Tuesday, November 17, 2015

SOMA HABARI KUBWA ZILIZOPEWA UZITO MAGAZETI YA LEO NOV 17 TZ

Uchambuzi huu wa magazeti unaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya kituo cha Elimu Cha Candle Education Centre Tanga, kituo kinaongoza kufaulisha wanafunzi kidato cha pili hadi cha sita na wanaojiendeleza kielimu, Kituo pia kinatoa kozi mbalimbali za kielimu na ufundi ukiwemo Umeme na Computer na pia wako na huduma ya Hostel, Wapo Tanga mkabala na Bank ya CRDB simu 0715 772746
HABARILEO
Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) umesimamisha kwa muda huduma za uchunguzi kupitia mashine ya MRI kuanzia mwishoni mwa wiki, kwa ajili ya matengenezo zaidi ya mashine hiyo.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma na Huduma kwa Wateja cha MNH, Aminiel Aligaesha aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa matengenezo zaidi ya mashine ya MRI yatakwenda sambamba na matengenezo ya mashine ya CT-Scan.
“Mtakumbuka kwamba mapema wiki iliyopita tuliwatangazia wananchi kwamba huduma za MRI zimeanza kutolewa baada ya mashine hiyo kutengenezwa na kuanza kufanya kazi. “Katika taarifa yetu tuliwaeleza pia wananchi kuwa mashine ya CTScan ilikuwa inaendelea kufanyiwa matengenezo ili nayo ianze kutoa huduma kwa wagonjwa.
Hata hivyo, mashine ya MRI baada ya kufanya kazi Novemba 11 na 12, 2015 ilionekana kuwa na hitilafu ya kiufundi ambayo inahitaji matengenezo zaidi hali inayotulazimu kuisimamisha kufanya kazi,” alisema Aligaesha.
Kuhusu jitihada zilizofanyika, alisema uongozi wa hospitali umewasiliana na Kampuni ya Philips a
mbayo ina mkataba wa kufanya matengenezo ya mashine za MRI na CT- Scan ili kurekebisha hitilafu hizo.
“Baada ya uchunguzi wa kina mafundi wamegundua hitilafu kwenye mashine ya MRI ambapo kifaa kimoja kinachoitwa RF Amplifier kimeharibika na inabidi kiwekwe kingine. Kifaa hiki kazi yake ni kuipatia mashine hiyo mawimbi ya sauti ambayo yanahitajika katika sehemu nyingine za mashine kuiwezesha kufanya kazi yake vizuri,” alifafanua.
Kuhusu mashine ya CT- Scan, alisema uchunguzi wa mafundi umeonesha ina hitilafu kwenye vifaa viwili; Image re-constructor (server), kifaa kinachohusika kutengeneza picha na kingine kiitwacho Inverter Power Supply kinachohusika na kupeleka umeme wenye kiwango kinachohitajika kwenye mashine.
“Vifaa vyote hivi havipatikani nchini na vimeagizwa kwa hati ya dharura nchini Uholanzi kwa mtengenezaji wa mashine hizi ambaye ni Philips na vinatarajiwa kuwasili nchini ndani ya wiki hii. Tunaomba wateja wetu wawe watulivu wakati huu ambapo tunashughulikia suala hili,” alisema Aligaesha.
Hatua hiyo ya MNH kusimamisha MRI imekuja siku chache baada ya kifaa hicho kutengenezwa baada ya Rais Dk John Magufuli kufanya ziara ya kushitukiza hospitalini hapo. Moja ya mambo aliyoelezwa ni kusimama kwa huduma za MRI na CT-scan kwa miezi miwili, jambo lililomfanya aagize ndani ya wiki moja mashine hizo zifanye kazi.
MTANZANIA
Wachimbaji wadogo watano katika mgodi wa Nyangarata, Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga,  wameokolewa baada ya kufukiwa na kifusi cha udongo ardhini kwa siku 41.
Wakizungumza katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ambako wamelazwa kwa matibabu jana, wachimbaji hao walisema waliishi siku zote hizo kwa kula wadudu kama mende na mizizi mbalimbali.
Kwa mujibu wa wachimbaji hao, walikuwa wakitumia kofia zao kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu kwa ajili ya kunywa.
