Saturday, December 13, 2014

WAHAMIAJI HARAMU 12 WANASWA WAKIWA HOI KWA NJAA

Kumekucha blog

Korogwe,POLISI Wilayani Korogwe Mkoani Tanga  imewakamata wahamiaji haramu 12 wenye asili ya Kiethopia wakiwa wamefichwa katika gari wakisafirishwa kuelekea Dar esSalaam na hali zao kukutwa zikiwa mbaya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake, kamanda wa polisi Mkoani hapa, Freisser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni katika kizuizi cha polisi kijiji cha Bwiko barabara ya Mombo Segera.

Akiwataja watu hao kuwa ni, Kashoma Bayen(24), Berchano Gamada(32), Awal Jamal(23),Yanis Gatiso(28), Metson Sipril(21), Tashona Hayalis(30), Adino Samiru(20)Kengeny Siyun(22),Charnes Egesa(20),Abdi Badru(21), Siumanda Samadu(26) na Malako Abuu (23) wote wakiwa ni raia wa Ethopia.

“Hawa watu walikamatwa wakiwa wamefichwa katika gari aina ya scania wakiwa hali zao ni dhaifu na kutia  huruma----ukiwaangalia utwaonea huruma kwani hata kuzungumza hawawezi kwa njaa” alisema Kashai na kuongeza

“Tunapowakamata wahamiaji haramu kwanza tunawabana waliowasfirisha ninani  lengo ni  kuwatia mbaroni----tatizo lililojitokeza kwa a hawa  hawajui kuzungumza Kiswahili wala kiingereza na zaidi kusema pia ni tabu kwa kuumwa na njaa” alisema

Alisema wakati wa mahojiano ilikuwa vigumu kufahamiana baada ya watu hao kutojua kuzungumza Kiswahili wala kiingereza na hivyo kupata majina yao na kuwa vigumu kupata maelezo ya watu waliowasafirisha.

Alisema kwa sasa polisi inaendelea kufanya upelelezi na mara baada ya kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kuingia nchini bila kibali.

Akizungumzia kuhusu watu wanaofanya biashara ya kusafirisha watu, kamanda Kashai alisema polisi itaendelea kufanya upelelezi kwa baadhi ya watu ambao wanatuhumiwa kujihusisha na biashara hiyo haramu.

Alisema polisi iko na taarifa kutoka kwa watu mjini na maeneo ya mipakani mwa nchi jirani ya Kenya hivyo kuamini kuwa itawakamata na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

“Tuko na majina ya baadhi ya watu na tunayafanyia uchunguzi na ukikamilika kama itabainika tutawakamata kwa mahojiano-----tunataka kudhibiti mianya yote ya upitishaji wa mali za magendo na wahamiaji haramu” alisema Kashai

Akitoa wito aliwataka wananchi kushirikiana na polisi katika mambo mbalimbali ya kiusalama pamoja na kupeana taarifa za matukio ya kihalifu pamoja na kuwafichua watu wanaofanya biashara haramu ya kusafirisha binadamu

                                         Mwisho                        

No comments:

Post a Comment