Tuesday, November 10, 2015

MITANDAO YA KIJAMII YAMFUKUZISHA KAZI ASKARI WA USALAMA BARABARANI, TANGA



Tangakumekuchablog
Tanga, JESHI la Polisi Mkoani Tanga, limemfukuza kazi askari kikosi cha Usalama Barabarani kituo cha Kabuku Wilayani Handeni Mkoani Tanga, Antony Temu (46) kwa tuhuma ya kuomba rushwa akiwa kazini.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 10 jioni kijiji cha Kitumbi Tarafa ya Mazingara Wilayani Handeni baada ya askari huyo kusimamisha gari kwa ukaguzi.
Alisema polisi ilipata taarifa kupitia mitandao ya kijamii na kuifanyia kazi na kubaini tukio hilo ni la kweli na kumtambua askari huyo ambaye kituo chake kilikuwa Kabuku barabara ya Segera Chalinze.
“Tulipokea picha kupitia mitandao ya kijamii ionyeshayo askari wetu aliekula kiapo akipokea pesa ambazo idadi yake hazijajulikana lakini zinaonekana noti za elfu kumi kumi” alisema Mombeji na kuongeza
“Askari huyu amelitia aibu jeshi la polisi na kwa kutumia sheria za kijeshi tumemfukuza kazi mara moja----hivi tunavyozungumza nanyi tumemkabidhisha kwa wenzetu wa kikosi cha kupambana na rushwa Takukuru” alisema
Kamanda Mombeji alitoa shukurani kwa watu walioibua uovu huo ambao haukuzingatia maadili na kuwataka wananchi kushirikiana na polisi katika kuwafichua watu wenye tabia kama hiyo.
Akizungumzia maadili, Kamanda Mombeji aliwataka askari polisi na wa usalama barabarani kuacha kulitia aibu jeshi hilo na badala yake wafanye kazi kwa kuzingatia maadili.
Alisema yoyote ambaye atabainika kulitia madoa jeshi la polisi atachukuliwa hatua kali za kijeshi ikiwemo kufukuzwa kazi na hivyo kuwataka kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
“Natoa agizo kwa askari yoyote ambaye atajishughulisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa hatutomvumilia---sheria zipo na zitachukua mkondo wake nah ii nataka iwe fundisho kwa wengine” alisema Mobeji
Alisema kufuatia tukio hilo jeshi la polisi litakuwa likiwafuatia polisi wa usalama barabarani pamoja na wengine ili kuhakikisha vitendo vya upokeaji na kuomba vinakomeshwa.
                                              Mwisho




  Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji, akizungumza na waandishi wa habari leo juu ya tukio la kufukuzwa kazi askari wa kituo cha polisi cha Kabuku Wilayani Handeni, Antony Temu  kwa kosa la kupekea  rushwa tukio lililoonekana katika mitandao ya kijamii na kwa sasa anahojiwa na kikosi cha Kupambana na Rushwa (Takukuru) Tanga.



No comments:

Post a Comment