Inaelezwa kuwa wachimbaji hao walifukiwa Oktoba 5, mwaka huu saa 5.00 asubuhi wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji chini ya ardhi.
Watu walioshuhudia tukio hilo, walisema ardhi ya juu ya machimbo hayo ilititia na kuporomoka kutokana na mvua iliyonyesha, na hivyo kuwafunika wachimbaji hao.
Wakati huo jitihada za uokoaji zilifanikisha kuokolewa wachimbaji sita wakati wengine hawakuweza kufikiwa, ikizingatiwa pia kuwa zilikosekana taarifa sahihi za idadi yao na eneo halisi walikokuwa wamefukiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema wachimbaji hao waliokolewa baada ya kugunduliwa na wazamiaji walioingia kwenye mashimo hayo kwa lengo la kuiba mchanga.
Alisema wachimbaji hao walisikia watu wakiomba msaada katika mashimo hayo.
“Baada ya wachimbaji hao kusikia sauti, waliwasiliana na wenzao na kuanzisha jitihada za kuwaokoa,” alisema.
Kamanda Kamugisha alisema hatimaye waliweza kuwatoa katika mashimo hayo juzi wakiwa wamekaa kwa siku 41 tangu Oktoba 5, mwaka huu.
Aliwataja waliookolewa kuwa ni Chacha Wambura, Amos Muhangwa, Joseph Burulwa, Msafiri Gerald na Wonyiwa Moris.
Alisema mchimbaji mmoja, Musa Spana, alikufa siku chache baada ya kufukiwa na kifusi kwa kukosa chakula.
Mmoja wa wachimbaji hao, Wambura, alisema awali walifukiwa sita, lakini bahati mbaya mwenzao Spana alifariki dunia siku chache baadaye baada ya kukataa kula mizizi.
Alisema hatua hiyo ilisababisha akumbwe na ugonjwa wa kuhara uliosababisha kifo chake.
“Tulikuwa tukitumia miti inayojengea kingo za mashimo kama chakula pamoja na wadudu wadogo wadogo ndani ya  mashimo hayo, hasa mende.
“Pia tulikuwa tukitumia kofia zetu ngumu (helmet) kukinga maji yaliyokuwa yakitiririka kutoka juu ya ardhi ingawa yalikuwa ni machafu.
“Mwenzetu Musa alifariki dunia baada ya kukataa kutumia vitu hivyo,” alisema Wambura.
Akizungumzia tukio hilo, Naibu Kamishna wa Madini, Ali Samaje, aliwataka wachimbaji wadogo kuimarisha migodi  yao huku wakizingatia masuala ya usalama zaidi.
Samaje alisema hatua hiyo itawafanya kufanya kazi zao kwa uhakika na kuepukana na ajali kama hizo.
Pia aliwataka kuacha kuchimba madini kwa ajili ya kuuza tu, bali wajaribu kusaidiana katika mambo mbalimbali   wanapokuwa na matatizo.
Alitoa ushauri huo kwa kuzingatia kuwa shughuli zao  wanaziendesha katika maeneo ambayo hayako salama.
Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, alisema ameshtushwa na tukio hilo la wachimbaji hao kukaa kwa muda huo shimoni.
Alisema tukio hilo linaweza kuwa ni maajabu ya nane ya dunia.
Dk. Ngowi alisema kwa sasa waathirika hao wanapatiwa matibabu ya saikolojia pamoja na lishe maalumu kuhakikisha  wanarudi katika hali zao za kawaida kwa muda usiopungua siku saba.
“Waathirika hao tunao katika hospitali yetu katika kitengo cha lishe…Kwa sasa hawaoni hadi zipite siku saba kwa sababu walikaa gizani muda mrefu.“Pia tunawapatia matibabu ya saikolojia kuhakikisha wanakuwa sawa na afya ya akili,” alisema.
MTANZANIA
Huku ikiwa bado haijaanza kutumika, barabara ya Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi (Dart), imeanza kuwekwa viraka, hali ambayo imesababisha msongamano wa magari katika barabara za Morogoro, Mandela na Samnujoma, jijini Dar es Salaam.
