Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu cha Candle Education Centre Tanga. Kituo kinaongoza kwa kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita kwa wanaorisiti. Pia kituo kinatoa kozi ya Kiingereza na Computer. Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limeshindwa kumhoji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Askofu Josephat Gwajima, kutokana na mwenendo wa afya yake.
Jana Mwanasheria wa askofu huyo Paul Mallya
akiambatana na Askofu Gwajima akiwa kwenye baiskeli ya magurudumu
mawili ya kubeba wagonjwa, walifika katika Kituo Kikuu cha Polisi,
jijini Dar es Salaam saa 2.00 asubuhi kwa ajili ya kuitikia wito wa
polisi uliotaka Askofu huyo akahojiwe.
Hata hivyo, kabla hajamaliza kupandishwa
ngazi ya pili kuingia kwenye jengo la ofisi za kituo hicho, polisi
walisema hawawezi kumhoji mpaka afya yake itakapoimarika.
“Tulifika
kituo kikuu cha polisi saa 2.00 asubuhi tukiwa tayari kwa mahojiano.
Askofu alipoanza kupandishwa ngazi akiwa katika baiskeli ya magurudumu
mawili ya kubeba wagonjwa, polisi walipomuona, kabla hajamaliza kupanda,
walitwambia ni vyema akarudi nyumbani mpaka Aprili 9, mwaka huu ndipo
wamhoji,” alisema Mallya.
Alisema kuna mtu aliyetambulika kwa jina
la Abubakar Yusufu, mkazi wa Kiluvya, wilaya ya Kisarawe, mkoa wa
Pwani, ndiye amefungua kesi ya jinai polisi akilalamika kukwazwa na
lugha iliyotumiwa na Askofu Gwajima dhidi ya Askofu Mkuu Kanisa Katoliki
Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Polycarp Kardinali Pengo.
Askofu Gwajima alifika katika kituo hicho akisindikizwa na msafara wa magari matatu.
Gari la kwanza lilimbeba Mchungaji
Baraka; la pili, aina ya Land Cruiser alikuwamo Askofu Gwajima na la
tatu lilikuwa lake (Mallya).
Tofauti na ilivyokuwa Jumanne kwa
wafuasi wengi wa Askofu Gwajima kufurika katika kituo hicho na
kulilazimisha Jeshi la Polisi liimarishe ulinzi kwa ajili ya
kuwadhibiti, jana hawakuwapo.
Jana Askofu huyo hakuzungumza chochote badala yake Mallya ndiye aliyezungumza kwa kifupi na waandishi.
Mallya alisema Askofu Gwajima amefunguliwa mashtaka ya jinai yanayohusisha kutumia lugha kumkashifu Kardinali Pengo.
Alisema Yusufu alifungua mashtaka hayo
kutokana na picha ya video aliyoiona kwenye mitandao ya kijamii
inayomuonyesha Askofu Gwajima akitumia lugha ya matusi kumkashifu Askofu
Pengo ambayo kisheria ni kosa.
Machi 26, mwaka huu, Jeshi la Polisi
Kanda hiyo lilimwamuru Askofu Gwajima kujisalimilisha polisi kwa tuhuma
za kumkashifu Kardinali Pengo.
Baadaye, Machi 27, Askofu Gwajima
alijisalimisha kituo hicho lakini wakati akihojiwa alizimia akiwa chumba
cha mahojiano kisha kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ kwa matibabu.
NIPASHE
Shinikizo la kumshawishi Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa,
kuchukua fomu ya kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu Oktoba, mwaka huu,
limeendelea na safari hii wanafunzi wa vyuo vikuu vitatu vya jijini
Mwanza, wakitoa tamko la kumtaka kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana jijini hapa, viongozi wa vyuo vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo Kikuu Katoliki cha Sayansi na Tiba za Afya (CUHAS), walimtaka Lowassa kuchukua fomu ya kuwania urais wakati ukifika.
