Saturday, December 13, 2014

HADITHI, KISIWA CHA HARISHI SEHEMU YA (10)

SIMULIZI
 
KISIWA CHA HARISHI (10)
 
ILIPOISHIA TOLEO LILILOPITA
 
Tulikula pilau ikiwa ndani ya kapu. Tukashiba na kupata nguvu.
 
“Nimesahau kuwachukulia maji ya kunywa” Yasmin akatuambia.
 
“Na maji tuliyokuwa nayo yamekwisha” nikasema.
 
“Lakini kwa leo Harishi hatarudi, mnaweza kuja nyumbani” Yasmin akatuambia.
 
“Mh!. Nyumbani kwako kunaogopesha” nikamwambia Yasmin.
 
“Tunaweza kwenda mnywe maji halafu mtarudi huku huku”
 
Tukajadiliana na Yasmin, mwisho tukaamua turudi katika lile jumba. Tukarudi.
 
Tulipofika alitupatia maji ya kunywa. Tukamshukuru kwa wema wake.
 
“Bado mna wasiwasi?” Yasmin akatuuliza.
 
“Kuwa na wasiwasi ni lazima” nikamjibu na kuongeza. “Tunajiona kama tuko kwenye vita”
 
“ Kwa leo msiwe na wasiwasi. Yule jini hatarudi tena. Kama ni kurudi ni kesho. Tunaweza kukaa tukaongea hadi usiku mkaenda zenu”
 
Tukashauriana na kukubaliana tukae hadi usiku kwa vile mwenyeji wetu ameshatuhakikishia kuwa tutakuwa salama. Pia tulikuwa tunamuhurumia Yasmin aliyekuwa mpweke katika jumba lile. Tukaona tukae tumchangamshe.
 
Tukakaa kwenye ule ukumbi pamoja na Yasmin na kuanza kuzungumza.
 
“Yasmin alitupa hadithi ya jinsi alivyofikishwa katika jumba lile na jinsi alivyokuwa akilia katika siku za mwanzo mwanzo.
 
ITAENDELEA
.  
“Lile jini hata ukilia, halijali. Linakwambia utazoea tu. Na ni kweli kadiri siku zilivyokwenda nilijikuta nikizoea” Yasmin aliendelea kutuhadithia.
 
“Sasa mnaishije, wakati wewe ni mtu na yule ni jini?” Mwenzetu mmoja akamuuliza.
 
“Tunaishi kama mke na mume ingawa mwenzangu ni jini lakini ndio nimeshamzoea. Ameshaniambia kwamba nitaishi naye hadi kufa kwangu”
 
“Je kama akifa yeye?” nikamuuliza.
 
“Amesema yeye hatakufa haraka. Umri wa majini ni mrefu sana. Pale alipo ana miaka mia tatu na anaweza kuishi hadi miaka mia tano”
 
“Loh!. Wewe utakufa, yeye ataendelea kuishi kwa miaka mingi sana” Mtu mmoja akamwambia Yasmin.
 
“Lakini mimi ningependa kujua hisia zako. Unajisikiaje unapohisi kuwa utaishi ndani a jumba hili hadi ufe wakati bado ni msichana mdogo” Mimi nilimuuliza Yasmin swali hilo.
 
Yasmin akabetua mabega.
 
“Nasikia vibaya lakini nitafanyaje sasa. Nimelia nimechoka, sasa silii tena”
 
 
“Kwa hiyo ndio unaishi ukisubiri kifo chako kitokee humu humu ndani?” Mtu mwingine alimuuliza. Lilikuwa si swali zuri. Sikulipenda. Lakini Yasmin alimjibu.
 
“Wakati mwingine najidanganya kwamba iko siku yaweza kutokea miujiza nikaokolewa kwa namna nisiyoijua.
 
“Na tangu uishi humu hakujatokea watu kama sisi wakaingia katika jumba hili?” nikamuuliza.
 
“Nyinyi ndio watu wa kwanza kuwaona tangu nianze kuishi katika jumba hili”
 
Tukaendelea kuzungumza na Yasmin hadi alipotuambia kuwa anakwenda kupika chakula cha usiku.
 
Tukabaki sisi peke yetu na kuendelea kuzungumza na kujadiliana kuhusu maisha ya Yasmin na maisha yetu wenyewe.
 
Jua lilipokuwa limekuchwa nilimfuata Yasmin jikoni nikamwambia kwamba tunaondoka.
 
“Kwanini…subirini mle chakula. Nimepika chakula kingi kwa ajili yenu” Yasmin akaniambia
 
“Giza linaingia. Tuna hofu yule jini anaweza kutokea. Acha tuondoke tu”
 
“Jamani mkiwepo mnanichangamsha na mimi. Sasa mnataka kwenda wapi?”
 
“Tunarudi kule kule ulikotukuta”
 
“Kwanini jamani? Nimewambia Harishi hawezi kurudi leo labda kwa kesho. Mnaweza hata kulala hapa na mkawa salama. Muhimu ni kuamka kabla hakujapambazuka mwende zenu”
 
“Unajua tuna hofu na wasiwasi, wenzetu wawili wameshauawa humu humu ndani”
 
“Sasa kule mtakaaje usiku huu na baridi? Je mvua ikinyesha usiku huu mtafanyaje. Si bora mlale hapa hapa”
 
“Ngoja nikawashauri wenzangu” nikamwambia Yasmin na kurudi kule ukumbini. Yasmin naye akanifuata.
 
“Yasmin amesema tusubiri chakula na pia tunaweza kulala hapa hapa” nikawambia wenzangu.
 
“Tulale hapa hapa?” Mtu mmoja akaniuliza kwa mshituko.
 
“Hakuna neno. Mnaweza kulala tu ilimradi muamke alfajiri kabla ya kupambazuka mwende zenu” Yasmin akawambia.
 
“Una hakika kwamba Harish hatakuja usiku huu?’
 
“Hatakuja tena kwa leo ila kesho anaweza kuja. Sasa kwa vile sijui atakuja saa ngapi ndio maana nninawambia muondoke alfajiri”
 
Yasmin alipoona wenzangu wameduwaa wakitazamana kutafakari yale maneno yake akatuambia.
 
“Jamani kuweni na mimi. Hivi nashukuru kupata wenzangu wa kunichangamsha. Harish hatakuja tena leo”
 
“Mimi naona tumsikilize mwenyeji wetu, acha tukae” Nikawambia wenzangu kwa kumuonea huruma Yasmin.
 
Pia huko tulikotaka kwenda hakukuwa salama. Tungeweza kushambuliwa na wanyama usiku ule au kunyeshewa na mvua.
 
Tukakubaliana kuwa tubaki na Yasmin.
 
“Hakuna lolote litakalotokea, kaeni kwa roho moja. Mimi ndiye ninayejua kawaida na nyendo za Harishi. Mnachotakiwa ni kujihimu wakati wa alfajiri muondoke humu ndani ili kama kesho atatokea asiwakute” Yasmin akatusisitizia kabla ya kurudi jikoni.
 
Baada ya muda kidogo alituletea chakula, tukala pamoja na yeye.
 
Tulipomaliza kula Yasmin aliondoa vyombo. Aliporudi tena alikuwa ameshika karata. Akaketi na kutuambia. “Sasa tuchezeni karata, tukichoka tunakwenda kulala”
 
ITAENDELEA KESHO
USIPITWE NA KISA HIKI CHA KUSISIMUA KESHO NINI KITATOKEA WAKATI WA KUCHEZA KARATA

No comments:

Post a Comment