Monday, December 15, 2014

KISIWA CHA HARISHI

HADITHI
 
KISIWA CHA HARISHI (11)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Akagawa karata, tukacheza hadi usiku mwingi. Wenzangu wengine walikuwa wameshaanza kusinzia. Tukavunja mchezo na kwenda kulala.
 
Tuliingia katika vyumba viwili. Chumba kimoja waliingia watu wawili na chumba kingine waliingia watu watatu. Mmoja aliweka godoro chini. Mimi nilikuwemo katika kile chumba walichongia watu watatu. Nililala kitandani. Na mwenzetu mmoja ndio alilala chini.
 
Licha ya Yasmin kututoa wasiwasi kuwa Harishi hatatokea usiku ule, hatukulala kwa raha. Mara kwa mara nilikabiliwa na hofu. Nilipolala kidogo nilijikuta ninagutuka na kutupa macho huku na huku.
 
Wakati inakaribia kuwa alfajiri ndipo nilipopata usingizi wa uhakika. Nikalala moja kwa moja. Sikuzinduka mpaka kumekucha. Kilichonizindua ni hisia zangu. Niliona kama mlango wa mle chumbani unafunguliwa na mtu aliyekuwa nje.
 
Nilipofumbua macho niliona kweli mlango unafunguliwa na kulikuwa kumeshakucha ingawa Yasmin alituambia tuamke alfajiri na kuondoka.
 
Nikajiuliza ni nani anayefungua mlango. Nikaona kanzu yenye madoa ya damu ikiingia ndani.
 
Alikuwa harishi!
 
SASA ENDELEA
 
Nilishituka sana nilipogundua kuwa aliyefungua ule mlango alikuwa ni jini Harishi. Tulipaswa kujilaumu kwa uzembe wetu wa kulala hadi muda ule wakati Yasmin alituambia tuondoke kabla hakujapambazuka.
 
Na kwa kweli haukuwa uzembe bali tulipitiwa na usingizi, tena wakati mimi nazinduka wenzangu wote walikuwa bado wamelala.
 
Harishi aliingia ndani ya kile chumba. Sasa niliweza kuuona vizuri uso wake. Alikuwa na macho makubwa yenye makengeza.
 
Nikajifanya kama nimelala lakini nilikuwa nikimuangalia kwa pembeni na kwa makengeza huku mwili wangu ukitetemeka kwa hofu.
 
Pengine ni kutokana na ale makengeza yake, Harishi alipoingia mle chumbani macho yake yalikwenda kwa yule mtu aliyelala chini.
 
Mara moja aliinama na kumshika shingo yake kisha akamuinua na kutoka naye ukumbini.
 
Nikaisikia sauti ya Harishi akiuliza.
 
“Hii nyumba ni yako?”
 
Sikusikia jibu bali nilimsikia mwenzetu akipiga ukulele mmoj tu.
 
“Jamani nakufa!”
 
Halafu sikusikia kitu tena.
 
Hapo nilijua mwenzetu huyo alikuwa ameshatoolewa utosi na  alikuwa akifyonzwa damu.
 
Ule ukulele aliopiga ulimuamsha mwenzangu niliyelala naye. Akainuka na kuketi kitandani.
 
“Kitu gani?” akaniuliza.
 
Nikaweka kidole changu cha shahada kwenye midomo yangu kumkataza asitoe sauti.
 
“Nini kwani?” Sasa sauti yake ilikuwa ya chini. Uso wake ulikuwa umeanza kushituka.
 
Nilishuka kitandani nikamnong’oneza “Harishi!”
 
Akagutuka. Uso wake ukabadilika na kuvamiwa na hofu.
 
“Yuko wapi?” akauliza kipumbavu
 
Sikumjibu. Nikamwambia “Tuingie mvunguni mwa kitanda”
 
Akakurupuka na kujiingiza kwenye mvungu huku akiburuza shuka aliyokuwa amejifinika. Tulipoingia kwenye mvungu huo tukanyamaza kimya.
 
Tuliamua kujificha humo japokuwa hatukuwa na uhakika kuwa tutapona. Bada ya muda kidogo tuliona mlango unafunguliwa tena.
 
Nilimuona mwenzangu anatikisa kichwa kwa hofu. Tuliona miguu ya Harishi ikiingia. Ilikuwa miguu mikubwa iliyochafuka na yenye vidole vyenye kucha ndefu. Ilikuwa pekupeku.
 
“Kumbe alikuwa ni yule peke yake!” Tukamsikia akisema Peke yake.
 
Ile shuka ya mwenzangu aliyokuwa akiiburuza ilitokeza nje ya mvungu wa kitanda. Harishi akaiona!
 
Tukaona mkono wake ukishika ncha ya shuka na kuivuta. Jamaa akaiachia. Shuka yote ikavutwa na kuchukuliwa na Harishi.
 
“Hizi ni shuka zangu ninazoziiba kwa Wahindi. Imewekwa na nani huku mvunguni?’ akajiuliza mwenyewe kisha akaitupa chini.
 
Tukaona miguu inageuka na kutoka. Alipotoka tulishukuru. Mimi nilitambaa hadi kwenye mlango, nikaufungua na kumchungulia.
 
Nilimuona akiinama na kuushika mguu wa mwenzetu aliyemuua, akamburuza kuelekea kwenye mlango wa kutokea.
 
Mwenzangu alikuwa amebaki mvunguni akinitazama. Nikaufunga mlango taratibu kisha nikarudi mle mvunguni.
 
“Mwenzetu ameuawa” nikamwambia mwenzangu. “Harishi amemburuza na kutoka naye”
 
“Alimuona wapi?”
 
“Mara ya kwanza aliingia ndani, wewe ulikuwa umelala, Akamsomba pale kwenye godoro na kutoka naye kwenda kumuua. Ndio pale ulipoamka”
 
“Kumbe Yasmin alitaka tufe alipotuambia tulalae humu?”
 
 “Ni makosa yetu sisi. Yasmin alituambia tutoke Alfajiri, sisi tumelala hadi saa hizi kumekucha”
 
“Lakini ni kweli”
 
Wakati tunazungumza kwenye mvungu, Yasmin akaingia.
 
 Tulipoona miguu yake tulitoka mvunguni.
 
“Jamani niliwambia nini?” akatuuliza kwa kutaharuki.
 
ITAENDELEA KESHO NINI KITATOKEA, kumekucha blog

No comments:

Post a Comment