Viongozi hao waliyazungumza hayo wakati
wakikabidhi misaada mbalimbali kwenye kituo cha kulelea watoto yatima
cha Upendo Daima, jijini Mwanza.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa CUHAS, Godfrey Kisigo, alisema wameamua kumuunga mkono Lowassa kwa sababu anapendwa na kila Mtanzania.
Alisema wanamuomba muda ukifika awe mtu wa kwanza kujitokeza kuchukua fomu ili kugombea nafasi ya urais.
“Tamko
hili ni la vyuo vikuu vyote vya Mwanza, sauti zetu ni za busara kwa
sababu zinataka kuikomboa nchi yetu kwa miaka 10 ijayo, tunayo imani
kubwa na Lowassa katika hatma ya nchi hususan elimu kwa watu wote,” alisema na kuongeza:
“Hatma
ya nchi hii ipo mikononi mwako na sisi wanavyuo hatuwezi kusubiri kuona
tunakosa kiongozi atakayelisaidia Taifa kwa kuzibwa midomo, tupo tayari
kufa ili uwe rais uokoe watakaobaki na Tanzania.”
Waziri Mkuu wa Serikali ya wanafunzi SAUT, Christopher Mkodo, alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM)
kisijaribu kukata jina la Lowassa kwani Tanzania bila kiongozi huyo
Watanzania watakuwa wamenyimwa fursa ya kupata maendeleo ndani ya miaka
10.
Waliitaka CCM kusikiliza maoni ya wanachama wake vinginevyo chama kitaharibika.
Mwakilishi wa CBE, Paul Dotto,
alisema Lowassa ni chaguo la wanafunzi wa vyuo vikuu na wana imani
ataifikisha Tanzania katika uchumi wa kati kabla ya malengo yaliyowekwa
na Serikali.
NiPASHE
Chama cha Wananchi (CUF) kimelaani kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kwamba anawaburuza wabunge wa upinzani kwa sababu hawafuati utaratibu bungeni.
Makinda alisema hayo alipokuwa akiwajibu wabunge wa upinzani waliolalamika kuburuzwa baada ya Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, kuomba majibu kutoka kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuhusu kura ya maoni.
Naibu Mkurugenzi wa Habari na Uenezi a CUF Taifa, Abdul Kambaya, alisema kauli hiyo ya Makinda ni ya dharau, ambayo hazipaswi kutolewa, hasa na kiongozi wa wabunge.
“Spika
Makinda anakuwa chanzo cha vurugu bungeni, hasa kwa kuwa mtetezi wa
serikali bungeni, badala ya kuwa kiongozi wa Bunge asiyeegemea upande
wowote,” Kambaya.
Alisema kitendo cha Spika Makinda
kulazimisha kusomwa miswada miwili kuhusu habari na matumizi ya mitandao
ya kijamii, hakikubaliki kwa Watanzania na kinadhihirisha kishachoka
kuliongoza Bunge.
“CUF tunamuonya Spika Makinda aache ukada wa CCM na kuiegemea serikali wakati maslahi ya wananchi yanavunjwa na kukanyagwa,” Kambaya.
Alimtaka Spika Makinda kutambua kuwa iwapo ataendelea na utaratibu huo, atalivuruga Bunge na kutowesha amani.
MWANANCHI
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)
imekubali kuahirisha upigiaji Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa
iliyopangwa kufanyika Aprili 30, mwaka huu kutokana na kutokamilika kwa
uandikishaji wa Daftrai la kudumu la wapiga kura kwa kutumia teknolojia
ya Biometric Voters Registration (BVR).
Hatua hiyo inakuja baada ya kuwepo
mfululizo wa matamko na ushauri kutoka kwa wadau mbalimbali wa
demokrasia kwamba zoezi hilo lisingewezekana kwa sasa hasa kutokana
kusuasua kwa mwenendo wa BVR.
Mwenyekiti wa Nec Jaji Mstaafu Damian Lubuva
aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa kazi ya
uboreshaji daftari la wapiga kura ni ya msingi kabla ya taratibu zote za
upigaji kura.