Viraka hivyo vimeanza kuwekwa kwenye barabara hiyo eneo la Ubungo  ambalo linaunganisha barabara hizo zilizokumbwa na misururu mirefu ya magari jana.
Mradi huo ulitakiwa kukabidhiwa tangu Oktoba mwaka huu  ili mabasi hayo yaweze kuanza kazi.
Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dart, Asteria Mlambo, alisema ukarabati huo umekuja kutokana na dosari zilizojitokeza katika eneo hilo.
“Katika eneo la Ubungo karibu na maungio ya barabara za Morogoro, Mandela na Samnujoma, kuna dosari ndogo ndogo ambazo zinapaswa kufanyiwa marekebisho kabla ya kuanza kwa mradi huo.
“Kuna baadhi ya maeneo mafundi wanaendelea na ukarabati wa miundombinu iliyoharibika kutokana na dosari ndogondogo zilizojitokeza, hivyo tuwaache wafanye kazi ili waweze kumaliza kwa wakati,”alisema Mlambo.
Aliongeza, awali walishatoa taarifa katika vyombo vya habari juu ya marekebisho hayo na kuwaomba wananchi waache kuuliza maswali ili waweze kuendelea na shughuli zao.
“Tulishatoa maelezo kwenye vyombo vya habari juu ya kinachoendelea kwenye mradi huu, lakini kila siku mnarudi na kuuliza jambo hilo hilo.
“Ninawaomba mtuache tufanye kazi kwa sababu mradi wenyewe haujakabidhiwa, tuna haki ya kuangalia dosari na kuzifanyia marekebisho kabla ya kuukabidhi,” alisema.

NIPASHE
Mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge la 11, Job Ndugai, amejitabiria magumu katika Bunge hilo kwa kueleza kuwa litakuwa ni lenye changamoto nyingi ambazo atahakikisha anazimudu.
Kadhalika, ameweka bayana magumu ya Bunge hilo kuwa ni uwapo wa wabunge wengi wa upinzani, wabunge wasomi kuliko mabunge yaliyopita na kwamba kuna uwezekano wa kuwa na migomo ya hapa na pale.
Akizungumza na waandishi wa habari, baada ya kutangazwa kupewa idhini na Chama Cha Mapinduzi kupeperusha bendera yake katika uchaguzi wa Spika, alisema anatambua kuwa Bunge hilo litakuwa ni lenye mabadiliko makubwa tofauti na mabunge yaliyopita.
“Kuna ongezeko la vijana, wapinzani na wabunge wengi ni wasomi tofauti na mabunge yaliyopita, hivyo uendeshaji wake ni lazima ubadilike. Natambua changamoto nyingi zilizopo mbele tutarajie migomo mingi, lakini tutegemee Bunge lenye kuishauri na kusimamia serikali,” alisema.
Ndugai ambaye pia ni Mbunge Mteule wa Kogwa, alisema Bunge lijalo atalisimamia lifanye kazi kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuwa hakikisha wanawatumikia Watanznaia.
“Nitatenda haki kwa Wabunge wote, nitasimamia haki kwa vyama vyote, hakuna ambaye hatapata haki mbele ya kiti cha Spika, nawaomba wote waniunge mkono na wanipe kura nyingi za ushindi ili imani yangu kwao izidi,” alisema.
Alieleza kuwa alipokuwa Naibu Spika alifanya kazi kwa haki na kwa sasa atahakikisha kila mbunge anapewa kipaumbele cha fursa ya kuhakikisha anatoa hoja yake.
Ndugai alisema kaulimbiu yake atakayoisimamia ni ‘Sasa Kazi tu’ inayotimiwa na Rais John Magufuli, na kwamba Bunge lijalo litakidhi matarajio ya Watanzania.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, akizungumza na waandishi wa habari, alisema wabunge wateule kwa kauli moja walipitisha jina la Ndugai, baada ya wagombea wenzake kujitoa.
