Tuesday, November 17, 2015

WATATU WANASWA WAKISAFIRISHA MIHADARATI KILO 530 TANGA



Tangakumekuchablog
Tanga, JESHI la polisi Mkoani Tanga linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuingiza nchini madawa ya kulevya aina ya mirungi kilo 530 yakitokea Mombasa nchini Kenya kwa kutumia kampuni ya usafirishaji abiria (Smart Bus).
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji, alisema kukamatwa kwa watu hao ni taarifa za wasamaria wema kuliambia jeshi la polisi juu ya kuingiza madawa hayo.
Aliwataja watu hao kuwa ni, Mohammed Omary (32), Haruna Hassan (35) na Aziz Othman (27) wote wakiwa wenyeji wa Tanga na kusema kuwa taarifa za wasamaria wema zilifanikiwa kuwakamata.
“Taarifa za wasamaria wema kwa kushirikiana na jeshi la polisi tuliweza kuikamata mirungi ikiwa imefichwa uvungu wa basi juu ya vyuma----ni vigumu kugundua mara moja” alisema Mombeji na kuongeza
“Hawa vijana ni hatari sana wameficha mirungi kilo mia tano na thalathini----ni mingi sana ila tumeikamata na watuhumiwa tutawakomesha na kuwa funzo kwa wengine” alisema
Alisema watuhumiwa hao wanahojiwa na polisi na mara baada ya kukamilika kwa ushahidi watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili na kuwa mfano kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
Akizungumza kuhusu usalama wa mipaka, kamanda Mombeji alisema kwa sasa wamezidisha doriia katika mpaka wake na nchi jirani kuzuia mianya ya upitishaji wa wahamiaji haramu na mali za magendo.
Alisema awali wahalifu walikuwa wakiitumia mipaka hiyo kwa kupitisha wahamiaji haramu kutoka Ethopia na Somalia pamoja na mali za magendo lakini kwa sasa wamezidisha ulinzi maradufu.
“Tumezidisha ulinzi katika mipaka yetu kuzuia upitishaji wa wahamiaji haramu na mali za magendo----wahalifu walikuwa wakiitumia vibaya  na sasa tutakula sahani moja” alisema kamanda Mombeji
Aliwataka wananchi kushirikiana na jeshi hilo kwa kupeana taarifa za matukio mara kwa mara na kuacha kushirikiana  na wahalifu kwani wataweza kuwaingiza katika matatizo ambayo hawana matarajio nayo
                                               Mwisho

  Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji akiwaonyesha waandishi wa habari na maofisa polisi mirungi kilo 530 iliyokamatwa katika basi la abiria lililokuwa likitokea Mombasa nchini Kenye .


Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji akiwaonyesha watuhumiwa wa kuingiza mirungi kilo 530 kutoka Mombasa Kenya kwa waandishi wa habari wa Tanga jana nje ya Ofisi yake. Chini ni viroba vya mirungi vikiwa vimetawanywa

No comments:

Post a Comment