Jaji Lubuva aliyeonekana kuwa mpole
zaidi, alisema kwa uzoefu walioupata Njombe, zoezi la uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapiga kura bado halijakamilika katika mkoa huo na
mingine iliyosalia.
“Hivyo
tume haitaweza kuendelea na zoezi la upigaji kura ya maoni na zoezi
hilo lililotangazwa hapo awali kufanyika Aprili 30, 2015 limeahirishwa
hadi tarehe itakapotangazwa na Nec baada ya kushauriana na Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar,” Jaji Lubuva.
Kwa nyakati tofauti, vyama vya siasa,
asasi za kiraia, taasisi za kidini na wananchi wamekuwa wakiishauri Nec
kuahirisha Kura ya Maoni huku vyama vya siasa vikimtaka Rais Jakaya
Kikwete atii makubaliano yaliyofikiwa na Kituo cha Demokrasia (TCD)
mwaka jana ya kuahirisha zoezi hilo hadi baada ya Uchaguzi mkuu.
Jaji Lubuva alisema kuwa tume yake
inaendelea kuboresha daftari la wapiga kura nchi nzima ambapo
wanatarajia kukamilisha ifikapo Julai mwaka huu. Nec ilieleza kuwa baada
ya kumaliza uandikishaji mkoani Njombe watahamia mikoa ya Ruvuma,
Lindi, Mtwara na Iringa.
MWANANCHI
Mwanamke mmoja aliyejeruhiwa na wananchi
ametelekezwa barabarani na wauguzi wa Zahanati ya Nzera iliyopo Geita
kwa kile kinachodaiwa ni mchawi.
Hata hivyo kaimu mganga wa Zahanati hiyo
Bigaeli Kasala alipinga madai hayo akisema hajatelekezwa bali bali
alikuwa akitafutiwa usafiri wa kumpeleka Geita kwa matibabu zaidi.
“Huyu
mgonjwa hatujamtupa,niliwakabidhi wahusumu wampandishe basi la asubuhi
linalokwenda Geita lakini inaonekana walipitwa na basi hivyo wakamuacha
barabarani akisubiri basi jingine”-Kasala.
Dk. Kasala alisema kituo chao hakina gari la wagonjwa ndio maana walimwacha barabarani akisubiri gari lingine.
Awali alidai mwanamke huyo alipelekwa
Zahanati hapo wa kituo ch polisi baada ya kumwokoa mikononi mwa wananchi
waliokuwa wakimpiga wakimtuhumu kuwa ni mchawi.
Alisema alikutwa kwenye nyumba akiwa
mtupu na kutuhumiwa alikuwa akifanya uchawi na ndipo watu wakaanza
kumpiga hadi kumvunja kiuno.
MWANANCHI
Hoja 22 za kupinga vifungu Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao wa
mwaka 2015 zilizotolewa juzi na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu jana zilisababisha kikao cha 14 cha Bunge kuvunja rekodi ya kutumia muda mrefu baada ya kumalizika saa 6.15 usiku.
Marekebisho yaliyowasilishwa na Lissu yaliungwa mkono na Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika
ambaye pia alikuwa na marekebisho yake katika muswada huo, hivyo wote
wawili kuichachafya Serikali bila mafanikio baada ya muswada huo
kupitishwa kwa sauti kubwa ya “Ndiyooo” ya wabunge wa CCM.
Kuanzia saa 12.30 jioni, Bunge lilikaa kama kamati kupitisha muswada
huo baada ya kumaliza kuupitisha muswada wa Sheria ya Miamala ya
Kielektroniki ambao haukuwa na mvutano mkali.
Mvutano wa kisheria kati ya Lissu dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, naibu wake, January Makamba ulianza saa 12.30 jioni hadi saa 5.30 usiku na baadaye Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akatumia muda uliosalia kuahirisha Bunge.
Mpaka inafika saa 5.00 usiku wabunge wa upinzani waliokuwapo bungeni
walikuwa 12 tu, akiwamo Lissu na Mnyika na hivyo kufanya idadi ya
wabunge wote kuwa 86, wakiwamo wa CCM na mawaziri.
