Wednesday, November 11, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETINI LEO ,NOV 11 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Kituo kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na ufundi ukiwemo Umeme na Computer. Candle wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746


NIPASHE
Katibu wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi mkoani Kilimanjaro (UVCCM), Yasini Lema, ‘amefunguka’ kuhusu mchakato wa uchaguzi mkuu uliopita namna ulivyokiathiri chama hicho na kukifanya kipoteze majimbo ya uchaguzi ya Siha, Same Mashariki na Moshi Vijjini waliyokuwa wakiyashikilia kwa zaidi ya miaka 15.
Lema amedai kuangushwa kwa mawaziri wawili wa serikali iliyopita, Aggrey Mwanri aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Anne Kilango Malecela (Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi) na Dk. Cyril Chami, kulitokana na ushawishi mkubwa wa aliyekuwa mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa.
Lema aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Nipashe, kuhusiana na tathimini yao waliyoifanya Novemba 7, mwaka huu baada ya kupitia zoezi zima la uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema Lowassa ndiye aliyeisaidia Chadema kuwapokonya majimbo hayo kutokana na kuungwa mkono na wananchi wengi wakiwamo pia baadhi ya makada wa CCM ambao hawakufurahishwa na kitendo cha Kamati Kuu ya chama hicho kuliengua jina lake wakati wa mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho.
“Chadema imefanikiwa kuchukua majimbo ya CCM kutokana na mkakati wa Lowassa pamoja na kuhama kwake, kitu ambacho kilitengeneza mpasuko ulioiua CCM na wagombea wake,” alisema.
Alidai kulitokea usaliti ndani ya CCM kwa madai kulikuwa na kundi ambalo lilikuwa likiendelea kushiriki vikao vya ndani huku likikerwa na kuondoka kwa Lowassa jambo ambalo lilisababisha chama hicho kushindwa katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Aidha, akizungumzia mkakati wa CCM kuyarejesha mikononi mwake majimbo ya Moshi Mjini na Rombo, Lema alidai kuwa sababu ya kushindwa kwao ni  kutokana na wagombea wa nafasi za ubunge kupitia chama hicho kupora mamlaka ya viongozi wa wilaya.
“Wagombea ubunge katika majimbo haya mawili walikuwa na nguvu zaidi katika chama, atakalolisema yeye na atakalopanga ndilo atakalolisimamia lifanyike. Ukweli ni kwamba viongozi wa wilaya nao waliwaogopa, huku kampeni zao zikikwepa kabisa kuwashirikisha viongozi wa chama ngazi za matawi na kata” alisema Lema.
Alisema pamoja na kwamba CCM kilianzisha vikosi kazi maalum kwa ajili ya kutafuta kura, lakini katika hali ya kushangaza wagombea wao wa ubunge katika majimbo yote tisa ya Mkoa wa Kilimanjaro, walijiweka kando kuwatumia viongozi wa matawi na ngazi ya kata.
Sababu nyingine ya kupoteza viti vingi vya udiwani alisema ni wagombea wao kujiaminisha kwamba CCM ingewaletea fedha nyingi kwa ajili ya kampeni huku wengine wakiamini wangesaidiwa na wagombea ubunge ambao waliamini walikuwa na fedha nyingi kuwashinda wagombea wa vyama vya upinzani.
NIPASHE
Mwanamkakati wa aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bashir Awale, amekamatwa na kuwekwa ndani katika Kituo cha Polisi cha Kati.
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya timu ya kampeni ya mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, zinasema kuwa Awale alikamatwa juzi jioni kwenye maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Taarifa zaidi zinasema kuwa Awale alisimamamishwa na askari, ambao walimchukua kwenye gari lao huku wakilitelekeza gari lake kwenye maeneo hayo.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, aliliambia Nipashe atalizungumzia suala hilo leo pamoja na mambo mengine.
“Nimewaagiza vijana wangu waniandalie taarifa juu ya suala hilo. Nitalizungumzia jambo hilo kesho (leo) pamoja na mambo na mengine,” alieleza Kamishna Kova, ambaye hakutaka kuingia kwa undani wakati alipohojiwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba kukamatwa kwa Awale kunahusishwa na masuala ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni kutokana na ukaribu wake na Lowassa.
Lowassa alishindwa kwenye uchaguzi wa urais baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072, 848 sawa na asilimia 39.97 wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.
Awale alikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi kwenye timu ya kampeni ya Lowassa tangu wakati alipokuwa mwanachama wa CCM.
Lowassa alipoachana na CCM na kujiunga na Chadema, Julai 28 mwaka huu, Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana naye.
Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana Lowassa siku anatambulishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, baada ya kujiunga rasmi na chama hicho.
Kabla ya kuingia kwenye masuala ya siasa, Awale alikuwa Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Stanbic nchini Tanzania kabla ya kuachia ngazi mwaka 2013.

NIPASHE
Siku moja baada ya Rais Dk. John Magufuli, kufanya ziara ya kushtukiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, hali imebadilika ghafla ambapo huduma za matibabu zimeanza kutolewa haraka na kwa ufanisi.
