HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 5
ILIPOISHIA
Kwa mtu mwenye uzoevu mdogo
tu wa vitendo vya uhalifu ilikuwa kazi ndogo tu kuutupa mwili wa Pili na
kukimbiza gari kuondoka mahali hapo. Lakini kwa afisa wa serikali aliyezoea
kukaa ofisini na kutoa amri kwa maneno, ilikuwa kazi kubwa sana.
Kitendo kile cha kufumwa na
mlinzi kilimfanya ataharuki na kuamsha mapigo yake ya moyo. Ingawa alifanikiwa
kufika nyumbani kwake salama hakuamini kwamba ilikuwa salama. Alijiambia huenda
mlinzi aliziona namba za gari lake
wakati
akikimbia na atawatajia polisi.
Karibu njia nzima alikuwa akilaani na kujiona
alikuwa amefanya kitendo cha kizembe.
Wakati analizima moto gari hilo alishusha pumzi ndefu
kisha akafungua mlango na kushuka. Mke wake
alikuwa amesimama
kwenye mlango wa nyumba yake akimsubiri.
“Vipi?” akamuuliza.
Waziri Mkuu hakumjibu kitu,
aliingia ndani. Aliketi sebuleni akauweka mguu wake juu ya mwingine. Kitendo
hicho kilikuwa ni cha mazoea ya ukwasi
tu, hakikuwa cha kujinafasi katika muda ule wa taharuki.
SASA ENDELEA
“Umefanikiwa?” mke wake
alimuuliza tena alipomuona yuko kimya.
“Nimefanikiwa lakini…”
Mke wake akashituka kidogo.
“Kumetokea nini?”
“Unajua nilikwenda kumtupa
kinondoni karibu na eneo la shule. Nikadhani hapakuwa na mtu”
Vicky alianza kutikisa
kichwa.
“Enhe. Nini kilitokea?”
“Wakati nataka kuuweka chini
ule mwili, mlinzi wa ile shule aliniona akaja haraka na kunimulika tochi.
Mke wa Waziri Mkuu akapiga
mluzi.
“Alikuona?”
“Sijui lakini nadhani
hakunitambua. Nikautupa ule mwili chini na kukimbilia kwenye gari ili
asinitambue. Alikuwa ameshika
sime…”
“Enhe..?’
“Sasa sijui huko nyuma nini
kilitokea. Mimi niliondoka na gari haraka”
“Lakini nadhani hakukutambua”
“Ndiyo imani yangu”
“Habari zaidi tutazipata hapo
asubuhi”
*******************
Land Rover ya polisi wa kituo
cha Kinondoni ilisimama pembeni mwa barabara karibu na uwanja wa shule ya msingi.
Polisi aliyekuwa amesimama na mlinzi alilifuata gari hilo kwa hatua za hima.
Polisi wemzake walipomuona walishuka kwenye gari.
Walikuwa polisi wanne akiwemo Inspekta Alex.
Alimpigia saluti Inspekta
Alex kisha
akamwambia.
“Tukio limetokea sehemu ile”
Alimuonesha kwa kidole mahali
hapo.
Dereva wa gari hilo alilielekeza gari
mahali walipooneshwa na kumulika taa. Mwili wa msichana ulionekana waziwazi
pamoja na mlinzi wa shule aliyekuwa amesimama kando yake.
Walikwenda mahali hapo na
kuukagua mwili huo.
“Hebu tueleze nini
kilitokea?” Inspekta Alex akamuuliza mlinzi wa shule.
“Nilikuwa nimekaa mbele ya
jengo la shule nikiendelea na shughuli zangu za ulinzi, nikaona gari linasimama
hapa…” Mlinzi alieleza huku akionesha mahali liliposimama gari hilo.
“Lilikuwa gari la aina gani”
“Ni hizi Toyota Land Cruiser”
“La rangi gani?”
“Nyeupe”
“Namba
zake za usajili
uliziona?”
“Namba sikuwahi kuziona”
“Enhe. Gari hilo liliposimama hapa nini kilitokea?”
“Niliona mtu mmoja akishuka
akafungua mlango wa nyuma na kumtoa huyu mtu. Alikuwa amemmbeba kwenye mikono
yake. Hapo nikashituka na kumfuata haraka. Aliponiona akanirushia huyu mtu,
akaanguka kando
yangu. Yeye mwenyewe akaimbilia kwenye gari na kulipiga moto”
Mlinzi alisita kidogo akavuta
pumzi kisha
akaendelea.
“Ilikuwa
kidogo anikanyage kwa sababu nilikuwa namfuata ili anieleze ni kwanini amemtupa
huyu mtu hapa”
“Nadhani atakuwa ameshakufa. Vaeni gloves
zenu mumpakie kwenye gari” Inpekta Alex aliwambia polisi wenzake.
