HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 2
ILIPOISHIA
“Unajisikia kuumwa?” Lazaro
akaendelea kumuuliza.
“Nasikia kichwa kinagonga kwa
mbali”
“Hukuuma mtu?”
Sofia akatikisa kichwa.
“Sijauma mtu”
“Wewe si ulikuwa umekwenda
jikoni baada ya kuondoka kwenye chakula?”
Sofia alifikiri kisha akajibu.
“Ndiyo nilikwenda jikoni
kuchukua pilipili”
“Ulimkuta Pili?”
“Ndiyo nilimkuta”
“Halafu nini kilitokea?’
Sofia alivuta kumbukumbu kisha akatikisa kichwa.
SASA ENDELEA
“Sikumbuki. Kichwa kinaniuma
sasa”
Lazaro akashusha pumzi ndefu.
Akamtazama mke wake.
“Inawezekana ana malaria na
imepanda kichwani” alimwambia mke wake.
“Inawezekana” Vicky alisema
huku hofu na wasiwasi vikisomeka wazi usoni kwake.
“Sijui yule msichana
amemfanya nini. Mwenyewe hakumbuki kitu”
“Naona kama amemng’ata”
Wakati Waziri Mkuu Dastan
Lazaro na mke wake Vicky wakisemeshana, Sofia
alikuwa akiwasikiliza na kuwatazama kwa mshangao.
“Nimemng’ata nani?”
akawauliza.
“Pili, mpishi wetu” Lazaro
akamjibu.
Sofia akatikisa kichwa.
“Hapana, sijang’ata mtu”
“Umemng’ata na ndio sababu
una damu midomoni”
Mama yake naye akaongeza.
“Hicho kipande cha kitambaa
ulichokuwa umeshika ni cha nguo aliyovaa. Ulikichana wakati umemshika lakini
mwenyewe ulikuwa hujijui”
Mshangao wa Sofia sasa ulionekana waziwazi usoni kwake.
Lazaro alimshika mkono mke
ake wakatoka mle chumbani.
“Unadhani kitu gani
kimesababisha kifo cha yule msichana?” Lazaro akamuuliza mke wake.
Walikuwa wamesimama kando ya
mlango.
“Labda alimkaba koo”
“Sidhani”
Sofia akawafuta kusikiliza walichokuwa wanazungumza.
Wakaliona tumbo lake, lilikuwa limejaa kama
mja mzito. Wakati akiondoka kwenye meza ya chakula, tumbo lake halikuwa
hivyo.
“Mbona tumbo limejaa Sofia?” Mama yake
akamuuliza.
Sofia akalitazama tumbo lake na
kulishika.
“Limejaa kweli mama, na
nateuka ladha ya damu tupu”
Lazaro na mke wake wakatambua
kwamba Sofia
alikuwa amemfyonza damu yule msichana na ndiyo iliyokuwa imejaa kwenye tumbo
lake.
“Subiri upelekwe hospitali
mwanangu” Lazaro akamwambia.
“Nitakuwa nina malaria baba?”
“Bila shaka”
Lazaro alitoa simu yake
akampigia dereva wa mke wake ambaye muda ule alikuwa amesharudi nyumbani.
“Hebu njoo, kuna tatizo
kidogo” Lazaro alimwambia dereva huyo kwenye simu.
“Sawa, mzee ninakuja”
“Unaweza kukodi teksi ikulete
mara moja, tutailipia”
“Sawa mheshimiwa”
Lazaro akakata simu.
“Mtayarishe mwanao, dereva
anakuja umpeleke hospitali”
Mke wa Waziri Mkuu akamtazama
Sofia.
“Nenda chumbani mwako ubadili
nguo kisha usukutue mdomo wako” alimwambia.
“Sawa mama”
Sofia akaondoka.
“Sofia ndio amemuua yule mpishi wetu” Lazaro
akamnong’oneza mke wake.
“Sasa tutafanyaje” Vicky
akauliza kwa tashiwishi.