Kuna wakati Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge
alilazimika kusimama kutoa ufafanuzi wa kina, ikiwa ni pamoja na namna
ya kuvitamka kwa ufasaha vifungu vya sheria ili kukubalika na pande
mbili zilizokuwa zinavutana.
Mapendekezo yote yaliyotolewa na Chenge ambaye amewahi kuwa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, yaliungwa mkono na Lissu pamoja na Masaju
na Wizara ya Mawasiliano.
Wakati mnyukano huo ukiendelea, Pinda alikuwa kimya akisubiri kusoma hotuba yake ya kuahirisha Bunge.
Pinda alianza kusoma hotuba hiyo saa 5.30 usiku mpaka saa 6.00 usiku,
ikiwa ni baada ya Bunge kuupitisha muswada huo. Baada ya dakika 15 za
kutoa matangazo mbalimbali na kuwashukuru wabunge, Spika Makinda
aliahirisha mkutano huo.
Kuna wakati Lissu aliwataka wabunge kutochoka kutokana na hoja
anazozitoa kusababisha kikao hicho kuwa kirefu, huku Makinda naye
akiwaeleza wabunge kuwa ‘zege halilali’, akimaanisha kuwa Bunge haliwezi kuahirishwa mpaka muswada huo upitishwe na Pinda atoe hotuba ya kuahirisha Bunge.
Kati ya marekebisho 22 yaliyowasilishwa
na Lissu, ni matano tu yaliyokubaliwa na Serikali huku Lissu akikubali
vifungu viwili tu vilivyofanyiwa marekebisho na Serikali, akivisifia
kuwa vimeandikwa kama sheria inavyotaka, lakini vingine akiviita vya
ovyo na sheria inayotungwa ni mbaya yenye malengo ya kuwakomoa baadhi ya
watu.
MWANANCHI
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Kanda ya Ziwa Magharibi, kimeanzisha operesheni maalumu kwa ajili ya
kusaka ubunge katika majimbo yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ambayo
yanashikiliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Operesheni hiyo inayojulikana kama ‘tigitigi’,
ilianza juzi kwa kutumia usafiri wa helikopta katika majimbo kadhaa,
ikiwamo Jimbo la Sengerema linaloshikiliwa na mbunge wa sasa, William Ngeleja.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Geita Alphonce Mawazo
ni miongoni mwa makada wa chama hicho waliofika katika jimbo la
Sengerema juzi, wakiambatana na kada wa chama hicho anayetaka kutangaza
nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo, Hamis Tabasamu.
Akihutubia kwenye mikutano ya hadhara iliyofanyika katika vijiji
tofauti kwa muda wa dakika 30 katika kila kijiji, Mawazo alisema
wameanzisha operesheni hiyo kwa lengo la kushinda ubunge kwenye majimbo
yote yaliyoko kwenye kanda hiyo ili kuleta ukombozi wa kweli kwa
wananchi.
“Wananchi naomba niwambie tumeanza
na Jimbo la Sengerema, tutapambana hadi hatua ya mwisho ili kulikomboa
jimbo hili. Tunataka Kanda ya Ziwa iwe ya mfano, tutazunguka kata zote
na vijiji vyote katika mikoa ya Geita, Simiyu, Mwanza, Tabora, Shinyanga
na Mara kuelimisha wananchi,” alisema Mawazo na kuongeza’
“Pia naomba wananchi mjitokeze
kujiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga kura ili tuweze kupata
nafasi ya kufanya mabadiliko ya kweli mwezi Oktoba. Ndugu zangu
mapambano yameanza hakuna kulala, huu ni wakati wetu Chadema,” alisema.
Naye mtangaza nia wa jimbo hilo, Hamis Tabasamu
ambaye aliwahi kuwa diwani wa Sengerema, alisema kuwa watafungua ofisi
78 za Chadema kwenye jimbo hilo ili wananchi waweze kuwa na sehemu za
kutoa malalamiko yao kwa viongozi na kuhudumiwa.