“Tulivyoanza kikao tu wagombea Dk. Tulia Ackson na Abdallah Ali Mwinyi, walitangaza kujitoa na kumuachia Ndugai, wabunge wateuele kwa kauli moja walimpitisha na kuonyesha kuwa ameshinda kwa asilimia 74.8,” alisema na kuongeza:
“Tunaamini huyu ndiye Spika kwa kuwa Bunge la 11 wabunge wa CCM ni asilimia 74.8, hivyo moja kwa moja huyu ndiye mshindi…sifa za Ndugai zinatosha kumpa ushindi, hakuna mgombea aliyeonyesha kazi zake kwa vitendo kama huyu.”
Alisema wagombea wenzake walijitoa baada ya kueleza kuwa wanaamini uwezo wa Ndugai hawalingani nao, hivyo wakamuachia nafasi hiyo.
Nape alisema jina hilo litapelekwa kwa uongozi wa Bunge kwa ajili ya kumshindanisha leo na wagombeawa vyama vingine.
NIPASHE
Upande wa Jamhuri katika kesi inayomkabili mwanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Tanzania (DIT), Benedict Ngonyani, anayetuhumiwa kusambaza taarifa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali, Davis Mwamunyange, amelishwa sumu, umewasilisha mahakamani kusudio la kukata rufaa kupinga mshtakiwa huyo kupewa dhamana.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, iliyoketi chini ya Hakimu Mkazi Mkuu, Respicious Mwijage, ilitengua hati ya kuzuia dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo iliyowasilishwa na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP).
Kabla ya uamuzi huo, hakimu alisikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili na alikubaliana na maombi ya utetezi ya kumpa dhamana kwa kuwa sababu za DPP kuzuia dhamana hiyo hazikuwa na msingi wa kisheria. Wakili wa Serikali Mkuu, Theophil Mutakyawa aliwasilisha kusudio hilo jana saa 7:00 mchana, kwamba upande wa Jamhuri haujaridhika na uamuzi wa mahakama kutengua hati ya DPP.
Pia, kupitia kusudio hilo, upande wa Jamhuri unapinga Mahakama ya Kisutu kutengua hati hiyo na kwamba haina mamlaka ya kuoindoa kwa kuwa huondolewa na DPP ama kesi inapomalizika na kutolewa hukumu. Awali hakimu alisema mshtakiwa ni mwanafunzi na shtaka analoshtakiwa nalo linadhaminika kwa hiyo haoni haja ya kukosa masomo yake ya darasani.
Katika kesi hiyo, inadaiwa Septemba 25, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa alisambaza taarifa za uongo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu cha 16 ya mwaka 2015 kuwa Jenerali Mwamunyange amenyweshwa sumu.
MWANANCHI
Wakati wanafunzi wa kidato cha pili wakianza mitihani jana, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza kwamba wanafunzi watakaofeli mtihani huo hawatorudia darasa, bali wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya jioni ili kuwawezesha kitaaluma.
Utaratibu huo mpya uliotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde, unafuta rasmi utaratibu wa awali ambao Serikali iliwataka wanafunzi wanaofeli mtihani huo kukariri darasa wakishindwa kufikisha wastani wa alama 30.
Dk Msonde alisema utaratibu huo mpya utawahusu pia wanafunzi wa darasa la nne ambao nao hawatalazimika kurudia darasa, bali watakuwa na muda wao wa ziada wa kusoma.
“Lengo la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya ufundishaji.
Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na siyo kuwarudisha darasa tu,” alisema.
Akizungumzia mtihani huo ulioanza jana, alisema watahiniwa 397,250 walisajiliwa nchi nzima, wakiwamo wanafunzi 67 wasioona na 224 wenye uoni hafifu. Mwaka 2008, Serikali ilifuta makali ya mtihani wa kidato cha pili, hali iliyotoa fursa kwa wanafunzi wengi hata wasio na uwezo kuingia kidato cha tatu na hatimaye kupata nafasi ya kufanya mtihani wa mwisho wa kidato cha nne.
Baada ya matokeo mabaya yaliyotokana na uamuzi huo na pia kelele za wadau wa elimu na jamii kwa jumla, hatimaye mwaka 2012, Serikali iliurudisha mtihani huo na kutangaza kuwa wanaofeli watakariri darasa, utaratibu ambao sasa umefutwa.