Aidha, uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungumzo na kampuni ya Philips kutengeneza mashine mbili za CT-Scan na MRI za vipimo mbalimbali vya magonjwa.
Juzi, Rais Dk. Magufuli alivamia ghafla hospitalini hapo kisha kumuondoa aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Hussein Kidanto pamoja na kuivunja Bodi ya Hospitali baada ya kutoridhishwa na utendaji wao wa kazi.

Nafasi yake imechukuliwa na Profesa Lawrance Mseru, ambaye alianza kazi hiyo jana saa 4:00 kwa kufanya vikao na Menejimenti na Kamati Tendaji ya Hospitali.
Akizungumza na Nipashe, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Muhimbili, Aminiel Aligaesha, alisema uongozi wa hospitali hiyo umeanza kufanya mazungunzo na kampuni ya Philips kwa ajili ya kutenge
neza mashine zilizoharibika.
Alisema kazi hiyo itafanyika hivi karibuni baada ya wataalam wa kampuni hiyo kuwasili kwa kazi hiyo.
Alisema wana matumaini ya mashine hizo kufanya kazi kwa muda waliopewa na Rais Magufuli.
“Tutakamilisha kazi hii ndani ya kipindi tulichopewa, tunachofanya sasa ni kuzungumza na kampuni husika waje kuzitengeneza ili tuanze kutoa huduma haraka kwa wagonjwa,” alisema Aligaesha.
Akizungumzia Mkurugenzi mpya, Aligaesha alisema kwamba Profeza Mseru aliripoti jana saa 4:00 asubuhi na kuitisha vikao mbalimbali kwa ajili ya kujua utendaji kazi wa hospitali hiyo.
Alisema baada ya kukamilisha kazi ya kukutana na makundi mbalimbali ya wafanyakazi, atazungumza na vyombo vya habari kuelezea kazi yake hiyo mpya.
Gazeti hili liliwashuhudia madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine wa hospitali hiyo wakifanya kazi kwa kasi tofauti na siku za nyuma.
Wodi nyingi zilionekana kuwa na madaktari muda wote, kitu ambacho wagonjwa walieleza kwamba kimewafurahisha.
Hata hivyo, katika daftari la mahudhurio, imeelezwa madaktari bingwa kwa mara ya kwanza wamejihorodhesha mapema asubuhi.
“Ninachokuambia leo ni mchakamchaka kila mtu anawajibika, kwa mara ya kwanza madaktari bingwa wamesaini daftari la maudhurio,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Mgonjwa Chacha Makange, ambaye Rais Magufuli aliagiza apatiwe matibabu pamoja na vipimo, alisema ndani ya dakika sita zimebadilisha maisha yake na wagonjwa wengine.
Chacha ambaye anafahamika kutokana na kuishi ndani ya handaki kwa miaka mitano maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema jana alipatiwa vipimo katika kituo binafsi cha kupimia magonjwa cha Besta kilichopo Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Alisema anamshukuru Mungu kumkutanisha na Rais Magufuli na kusababisha maisha yake kubadilika ghafla.

Chacha alisema alipomuona Dk. Magufuli, alimuomba aongee naye dakika tano, lakini Rais alimpa dakika moja ya kuzungumza.
MWANANCHI
Bibi harusi Doroth Msuya aliyetoroka saluni akipambwa saa tatu kabla ya kufungwa kwa harusi yao na kumwacha solemba bwana harusi, Joseph Machange amepatikana jijini Arusha.
Polisi mkoani Kilimanjaro imesema binti huyo hakutekwa nyara kama ambavyo wanafamilia walitoa taarifa Kituo cha Polisi Himo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Fulgence Ngonyani alisema jana kuwa uchunguzi uliofanywa umethibitisha kuwa bibi harusi huyo hakuwa ametekwa nyara.
“Polisi walifungua jalada la uchunguzi na ilibainika kuwa taarifa za kutekwa zilizokuwa zimetolewa hazikuwa na ukweli, bali aliondoka kwa kupanda pikipiki,” alisema.
Kamanda Ngonyani alisema uchunguzi huo ulibaini kuwa wakati akipambwa, aliomba kwenda kujisaidia na baadaye kuomba apelekewe kanga na ‘tishu’ lakini akatumia mwanya huo kuondoka,” alisema. Alisema uchunguzi huo umebaini kuwa baada ya kupanda pikipiki ilimpeleka hadi kituo cha mabasi na alimlipa dereva wa bodaboda kisha alipanda gari la abiria lililompeleka hadi mjini Moshi.
Tukio hilo lilitokea Jumamosi iliyopita saa 6.30 mchana eneo la Lole huko Mwika, Moshi wakati bibi harusi huyo alipotoroka saluni akimwacha mpambe wake akiendelea kupambwa. Ndoa hiyo ilikuwa ifungwe saa tisa alasiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Lole Dayosisi ya Kaskazini na baadaye sherehe ingefanyika katika Ukumbi wa Mamba Complex.
