Monday, April 6, 2015

WATOTO WANNE WAZALIWA MKESHA WA PASAKA, KITUIO CHA AFYA NGAMIANI



Tangakumekuchablog

Tanga, JUMLA ya watoto wanne wamezaliwa katika mkesha wa Sikukuu ya Pasaka katika kituo cha Afya Ngamiani Tanga  ikiwa ni pungufu ya idadi kama hiyo mwaka jana.

Akizungumza na waandishi wa habari, Muuguzi wa zamu kituo cha afya cha Ngamiani, Vestina Paul, alisema kati ya watoto hao wawili ni wa kike na wawili ni wakiume.

Alisema wazazi wote walijifungua salama na watoto wao wakiwa katika afya nzuri na kudai kuwa awali walitegemea idadi ya wajawazito kujifungua ingeongezeka na hivyo wauguzi walikuwa wamejipanga kupokea waliotaka kujifungua.

“Mara nyingi mikesha ya Sikukuu iwe ya Pasaka au Iddi kituo huwa kinaongeza nguvu zaidi ya kupokea wajawazito----hii ikiwa ni kuhakikisha wajawazito wanajifungua salama na kuweza kusherehekea sikukuu kama wengine” alisema Paul

“Jambo zuri ambalo hatukutegemea tumezalisha watoto wanne----hii ni idadi pungufu ya mwaka jana na ndio maana tulijipanga kwa kutegema kuongezeka” alisema

Wakati akizungumza na wazazi wa watoto hao, Muuguzi huyo aliwataka kuwa mabalozi wazuri katika maeneo yao kwa kutoa elimu ya wajawazito kuwa  na ada ya kutembelea vituo vya afya kujua mwenendo wa ujauzito wao.

Alisema kuna wajawazito wengi wamekuwa hawana ada ya kufika katika vituo vya afya  na badala yake wamekuwa wakienda wakati wanapojisikia uchungu na hivyo kuwa kero.

“Wajawazito wengi hawana elimu ya kutembelea vituo vya afya kujua mwenendo wa ujauzito wao----hii inapelekea mara nyingi mzazi kukumbana na changamoto wakati wa kujifungua” alisema Paul

Alitoa ushauri kwa wazazi hao kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri mitaani ikiwa na pamoja na kupiga vita mimba za utotoni pamoja na vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto.

                                                Mwisho

No comments:

Post a Comment