Maoni ya wadau Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo nchini (Tamongsco), Benjamin Nkonya alisema kuzuia wanafunzi wasikariri darasa ni kuwaondolea ari na hamasa ya kusoma kwa bidii, jambo ambalo ni hatari kwa maendeleo ya elimu nchini.
Alisema ili mwanafunzi asome kwa bidii lazima ajue kwamba akifeli ataondolewa kwenye mfumo rasmi wa elimu. Aliongeza kuwa Taifa litakuwa na watu wengi waliokwenda shule lakini hawana uwezo kwenye soko la ajira.
“Huu ni msumari wa mwisho kwenye jeneza la elimu. Serikali ikizuia wanafunzi kurudia darasa, elimu itaporomoka kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita na shule za binafsi zitakuwa kwa kasi,” alisema na kuongeza: “Hiyo elimu wanayosema ya bure itakuwa hamna kitu.
Mwanafunzi akija kwenye shule zetu za binafsi na kushindwa kufikisha wastani tunamfukuza.
Tunataka watu ambao wanasoma na kujua kwamba wakicheza wataondoka.’’ Meneja Mipango na Utafiti wa shirika la HakiElimu, Godfrey Boniventure alisema masomo ya jioni siyo suluhisho la kuzuia kiwango cha wanafunzi kufeli.
Alisema Serikali inapaswa kujua sababu inayochangia wanafunzi kufeli na kisha kutengeneza njia mbadala za kuwasaidia.
“Tatizo ni kwamba Serikali siku zote inaogopa neno kufeli, ndiyo maana wanafanya mabadiliko mengi ambayo hayana tija ili tu kuondoa neno kufeli. Remedial classes (masomo ya ziada) siyo njia mbadala ya kuzuia kufeli kwa wanafunzi,” alisem
MWANANCHI
Dk Tulia Ackson huenda akawa mmoja wa Watanzania wachache wenye bahati ya kupata vyeo tofauti vya juu nchini ndani ya siku 67. Katika kipindi hicho kifupi, Dk Tulia amepata fursa ya kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuteuliwa na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete Septemba 9, mwaka huu.
Cheo hicho amekitumikia kwa takriban miezi miwili akifanya kazi ya kuitetea na kushughulikia masuala ya kisheria yanayoihusu Serikali katika masuala mbalimbali, ikiwamo ya kuongoza jopo la mawakili wa Serikali katika kesi iliyovuta hisia za wengi ya kuomba tafsiri ya mahakama juu ya kifungu namba 104(1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343 iliyorejewa mwaka 2010.
Kesi hiyo ya kikatiba maarufu kwa jina la “kesi ya mita 200” ilifunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na mpigakura Amy Kibatala na baadaye Serikali ilishinda kutokana na Mahakama kuzuia watu kufanya mikusanyiko wala kukaa mita 200 baada ya kupiga kura.
Wakati wengi wakitafakari ushindi wa Serikali kuhusu kesi hiyo iliyoendeshwa ndani ya wiki ya mwisho kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, Dk Tulia aliamua kusaka nafasi nyingine ya juu ya muhimili mwingine wa dola ya uspika wa Bunge kupitia CCM. Novemba 13, alichukua fomu ya kuwania nafasi hiyo na siku mbili baadaye aliteuliwa na Kamati Kuu ya chama hicho akiingia kwenye ‘tatu bora’ akiwa na makada wenzake Job Ndugai na Abdulla Mwinyi.
Wakati akiwa na fursa ya uwezekano wa kuteuliwa na wabunge wa CCM kuwa mgombea wa uspika, jana asubuhi aliteuliwa na Rais John Magufuli kuwa mbunge akiwa wa kwanza kati ya nafasi 10 alizonazo Rais kikatiba. Uteuzi huo ulisababisha Rais atengue rasmi cheo cha Naibu Mwanasheria Mkuu alichokuwa akikishikilia.
Ndani ya saa chache za kuwa mbunge, Dk Tulia ambaye aliwahi kuwa mhadhiri wa sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, alijiengua kugombea uspika pamoja na Mwinyi na kumwachia Naibu Spika wa zamani, Ndugai.
Kujitoa kwa Dk Tulia hakukuwa mwisho wa safari ya kuwania cheo cha juu ndani ya Bunge na badala yake alikwenda kuchukua fomu ya kuwania unaibu spika kupitia chama hicho.
