Sunday, October 8, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 8

Hadithi hii imeletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya Mabasi yaendayo Mikoni ya FREYS LUXURY COACH ifanyayo safari zake Tanga hadi Singida kila siku kupitia Moshi, Arusha na Babati, na hufanya hivyo kutokea Singida kila siku, simu 0622 292990

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 8

ILIPOISHIA

“Aling’atwa kwenye mshipa wa shingo na alifyonzwa damu kupitia mshipa huo”

“Sasa alifyonzwa na nani?”

“Haijajulikana bado, ndio tuko kwenye uchunguzi”

“Katika akili yangu mimi nadhani aliuawa na binaadamu, ndio akaja kumtupa pale”

“Huyo aliyemfyonza na kumuua ni binaadamu si mnyama”

“Binaadamu anaweza kumfyonza damu mwenzake hadi kumuua?’

“Ndio uchunguzi ulivyoonesha. Ni uchunguzi wa kitaalamu, hatuwezi kuupinga”

“Ni nani huyo anayefyonza watu damu?”

“Ndio tunamtafuta sasa. Unaweza kutusaidia nini?”

Mlinzi akaguna.

“Ndio kwanza ninasikia mauaji ya aina hiyo. Sijui kama kuna watu wanafyonza damu wenzao!”

SASA ENDELEA

“Inawezekana ni kwa sababu za kishirikina. Hujawahi kusikia watu wanachuna ngozi za walemavu wa ngozi au kuwakata mikono na wakati mwingine kuwaua kabisa?”

“Nimeshawasikia”

“Sasa hao ndio mfano wa hao wafyonza damu. Kila siku kunaibuka vitendo vipya vya uhalifu. Mimi sishangai kusikia habari kama hii. Kuna watu ni wapumbavu sana. Mtu anamuua ndugu yake kwa sababu ni albino ili apate utajiri”

“Kwa hiyo sasa hivi ndio kumeibuka huu mtindo wa kufyonza damu ya binaadamu kama mashetani!”

“Tunahitaji maelezo yako. Hebu nieleze nini kilitokea jana usiku ulipokuwa kaika lindo lako lakini kwanza nitajie tena jina lako na umri wako”

“Naitwa Mrisho Rajab, umri wangu ni miaka arobaini na miwili”

“Unaishi wapi?”

Niko Mwananyamala B”

“Kazi yako ni mlinzi sio?”

“Ndio, kazi yangu ni ya ulinzi”

“Ile shule unayolinda inaitwaje?”

“Ile ni shule ya msingi ya Kinondoni”

Inspekta Alex aliandika. Alipomaliza akamtazama tena Mrisho Rajab.

“Sasa nieleze nini kilitokea jana usiku?”

“Kilichotokea nadhni unakifahamu”

“Hilo sio jibu. Nataka niandike maelezo yako kwa sababu wewe ndiye shahidi pekee uliyeshuhudia tukio hilo. Ilikuwa ni muda gani ulipoona hilo gari?”

“Ilikuwa ni mjira ya saa nane au saa nane na nusu usiku”

“Enhe…nini kilitokea?”

“Lilitokea hilo gari kunako kiwanja cha shule. Mimi nilikuwa nimekaa nje ya darasa moja”

“Lilikuwa gari la aina gani?”

“Ni Toyota Land Cruisser la rangi nyeupe”

“Gari hilo lilipotokea lilifanya nini?”

“Lilisimama karibu na miti ya magoli ya upande mmoja wa kiwanja hicho. Lilisimama kwa karibu dakika tano bila mtu yeyote kufungua mlango. Wakati nainuka ili niende nikamuulize aliyesimamisha gari lile pale, nikaona mlango unafunguliwa”

“Mlango uliofunguliwa ulikuwa wa mbele au nyuma?”

“Ulikuwa mlango wa dereva”

“Sawa, endelea”

“Akashuka mtu mmoja. Alikuwa amevaa pama, akafu….”

“Subiri. Mbali ya pama, alikuwa amevaa nini au nguo za rangi gani?”

“Alikuwa amevaa shati na suruali, sikuweza kuona vizuri zilikuwa za rangi gani”

“Alikuwa mtu mrefu, mfupi, mwembamba au mnene…?”

“Alikuwa mrefu kiasi lakini hakuwa mnene wala hakuwa mwembamba sana”

“Mtu huyo alifanya nini baada ya kushuka kwenye gari?”

