea kunieleza.

“Sasa yule jinni atatumaliza sote. Tulikuwa watu saba sasa tumebaki watano tu”

“Basi msije kule”

“Sasa tusipokuja utatuletea chakula?”

“Nitawaletea. Na leo ameshakula mtu mmoja harudi tena hadi kesho”

Tukawa tumefika walipokuwa wenzetu.

“Leo tumepata msiba mwingine” Mtu mooja akamwambia Yasmin.

“Nilishawambia tangu mapema kuwa usalama hapa ni mdogo sana kwa sababu ya Harishi. Sasa mnaona wenyewe, na ijui mtafanya nini ndugu zangu”

“Jamani kwanza tuleni chakula. Yasmin ametuletea chakula. Tukanawe mikono kwa maji ya chumvi. Mazungumzo baadaye” nikawambia wenzangu.

Tukaenda kunawa maji ya bahari kisha tukarudi pale chini ya mti, tukaketi. Yasmin naye akaketi.na sisi. Tukaanza kula.

“Kwani Harish ameshaenda zake?” Mtu mmoja akamuuliza Yasmin.

“Ameshaondoka” nikamjibu mimi. “Angekuwepo Yasmin asingeweza kuja huku”

Fuatiliakisahiki hapo na usikose

ITAENDELEA KESHO


Faki A Faki







No comments:

Post a Comment