Wednesday, December 10, 2014

VITENDO VYA KIKATILI VYA KIJINSIA NA NGONO LA KULAZIMISHANA HUCHANGIA UKIMWI

Kumekucha blog

Tanga,WANAHARAKATI na wadau mbalimbali wanaopiga vita vitendo vya Ukatili wa kijinsia Tanga, wamedai  kuongezeka kwa Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi Mkoani humo ni kutokana na baadhi ya wanaume kuwalazimisha wanawake kufanya vitendo vya ngono na usagaji kwa wanawake.

Akizungumza katika kilele cha siku 16 za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia jana, Afisa Mradi mwandamizi wa Asasi ya Kiraia ya Tree of Hope, Goodluck Malilo, alisema kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi ni kutokana na wanaume  kuwalazimisha wanawake kufanya vitendo vya ngono bila ridhaa.

Alisema jamii kama haitopiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto, maambukizi ya virusi vya Ukimwi havitopungua na hivyo kuitaka kukemewa kwa nguvu zote.

“Leo tunaadhimisha siku kumi na sita za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia----tumeona maambukizi badala ya kupungua yanazidi kuongezeka kwa kasi” alisema Malilo na kuongeza

“Kuna baadhi ya watu wanaojitambua wamekuwa wakiwalazimisha iwe ni wanaume au wanawake kufanya vitengo vya ngono zembe huku wakijijua kuwa wako na maambukizi---kwa pamoja tupige vita na tuishinde” alisema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Asasi ya Tree of Hope, Fourtunata Manyeresa, amewataka wanawake na wasichana mashuleni kutoa taarifa za vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia kwa walimu wao .

Alisema kuna baadhi ya wanawake na wasichana mashuleni wamekuwa wasiri baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na kudhani kuwa kusema  itakuwa aibu na fedheha kwa jamii.

Alisema hali hiyo pia imekuwa ikitokea majumbani ambapo wanawake wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kijinsia kwa waume zao na hivyo kuwataka kuwa na moyo wa ujasiri kwa kutoa taarifa katika madawati na vyombo vya sheria.

“Kampeni bado inahitajika majumbani na mashuleni pamoja na kutoa elimu katika sehemu za wazi hii ni kutokana na watu kumezea baada ya kuogopa kusema juu ya vitendo wanavyofanyiwa iwe ni waume zao au marafiki wa kiume na wa kike” alisema Manyeresa

Katika kuadhimisha siku 16 za kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia Asasi hiyo ya Tree of Hope ilienda sambamba na kampeni ya Tunaweza iliyolenga kusajili wanamabadiliko wanaume kwa wanawake watakaokuwa mstari wa mbele kukemea na kupiga vita vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kupita mitaani kuhamasisha kujisajili.
                                                   Mwisho

No comments:

Post a Comment