“Sijui
mke wangu. Kuliripoti
tukio hili ni sawa na kumwaga petroli kwenye moto, linaweza kumpa
matatizo Sofia na kuniweka mimi katika wakati mgumu japokuwa najua Sofia
alifanya hivyo akiwa
hajitambui lakini haitaonekana hivyo”
“Ninajua. Kuna mambo mengi
yataangaliwa na kusemwa”
“Ninaweza pia kutakiwa
kujiuzulu uwaziri mkuu kwa sababu tukio limetokea nyumbani kwangu na itaonekana
nimeshindwa kulizuia’
“Sasa tutafanyaje” Viccky
alirudia swali lake.
“Ile maiti tuihifadhi kwanza,
tungoje vipimo vya Sofia”
“Sawa. Ngoja nikamuandae.
Dereva akija twende naye”
Mke wa Waziri Mkuu akamfuata Sofia. Lazaro akawaita
wanawe wengine Vero na Monica.
“Nataka tukio hili liwe siri
ya humu ndani, lisitoke nje. Mmenielewa?”
Wasichana hao walikubali kuwa
wamemuelewa.
“Sofia ana malaria na imempanda kichwani, bila
kujielewa amemng’ata yule msichana mpishi wetu na kumfyonza damu hadi amemuua.
Kwa sasa sitaki habari hii ifike kwenye vyombo vya dola wala uraiani”
“Sasa ile maiti tutaipeleka
wapi?’ Vero akamuuliza baba yake.
“Tutaihifadhi humu humu ndani
tukisubri Sofia
apelekwe hospitali. Nimeshamuita dereva. Sasa twendeni tukasaidiane kuiondoa
kule jikoni’
Lazaro na wanawe wakashuka
ngazi na kuingia jikoni.
“Tumbebe tukamuweke stoo kwa
muda” Lazaro akawambia wanawe.
Waliubeba mwili wa Pili na
kwenda kuulaza stoo. Baada ya kumlaza, Lazaro aliichunguza ile sehemu ya
shingoni iliyokuwa inatoka damu. Akagundua kuwa ilikuwa imepigwa meno na
ilikuwa na tundu mbili za meno.
Wakati Waziri na wanawe
wanatoka stoo, mke wa Waziri na
Sofia walikuwa wanashuka ngazi. Sofia alikuwa ameshabadili nguo.
“Sisi tuko tayari” Mke wa
waziri alimwambia mume wake.
Waziri Dastan alimtazama Sofia. Safari hii alimuona
tofauti kidogo. Alikuwa amechangamka na alionekana wa kawaida.
“Mumsubiri dereva awapeleke”
“Sijui atakuja saa ngapi?”
Hapo hapo mlinzi akampigia
simu waziri. Waziri alipoipokea aliambiwa.
“Dereva ameshafika”
“Mwambie asubiri afunguliwe
geti”
Waziri akakata simu na
kumwambia mke wake.
“Dereva ameshafika, yuko nje”
“Ngoja nikamfungulie geti”
Alikuwa Vero ambaye alitoka kwenda kufungua geti. Dereva akaingia.
Waziri na mke wake pamoja na Sofia walikuwa wametoka na
kusimama karibu na banda la gari.
“Wapeleke hospitali, Sofia anaumwa” Waziri
akamwambia dereva huyo.
“Nichukue gari lipi?’
“Chukua gari langu binafsi”
Waziri alimwambia huku akimpa funguo.
Dereva alizipokea funguo za
gari akaingia ndani ya gari hilo
na kuliwasha.
Alilitoa kwenye banda
akalisimamisha. Mke wa waziri na Sofia
wakajipakia katika siti za nyuma. Walipofunga milango gari likaondoka. Lilitoka
kwenye geti na kukamata barabara.
“Tunakwenda hospitali gani?”
dereva akauliza.
“Tupeleke hospitali ya H.B.M”
mke wa waziri akamjibu.
Fuatilia hadithi hii katika blogy
hii hapo kesho
KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment