Tangakumekuchablog
Lushoto, SHIRIKA
la umeme Tanzania (Tanesco) Wilayani Lushoto Mkoani Tanga limefanikiwa kugundua
kusimikwa nguzo nne za umeme na watu wanaoaminika kuwa ni vishoka ambazo zilikuwa katika hatua za mwisho za kuunganishwa umeme na kuingizwa majumbani.
Hatua hiyo imekuja baada ya
operesheni saka vishoka iliyofanywa kwa siku tatu katika maeneo mbalimbali
Wilayani humo na kufanikiwa kugundua wizi wa umeme katika nyumba pamoja na
usimikaji wa nguzo za umeme kinyume na taratibu.
Akizungumza katika eneo la tukio
kijiji cha Baga na Mtae ziliposimikwa
nguzo hizo, Kaimu meneja wa Shirika la umeme Tanesco Lushoto, Daudy Kupaza,
alisema kugundulika huko kulikuja baada operesheni saka vishoka ambayo wameifanya
kwa siku tatu mfululizo.
Aliwataka wateja ambao wanataka kuunganishiwa umeme majumban kufuata taratibu kwa kufika katika ofisi za
shirika hilo na kuepukana na vishoka ambao huwatapeli .
“Tunatambua kuwa kuna watu ambao ni
vishoka kwa kujifanya wafanyakazi wa shirika la umeme-----watu hawa wamekuwa
wakitusumbua sisi na wateja wetu” alisema Kupaza na kuongeza
“Katika operesheni yetu saka vishoka
tumegundua kusimikwa kwa nguzo nne kinyume cha sheria---na sasa tunamtafuta huyo
alieziweka na tuko katika uchunguzi na mara tutakapomgundua itakuwa fundisho
kwa wengine” alisema
Kwa upande wake mkazi wa kijiji cha
Bagai, Shaban Juma, amelitaka shirika la umeme kuwaelimisha wateja wao
wanaotaka kufungiwa umeme hasa wa vijijini ili kuepuka kutapeliwa na mafundi
vishoka.
Alisema wateja wa vijijini ambao
umeme bado haujafika ni vyema shirika hilo kutoa elimu ya kujua namna ambavyo
taratibu za kupatiwa umeme zinavyofuatwa na kuepuka kutapeliwa na vishoka.
“Kama shirika la umeme halitokuwa na
utaratbu wa kuwaelimisha wateja wake hasa yale maeneo ya vijijini ambayo wanataka kupeleka umeme mafundi vishoka hawataisha” alisema Juma
“Kuna vishoka wengine wanadiriki
hata kuwa na vitambulisho feki vinavyowatambulisha kama wafanyakazi wa shirika
la umeme----na hii inaleta uaminifu wanapokuja kwetu na pale wanapotutapeli
ndio tunashtuka” alisema
Alisema ili kuweza kutokomeza
vishoka ni vyema shirika la umeme Tanzania Tanesco kuweka sheria kali za
kuwabana vishoka na kuweza kulitokomeza tatizo hilo ambalo limeota mizizi kila
kona.
No comments:
Post a Comment