Habari zilizopatikana jana kutoka kwa familia ya Machange, zilieleza kuwa Doroth alipatikana juzi baada ya kuonekana akiweweseka, kisha akapelekwa hospitali ya Seliani kwa matibabu. Ndugu wa karibu wa familia ya Machange ambaye aliomba jina lake lisitajwe, alisema kulikuwa na kikao kilichokuwa kikiendelea kati ya familia ya Machange na Msuya.
“Jana (juzi) tulipigiwa simu na kuelezwa kuwa Doroth amepatikana Arusha lakini yuko kama hajielewielewi na hajui nini kimetokea,” alisema. Habari zaidi kutoka ndani ya familia hiyo, zinadai kuwa bibi harusi huyo alikuwa ametaka harusi hiyo iahirishwe na ombi hilo alilitoa zaidi ya mara 10 bila kueleza sababu.
MWANANCHI
Jeshi la Polisi mkoani Katavi limefanikiwa kuzuia kufungwa kwa ndoa iliyohusisha watoto, muolewaji akiwa na umri wa miaka 14 na muoaji ana umri wa miaka 17.
Kwa mujibu wa taarifa, bibi harusi ni mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwamkulu iliyopo kijiji cha Senta John Mwamkulu, Wilayani Mpanda, mkoani Katavi, na bwana harusi aliacha shule alipokuwa darasa la tatu. Mwanafunzi huyo (14), siku ya harusi alikuwa afanye mtihani wa wilaya, lakini alikutwa akiwa amevaa shela tayari kwa kufungishwa ndoa ya kimila nyumbani kwao kwa mahari ya ng’ombe kumi na moja.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo lilitokea juzi saa saba mchana katika kijiji Senta John Mwamkulu, wilaya ya Mpanda.
Alisema polisi wakiwa na viongozi wa elimu wa Manispaa ya Mpanda, walienda nyumbani kwao na kukuta msichana huyo akiwa na shela tayari kufungishwa ndoa kinyume cha sheria.
Alisema jeshi hilo linamshikilia bwana harusi (jina linahifadhiwa), baba yake bwana harusi Ntunga Mkubaneja (40) na Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mwankulu, Raphel Kweka, anayedaiwa kupewa Sh500,000 ili afute jina la mwanafunzi huyo shuleni.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Kidavashari alisema wakati mchakato wa kufungwa kwa ndoa hiyo ukiendelea, mkazi wa kijiji hicho alifunga safari mpaka ofisini kwake na kutoa taarifa juu ya kuwepo kwa ndoa hiyo kinyume cha sheria.
“Tulipewa taarifa kuwa kuna mwanafunzi anaozeshwa kinyume cha sheria na harusi yake inafungwa mchana wa tarehe tisa, mwezi huu.
Tulijiandaa tukakubaliana na watu wa elimu kisha tukaenda kijijini na kukutana na shamra shamra za kumuozesha mwanafunzi kama tulivyoambiwa,”alisema.
Ofisa Elimu wa Manispaa ya Mpanda, Vincent Kayombo alisema mwanafunzi huyo alikuwa darasa la nne na kuwa siku ya harusi yake alitakiwa kufanya mtihani wa wilaya (Mock)
HABARILEO
Jeshi la Polisi mkoani Tanga limemfukuza kazi kwa kosa la fedheha aliyekuwa askari wake katika Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo Anthony Temu (46) wa Kituo cha Polisi Kabuku wilayani Handeni.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, kufukuzwa kwa askari huyo kumetokana na taarifa ya kuomba na kupokea rushwa iliyopatikana kupitia mitandao ya kijamii.
Alisema Novemba 9, mwaka huu saa 7.30 mchana kupitia mitandao ya kijamii, alionekana askari mmoja wa kikosi cha usalama barabarani akipokea rushwa kutoka kwa dereva wa gari alilokuwa amelisimamisha kutokana na makosa ya usalama barabarani.
Alisema; “Katika ufuatiliaji ilibainika kwamba eneo la tukio ni katika kijiji na kata ya Kitumbi iliyopo wilayani Handeni Mkoa wa Tanga katika Barabara Kuu ya Segera- Chalinze … askari aliyebainika kutenda kosa hilo ni F. 785 Anthony Temu na kutokana na uzito wa kosa lenyewe alichukuliwa hatua za haraka za kinidhamu.
“Amekamatwa na tayari mashitaka ya kijeshi yameendeshwa dhidi yake na kutiwa hatiani ambapo amepewa adhabu ya kufukuzwa kazi kwa fedheha … hivi ninavyoongea nanyi hapa ameshafukuzwa kazi si askari tena tangu jana (juzi) jioni.”
Alisisitiza mtuhumiwa huyo ameshakabidhiwa kwa maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) pamoja na kielelezo ambacho ni video iliyokuwa ikirushwa kwenye mitandao ya kijamii ili waendelee kumshughulikia kwa upande wa jinai katika makosa ya kuomba na kupokea rushwa.
Hata hivyo, alisema Polisi mkoani Tanga inawashukuru wananchi hao walioibua taarifa hizo na kuwataka kuliarifu kuhusu matukio yoyote yanayohusisha ukiukwaji wa maadili katika jeshi hilo.
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment