Friday, November 27, 2015

POLISI TANGA YAWATIA MBARONI WAHABESHI 34 KWA KUINGIA NCHINI BILA KIBALI

Tangakumekuchablog

Tanga POLISI Mkoani Tanga imewakamata wahamiaji haramu 34 wenye asili ya Kiethopia wakiwa wamefichwa kwenye Lori lililokuwa limebeba maji ya chupa ya Kilimanyaro wakisafirishwa kuelekea Tunduma  Mkoani Mbeya.

Akizungumza na waandishi wa habari , Kamanda wa polisi Mkoani Tanga, Zuberi Mombeji, alisema tukio hilo lilitokea juzi saa 8 usiku kwenye kizuizi cha polisi cha Mazinde kata ya Kisiga Wilayani Korogwe Tanga.

Alisema polisi wakati wakilikagua gari hilo ambalo lilikuwa limesheheni katoni za maji katikati ya tela kulikuwa na uwazi ambao ulitandikwa majamvi na magunia jambo ambalo amedai kuwa si rahisi kugundua.

Alisema lori hilo ambalo lilikuwa likielekea Tunduma Mkoani Mbeya lilikuwa limejaza maji na kuwa vigumu kuwatatambua na wakati wa ukaguzi wa gari walisikia sauti za watu wakizungumza na kukohowa.

“Wakati wa upekuzi wa lile lori lilikuwa limesheheni katoni za maji aina ya Kilimanjaro----dereva alishuka kwa kasi na kutokomea porini na kushindwa kumkamata” alisema Mombeji na kuongeza

“Haikuwa rahisi kuwagundua kwani gari lilikuwa limesheheni katuni za maji hadi juu ----kilichosaidia wakati polisi akiichunguza mipira sauti zilisikika ndipo alopopanda juu na kuona kundi la watu” alisema

Alisema wakati wa mahojiano dereva alikimbia mbio  na kubaki utingo peke yake ambapo kwa sasa anashikiliwa na polisi pamoja gari na mara baada ya uchunguzi kukamilika atapelekwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Katika tukio jengine, Kamanda Mombeji aliwaambia wanahabari kuwa polisi Kabuku  inamshikilia , Salim Mgazi mkazi wa Usagara kwa tuhuma za kukutwa na mirungi kilo 12 ambayo alikuwa ameificha katika begi lake lililokuwa na nguo.

Alisema tukio hilo lilitokea juzi saa  11 jioni katika kizuizi cha polisi cha Kabuku barabara Segera Chalinze kwenye basi la Tahmeed ambalo lilikuwa linatokea Mombasa kwenda Dar es Salaam.

Alisema polisi wakati wa ukaguzi wake wa gari na mizigo ndani ya buti na ndani ya gari ilifanikiwa kukuta mirungi iliyofichwa katika begi la nguo ambayo ilikuwa izungushiwa mfuko wa nailoni.

“Polisi wakati akikagua mizigo ndani ya buti na ndani ya gari ilifanikiwa kuikuta mirungi kilo kumi na mbili katika begi la abiria” alisema Mombeji

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano na jeshi la  polisi katika kutokomeza matukio ya kihalifu pamoja na upitishaji wa wahamiaji haramu na mali za magendo ambapo amedai kuwa kuna baadhi ya wakazi wa mpakani wamekuwa wakishirikiana na wahalifu.

                                            Mwisho

No comments:

Post a Comment