Monday, December 15, 2014

POLISI WAMTIA MBARONI KINARA KUSAFIRISHA WAHAMIAJI HARAMU

KUMEKUCHA BLOG

Tanga,WAKATI jeshi la polisi likiumiza vichwa kuwabaini wafanyabiashara wa kusafirisha wahamiaji haramu kwa kutumia mipaka na nchi jirani ya Kenya , polisi Mkoani Tanga imefanikiwa kumkamata mtu anaedaiwa kuwa kinara wa usafirishaji.

Mtu huyo alietajwa kuwa ni Ali Mbukuzi (27) mkazi wa kijiji cha Chongoleani kata ya Zingibari Wilayani Mkinga Mkoani hapa, anadaiwa kuwa kinara wa kusuka mipango na kuwasafirisha kupitia njia za panya ikiwemo misitu ya Horohoro na  Handeni.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, kamanda wa polisi Mkoani hapa, Freisser Kashai, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 8 usiku wakati polisi wakiwa katika doria katika vijiji na msitu wa Horohoro unaopakana na nchi jirani ya Kenya.

Alisema polisi ilitaarifiwa kuwepo kwa kundi la wahamiaji haramu ambao walikuwa wamefichwa katika nyumba kijiji cha Zingibari Wilayani Mkinga wakitokea nchi jirani ya Kenya.

“Tumemkamata mtu ambaye tunadhani ndie kinara wa kusafirisha na kusuka mipango ya kusafirisha wahamiaji haramu----kwa muda mrefu tulikuwa tunamtafuta na alikuwa akikwepa mitego yetu” alisema Kashai na kuongeza

“Tulivamia banda lililoko porini na kumkuta akiwa amelala usingizi na wahamiaji haramu wa Kiethopia na aliposhtuka hakuweza kukimbia---tunamuhoji ili kuujua mtandao mzima” alisema Kashai

Akitoa wito kwa wananchi wanaokaa kandokando na mpaka wa Mombasa , kamanda Kashai, aliwataka kuacha kushirikiana na watu wanaosafirisha wahamiaji haramu pamoja na magendo na kusema kuwa msako utafanywa usiku na mchana.

Alisema tatizo kubwa kwa wananchi wanaokaa karibu na mipaka wamekuwa wakiogopa kutoa taarifa za kihalifu na za kimagendo na hivyo kuwataka kuwasiliana na polisi kwa kutoa taarifa.

“Tatizo kubwa kwa wakazi wa mipakani wamekuwa wasiri na hofu ya kutoa taarifa za kihalifu----huenda wana maslahi nayo ndio maana wanawaficha----dhamira yetu ni kuharibu mitandao yote ya magendo na usafirishaji binadamu” alisema Kashai

Alisema hatua kali zitachukuliwa mtu yoyote ambaye atabainika kwa namna moja au nyengine kushirikiana na wahalifu na hivyo kuwataka kuwa makini na zoezi hilo litafanyika muda wowote.

                                     Mwisho              

No comments:

Post a Comment