“Alifungua mlango wa gari wa nyuma wa upande ule ule alioshuka yeye akautoa ule mwili wa msichana lakini muda ule niliona kama gunia hivi”

“Akaufanya nini?”

“Ndio pale nikawa ninamfuata, aliponioana alinirushia ule mwili ukaanguka chini miguuni mwangu. Wakati nutazama vizuri, yule mtu aliwahi kupanda kwenye gari lake. Hata hivyo nilimfuata akataka kunigonga na gari”

“Alitaka kukugonga kivipi?”

“Nilitinga mbele ya gari lake”

“Uliweza kuona ndani ya gari hilo kama kulikuwa na watu wengine?”

“Sikuweza kuona. Gari hilo liliondoka kwa haraka”

“Baada ya hapo ulifanya nini?”

“Nilipiga simu polisi”

“Ulipotupiwa huo mwili wa msichana miguuni mwako alikuwa bado yuko hai au alikuwa ameshakufa?”

“Alikuwa ameshakufa”

“Je kama utamuona tena yule mtu unaweza kumtambua?”

“Naweza kumtambua kwa sababu nilimmulika tochi usoni na nilimuona vizuri”

“Jana usiku nilipokuuliza uliniamabia kuwa namba za usajili za gari hilo hukuziona?”

“Sikuwahi kuziona”

“Sawa. Soma maelezo yako halafu weka sahihi”

Alex alimpa mlinzi huyo ile karatasi aliyokuwa anaiandika ili aisome.

Mlinzi aliichukua na kuisoma. Alipomaliza kuisoma Alex alimuuliza.

“Maelezo yako ni sahihi?”

“Ni sahihi”

“Sasa weka sahihi yako hapo chini”

Mlinzi aliweka sahihi yake chini ya maelezo yake.

“Tuachie namba yako ya simu”

Mlinzi huyo alitaja namba yake ya simu. Alex akaiandika chini ya maelezo yake.

“Kuna kingine?” Mlinzi huyo akauliza akionesha haraka ya kutaka kuondoka. Hakuna anayependa kukaa kituo cha polisi kwa muda mrefu.

“Unaweza kwenda, tutakapokuhitaji tutakujulisha kupitia simu yako”

“Sawa, asante sana”

Mlinzi akanyanyuka na kutoka.

Hakuna anayefurahia kuhojiwa kituo cha polisi hata kama ni kwa ajili ya kutoa ushahidi. Mlinzi huyo alipoondoka kituoni hapo shati lake lilikuwa limeloa kwa jasho. Dakika zile za kuhojiwa maswali zilikuwa kama dakika za jinamizi. Aliporuhusiwa kuondoka alijisikia amepata ahueni kubwa.

Dakika ile ile Waziri Mkuu alimpigia simu Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri huyo alipopokea simu ya bosi wake alisema.

“Hello mheshimiwa…habari ya asubuhi?”

“Habari ya subuhi si nzuri, nimepata taarifa sasa hivi kuwa mpishi wangu ameuawa”

Waziri wa Mambo ya ndani akashituka.

“Ameuawa wapi?”

“Sijapata taarifa kamili. Mke wangu alimpigia simu alipoona hatokei, ile simu ikapokelewa kituo cha polisi ambako alielezwa kuwa msichana huyo ameuawa”

“Polisi wameeleza ameuawa wapi na aliyemuua ni nani?”

“Wamesema maiti ya msichana huyo iliokotwa jana usiku katika eneo la shule ya Kinondoni ikiwa na jeraha shingoni kwake”

“Sasa acha niwasiliane na kamanda wa polisi anieleze nini kimetokea na nini kinaendelea”

“Sawa, wasiliana naye’

Waziri Mkuu akakata simu.

Waziri wa Mambo ya Ndani Jackson Maro akampigia simu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Dar.

Kwa vile kamanda wa polisi alikuwa amemzidi kiumri waziri wa Mambo ya Ndani, alipopokea simu yake Maro alimwamkia.

“Shikamoo”

“Marahaba, habari ya kazi” Kamanda wa polisi alimuitikia.

“Ni nzuri. Umepata taarifa ya mauaji yaliyotokea jana usiku huko Kinondoni?’

ITAENDELEA kesho hapahapa tangakumekuchablog, KUMEKUCHA UPYA

No comments:

Post a Comment