Polisi hao walitoa mipira ya
kuvaa mikononi kutoka mifukoni mwao na kuivaa mikononi kisha wakaubeba mwili wa Pili na kwenda
kuupakia kwenye gari.
“Na wewe utakuja asubuhi
kituoni uandikishe maelezo yako. Wewe ndiye shahidi pekee uliyeona tukio hili”
Inpekta Alex alimwabia mlinzi.
“Sawa. Nitafika kituoni
asubuhi”
Alex alitoa notibuku yake
mfukoni na kalamu.
“Unaitwa nani?” alimuuliza
mlinzi.
“Naitwa Mrisho Rajab”
“Shule unayolinda inaitwaje?”
“Ni shule ya msingi ya
Kinondoni”
“Okey”
Alex aliirudisha notibuku
yake mfukoni.
“Tuonane hapo kesho”
alimwambia mlinzi huyo.
“Sawa afande”
Inspekta Alex alilifuata gari
la polisi lilipokuwa limesimama akajipakia na gari hilo likaondoka. Kwanza
walikwenda kituo cha polisi cha Kinondoni.
Mwili wa Pili ulipekuliwa,
ulikutwa na simu moja ya bei mbaya na saa ya mkononi iliyokuwa imevunjika kioo.
Vitu hivyo vilihifadhiwa
mikononi mwa polisi kisha mwili huo ukapelekwa hospitali ya Muhimbili.
Daktari aliyeupokea mwili huo
baada ya kuuchunguza kwa dakika chache alimwambia Inspekta Alex.
“Huyu ameshakufa”
“Labda utueleze alikufaje,
aliuawa? Na kama aliuawa aliuawa kwa kitu
gani? Na pia utueleze kama aliwahi kubakwa”
“Tutatoa majibu kesho baada
ya uchunguzi kamili”
“Kwa hiyo tuje kesho kufuatia
majibu”
“Ndiyo mje kesho majira ya
saa nne, tutakuwa tumekamilisha uchunguzi wetu”
“Sawa dokta, kwaheri”
Alex na polisi wenzake
wakaondoka.
Walirudi kituoni. Alex
akaingia ofisini kwake na kuanza kuipekua simu ya Pili.
Ilikuwa imeseviwa majina ya watu wengi. Majina mengine
yaliwekwa kwa herufi moja au mbili. Alex akazingatia jina moja lililokuwa na
herufi mbili za ML. Jina hilo
lilionekana katika meseji nyingi za mapenzi zilizokuwa ndani ya simu hiyo.
Alex
akahisi kwamba
aliyewakilishwa kwa herufi hizo ndiye aliyekuwa mpenzi wa marehemu na
kwamba kama atapatikana ataweza kuwaeleza, msichana aliyeuwa
alikuwa nani, alikuwa anaishi wapi na pia kuisaidia polisi katika
uchunguzi.
Alex akampigia simu kwa
kutumia simu ileile.
Simu ikaita kwa muda mrefu kisha ikapokelewa. Sauti
nzito ya mtu aliyetoka usingizini ikauliza.
“Unanipigia saa hizi, ulikuwa
wapi?”
Kauli ile peke yake ilitosha
kumpa imani Alex kuwa mtu huyo aliyempigia hakuwa akifahamu chochote kuhusiana
na tukio lililomtokea marehemu.
“Kuna tatizo limetokea hapa”
Alex akamwambia.
“Na wewe ni nani?”
“Mimi ni afisa wa polisi,
niko kituo cha Kinondoni. Kuna tatizo limemtokea huyu msichana. Tunakuomba
ufike mara moja”
“Mh! Tatizo gani tena?”
“Huyu msichana ameshambuliwa na watu
wasiofahamika. Tumekuta namba yako kwenye simu yake, tunajua mnafahamiana”
“Ndiyo tunafahamiana”
“Sasa hebu njoo mara moja
hapa kituoni”
“Umeniambia ameshambuliwa,
ameshambuliwa
na nani?”
“Nimekwambia kwamba ameshambuliwa na watu
wasiojulikana”
“Hebu mpe simu nizungumze
naye”
“Hawezi kuzungumza, ndio
sababu nimekupigia mimi”
“Loh! Aisee umenishitua sana. Subiri nakuja”
“Tunakusubiri.”
Alex akakata simu.
Baada ya nusu saa tu teksi
ilisimama nje ya kituo cha polisi. Kijana mmoja mtanashati aliyekuwa amevaa
vizuri alishuka kwenye teksi na kuingia katika kituo hicho cha polisi.
Alijitambulisha kaunta
akapelekwa katika ofisi aliyokuwemo Inspekta Alex.
Alex akamtazama kabla ya
kumwambia.
“Kaa kwenye kiti?”
Itaendelea kesho hapahapa usikose kwani KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment