Kumekucha blog, Handeni
Handeni,KERO ya upatikanaji wa maji Wilayani
Handeni Mkoani Tanga bado limekuwa likiwasumbua
wakazi wake na hivyo kuitaka Serikali kama iko na dhamira ya kweli ya kulipatia
ufumbuzi kuanza mchakato wake.
Wakizungumza wakati wa kongamano la vijana na Maendeleo jana,
walisema wagonjwa wengi katika vituo vya afya wanaugua magonjwa ya kichocho na
matumbo na kushindwa kufanya kazi za kujiletea maendeleo.
Walisema kwa miaka mingi viongozi wa Serikali na wa vyama
wamekuwa wakitoa matumaini ya kulimaliza tatizo hilo lakini hakuna dalili
zozote na hivyo kutaka kuangaliwa kwa jicho la huruma ili kulinda afya za
wananchi.
“Serikali imekuwa ikipiga nara ya kampeni yake ya kilimo
kwanza----mimi nasema maji kwanza kwani bila ya maji huwezi kufanya jambo
lolote na hata huko maofisini hakutakalika” alisema Rajab Shamte
“Naiomba Serikali kubadilisha kauli mbiu yake na kusema maji
kwanza na sio kilimo kwanza----bila ya maji huwezi kulima hata bustani
majumbani” alisema Shamte
Vijana hao wamesema wamekuwa wakishirikishwa katika
makongamano mbalimbali kuzungumzia kero ya maji na kutumika pesa za wananchi lakini hakuna linaloendelea zaidi ya
malalamiko hayo kuishia katika makaratasi.
Kwa upande wake mkazi wa Misima, Farijala Said. Aliwataka vijana
wenzake kuutumia vyema uchaguzi wa Serikali za mitaa kwa kuwachagua viongozi
ambao watakuwa na uchungu na wananchi.
Alisema vipindi vya kampeni za uchaguzi ni wakati wa
kuwachagua watu ambao watakuwa na moyo wa kuitumikia jamii na kuwasikiliza
ikiwa na pamoja na kuzifikisha kero zao katika ngazi husika.
Alisema vipindi vya uchaguzi wamekuwa wakizuka wagombea na
kutoa ahadi kemukemu na kushindwa
kuzitekeleza jambo ambalo wananchi wanatakiwa kuwa makini na watu hao.
“Nawaomba vijana wenzangu kipindi hiki cha kampeni za
uchaguzi wa Serikali za mitaa kuwa makini na wagombea-----hii ni kutokana na
kuzoea kudanganywa” alisema Said
Aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi wa
viongozi na kuchagua wanaofaa ambao watakuwa bega kwa bega na wananchi walio
katika kuharakisha maendeleo yao.
Mwisho
No comments:
Post a Comment