Tanzania ifikapo mwaka 2025
Matokeo haya yametolewa na Twaweza
na Society for International Development (SID) kwenye muhtasari wa
utafiti wenye jina la Tanzania ifikapo mwaka 2025: Je, Watanzania wana
matarajio gani na maisha yao ya baadaye? Muhtasari umetokana na takwimu
za Sauti za Wananchi, utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi
wa kitaifa unaofanyika kwa njia ya simu za mkononi. Utafiti huu
hufanyika katika maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haimo kwenye
matokeo haya). Matokeo haya yametokana na takwimu zilizokusanywa kutoka
kwa wahojiwa 1,408 mwezi Agosti 2014.
Wakiangalia nchi kwa ujumla,
wananchi wawili kati ya watatu wanaamini kuwa Tanzania itakuwa mahali
pazuri pa kuishi mwaka 2025. Wananchi makundi yote bila kujali hali zao
za kiuchumi wanaamini hivyo; mathalan, wananchi wenye kipato kikubwa 64%
na wananchi maskini 68% wana matumaini na siku zijazo. Watanzania wana
matumaini na akiba tuliyonayo kwa ajili ya nchi.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi
bado wana wasiwasi. Karibu mwananchi mmoja kati ya watano (18%)
wanahofia maisha yako yatakuwa mabaya zaidi mwaka 2025 kuliko yalivyo
leo, na wapo wengine wanaodhani nchi itakuwa mahali pabaya pa kuishi
mwaka 2025. Hapa kuna baadhi ya tofauti kati ya matajiri na maskini,
mwananchi mmoja kati ya wanne katika kundi la matajiri (25%) na mmoja
kati ya watano katika kundi la maskini (18%) hawana matumaini kuhusu
siku zijazo.
Haijalishi mtazamo gani wananchi
wanao, bado wanaamini kuwa matokeo na mustakabali wa Tanzania uko
mikononi mwa Watanzania. Wananchi tisa kati ya kumi wanaamini kuwa
viongozi wa Tanzania (54%) au wananchi (37%) watakuwa na udhibiti zaidi
wa maamuzi ya nchi yao. Linapokuja suala la maisha yao wenyewe, wananchi
wanaamini jitihada zao wenyewe kuwa ndizo zitazobadilisha maisha yao;
wananchi sita kati ya kumi wanafikiri kuwa wao wenyewe ndio wenye
ushawishi zaidi juu ya hatma yao ya baadaye. Hata hivyo, wakati
mwananchi mmoja kati ya watano anaamini kuwa Serikali itakuwa na
ushawishi mkubwa juu ya ustawi wa maisha yao ya baadaye, hakuna
mwananchi wa mjini aliyetaja Serikali kama ina ushawishi muhimu. Mbali
na wao wenyewe, wahojiwa wa mijini walitaja familia zao (20%) na
marafiki au wenzao (19%) kuwa wenye ushawishi juu ya maisha yao ya
baadaye.
Ukiangalia kila jambo moja baada
ya jingine, karibu wananchi watatu kati ya wanne (72%) wanaamini kuwa
Tanzania itakuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025. Wananchi saba
kati ya kumi (68%) pia wanafikiri kutakuwa na Rais mwanamke ifikapo
mwaka 2025, na wananchi sita kati ya kumi (64%) wanatabiri kukua kwa
uzalishaji wa viwanda na kupungua kwa kilimo. Kwa upande mwingine,
wananchi wengi wanatabiri kutokea migogoro ya kidini (62%) na nusu yao
(51%) wanatarajia kugawanyika kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Chochote kitakachotokea huko mbeleni, wananchi wanaona mabadiliko
makubwa, wananchi sita kati ya kumi wanatabiri kuwa upinzani utashinda
urais, na tembo watapotea kabisa ifikapo 2025. Jambo la kushangaza,
matukio mawili yenye uwezekano mdogo kutokea ni Tanzania kufuzu
kushiriki mashindano ya Kombe la Dunia (38% ) na kuanzishwa kwa
Shirikisho la Afrika Mashariki chini ya Rais mmoja (34%).
Mambo muhimu wanayotaka wananchi
kwa siku zijazo ni maboresho kwenye huduma za kijamii (28% wanaona ni
kipaumbele chao muhimu) na ukuaji wa uchumi (16% wanaona ni kipaumbele
muhimu).
Aidan Eyakuze, Mkurugenzi wa
shirika la Society for International Development, alitoa maoni yake
kwenye matokeo haya “Watanzania kwa kiasi kikubwa wana matumaini na
maisha yao binafsi ya baadaye, hasa ikilinganishwa na wenzao kutoka nchi
zenye maendeleo makubwa kiuchumi, Marekani na Ulaya. Matumaini haya na
mtazamo chanya ni mtaji mkubwa. Vinaimarisha uwezo wa nchi kusonga mbele
kwa kujiamini na pia inaweka mzigo kwa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa
tunafikia malengo ya mafanikio kwa nchi yetu.”
Rakesh Rajani, Mkuu wa Twaweza,
alisema “Katika kipindi cha mabadiliko muhimu ya kitaifa na ya
kimataifa, wananchi wa matabaka yote kiuchumi, maeneo na jinsia zote,
wana matumaini kuhusu kile kilichopo siku za mbeleni nchini Tanzania.
Changamoto kwa Serikali ya Tanzania, wasomi wa ndani pamoja na wananchi
wenyewe, ni kuhakikisha kuwa matumaini haya yanaendelezwa kupitia
utungaji sera na utekelezaji wenye ufanisi, kuhimiza maendeleo yenye
usawa na kujenga mshikamano wa kijamii, ili matarajio ya wananchi ya
maisha bora siku zijazo yafikiwe.”
No comments:
Post a Comment