Kwa mantiki hiyo, iwapo wabunge wa CCM watampitisha kuwa mgombea wao wa nafasi ya naibu spika, hapana shaka kuwa ndiye mwenye nafasi kubwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la 11 kutokana na chama hicho kuwa na wabunge 252 kati ya 394 wa Bunge hilo.
Kitendo cha Dk Tulia kujitosa kugombea nafasi ya spika wa Bunge na hatimaye naibu spika kama kada wa CCM akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kimezua maoni tofauti miongoni mwa wachambuzi wa siasa na sheria, wengi wakieleza kuwa ni mbinu za CCM kujijenga ndani ya mihimili ya dola ambayo ni Mahakama, Bunge na Serikali.
Wachambuzi hao walisema tafsiri ya taswira iliyoonyeshwa na mwanasheria huyo imeendelea kudhihirisha kwamba, kila unapofanyika uteuzi wa majaji au wanasheria wa Serikali lazima ulenge kulinda masilahi ya chama kilichopo madarakani.
Profesa Mohamed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema kikatiba suala la kugombea uspika linatoa nafasi kwa kila Mtanzania mwenye sifa na siyo lazima awe kada wa chama cha siasa.
“Kwa hivyo inawezekana Mwanasheria Mkuu wa Serikali akagombea nafasi hiyo na asiwe anatokana na chama tawala,” alisema. Hata hivyo, alifafanua kwamba watumishi wanaopewa nafasi za juu za mihimili hiyo ya dola hutazamwa kwa jicho la kulinda masilahi ya CCM.
Mtaalamu huyo wa masuala ya utawala alisema hali hiyo itaendelea kuwapo hadi chama hicho kitakapoondoka madarakani na kuingia chama kingine madarakani.
Kwa upande wake, mwanasheria wa kujitegemea kutoka Zanzibar, Profesa Abdul Sheriff alisema asilimia kubwa ya uteuzi wa nafasi ya mwanasheria wa Serikali imejengewa msingi wa kulinda masilahi ya CCM. Profesa Sheriff alisema CCM bado imeshika ‘hatamu’ licha ya kuwapo majaji waliowahi kuonyesha msimamo wa kutoyumbishwa na mfumo huo na badala yake wakasimama katikati wakati wa kutekeleza majukumu yao.
“Kuna Jaji Robert Kisanga na marehemu Jaji Fransic Nyalali walionyesha msimamo wao wazi. Mifano iko mingi ya utendaji wao, lakini wapo majaji ambao walitimiza wajibu wao wakati bado ni makada, mfano Jaji Agustino Ramadhan alipojitokeza kuwani urais ilijenga maswali kwa muhimili wa Mahakama,” alisema.
Alifafanua kwamba udhaifu huo ungeweza kuondolewa na Katiba Mpya iliyokuwa na mapendekezo ya Tume ya Jaji Joseph Warioba. “Miiko ya utumishi wa umma ilibainishwa wazi kwenye rasimu hiyo na ingeweza kurejesha nidhamu na kuondoa udhaifu huo, lakini haikufanikiwa,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Profesa Abdallah Safari alisema pamoja na sheria kutoa nafasi kwa kila mmoja kuwania uspika, lakini imeonyesha udhaifu kwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuwania nafasi hiyo. Alisema udhaifu wa mfumo wa Serikali kujengwa na chama umesababisha kuwapo na ukandamizaji wa haki kwa vyama vingine vya siasa.
“Kwa mfumo ulivyo ni wazi hakuna mchakato bora wa kidemokrasia na tumepigania sana suala la udhaifu wa mfumo huo,” alisisitiza.
Profesa Safari alisema juhudi za kupambana na udhaifu huo ni kupigania Tume Huru ya Uchaguzi na siyo suala la Katiba kutokana na mazingira magumu yaliyojitokeza katika upatikanaji wake. Alisema mihimili yote imetekwa na CCM kwa sasa, hivyo hakuna mahali pa kukimbilia.
 
Kwa habari, matukio na michezo ni hapahapa tangakumekuchablog

No comments:

Post a Comment