Alisema muda uliopo sasa ni wa kufanya
mabadiliko na kwamba kazi ya kutafuta ukombozi Sengerema imeanza, hivyo
ni jukumu la wananchi wa eneo kuunga mkono jitihada za chama hicho za
kuwaletea maendeleo endelevu.
MTANZANIA
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Taasisi ya Taaluma na Maendeleo, Dk. Stephen Maluka,
ametangaza nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Nyasa (Mbinga
Magharibi) mkoani Ruvuma kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Oktoba
mwaka huu.
Dk. Maluka mwenye Shahada ya Uzamivu ya
Afya ya Jamii aliyopata nchini Sweden, amejitosa kugombea jimbo hilo
ambalo awali lilijulikana kama Mbinga Magharibi na lilikuwa likiongozwa
na marehemu Kapteni John Komba ambaye alifariki mwanzoni mwa mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana Dk. Maluka
alisema lengo la kuingia katika kinyang’anyiro hicho ni kuwakomboa
wananchi wa jimbo hilo, ambao kwa sasa wana hali ngumu ambayo
ilichangiwa na usimamizi mbovu wa rasilimali na bajeti za Serikali.
Alisema upungufu uliopo katika jimbo
hilo ni wa kiuongozi na endapo kutatokea mtu atakayekuwa na usimamizi
mzuri katika masuala muhimu atakuwa na nafasi nzuri ya kubadilisha
maisha ya wananchi waliopo.
“Nalijua
Jimbo la Nyasa matatizo yote yanatokana na usimamizi mbovu wa viongozi
katika miradi ya Serikali na fedha za bajeti zinazotolewa kwa ajili ya
jimbo hilo.
Alisema endapo atapata nafasi hiyo
atasimamia kwa umakini mapato na matumizi ya jimbo ili kuhakikisha
yanamnufaisha kila mwananchi.
MTANZANIA
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro
linawashikilia watu saba wanaodaiwa kuwa ni wamiliki wa vituo vitatu
vilivyogundulika kuhifadhi watoto 147 kwa siri Katika Wilaya ya Hai,
mkoani Kilimanjaro.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Geofrey Kamwela, alitoa taarifa hiyo jana, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema kwamba, watu hao wanashikiliwa
kwa kosa la kulea watoto katika mazingira hatarishi na kusababisha
wengine wasiendelee na masomo kinyume cha sheria.
“Tunawashikilia watu saba ambao inasemekana ni wamiliki wa vituo hivyo kwa tuhuma za kuwahifadhi watoto kinyume cha sheria.
“Katika
Msikiti wa Bilal tumekamata watuhumiwa wawili, katika Msikiti wa
Othman tumekamata watuhumiwa wawili na katika Msikiti wa Kwa Kiriwe
Markes bin Kain, tumekamata watuhumiwa watatu,” Kamanda Kamwela.
Akifafanua zaidi, Kamanda Kamwela alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kuna mtandao wa walimu wengi wanaofundisha watoto hao.
Katika hatua nyingine, kamanda huyo wa
polisi, alitoa wito kwa wananchi mkoani hapa kushirikiana na Jeshi la
Polisi ili kufichua wahalifu, wakiwamo wanaolea watoto bila kufuata
utaratibu.
Watoto wa kiume wenye umri kati ya miaka
11 na 21 kutoka mikoa mbalimbali nchini walikutwa juzi wilayani Hai,
Mkoa wa Kilimanjaro, wakilelewa misikitini.
Kugundulika kwa watoto hao ni mwendelezo
wa matukio ya watoto kukamatwa mkoani hapa baada ya watoto wengine 30
kugunduliwa mwezi uliopita katika maeneo mawili tofauti.
Nitaendelea kukupatia kila stori inayonifikia mtu wangu, niko tayari kukutumia wakati wowote kupitia www.tangakumekucha.blogspot.com
No comments:
Post a Comment