KAMA UNATAKA FEDHA ZA MAJINI
9
ILIPOISHIA
“Nikwambie ukweli tatizo lako
ni gumu. Kama nitajidai kuwa naweza kukusaidia
ninaweza kupata matatizo kwani hao majini wanaokalia hizo pesa ni majini
hatari. Ni majini wa jamii ya Subiani. Sisi huwaita Subiani Damisi au jini
maiti. Wanaweza kukukata mara moja”
Ustaadhi huyo aliponiambia
hivyo alinitisha. Uso wangu ulifadhaika hapo hapo.
Hapo nikaona nimuhadithie
kile kisa cha yule mganga aliyetandikwa bakora.
Utaadhi huyo alipokisikia
kisa hicho aliangua kicheko.
“Huyo mganga alipata tamaa.
Alitaka kuzichukua pesa hizo akiamini kuwa alikuwa na majini wanaoweza
kumlinda. Lakini huyo jini wa baba yako alipomfuata, majini wa huyo mganga
walisambaratika. Ni bahati yake alitandikwa bakora. Angeweza kumuua kabisa”
“Kwa hiyo utanisaidiaje”
nikamuuliza tena mganga huyo huku sauti yangu ikiwa imenywea.
“Sikufichi, hakuna mganga
yeyote atakayeweza kukusaidia kwa tatizo hilo
labda akudanganye tu”
SASA ENDELEA
“Una maana kwamba mke wangu
naye atafanywa taahira”
“Hilo ni lazima muda wake ukiwadia”
“Mpaka dakika hii sioni faida
ya zile pesa kwa sababu zimeshagharimu maisha ya mama yangu na mwanangu na bado
zitagharimu maisha ya mke wangu. Ni afadhali niende nikazitupe, zisiwe mikononi
mwangu”
“Hao majini wa pesa hizo
hawatakubali uzitupe kwa sababu baba yako alikwenda kuzitafuta huko Zanzibar na alikubali
masharti aliyopewa”
“Lakini ni yeye aliyezifuata
huko Zanzibar
na mwenyewe ameshakufa. Mimi hazinihusu”
“Zinakuhusu kwa sababu baba
yako alikutaja kama mrithi wake na ndio maana
zilikuja kwako”
Ustaadhi huyo alizidi
kunichanganya, nikainamisha kichwa changu na kukitikisa.
“Baba yangu atakuwa na hatia
kubwa mbele ya Mungu” nikajisemea kwa hasira.
“Wakati wewe unasema hivyo,
wako watu wanaozitafuta pesa hizo kwa udi na uvumba lakini hawajafanikiwa
kuzipata”
“Hawajali kuwapoteza wake zao
na watoto wao?”
“Mbele ya pesa hawajali”
“Sasa huu ulimwengu unakwenda
wapi!”
“Unajua binaadamu tuna roho
tofauti. Pesa zimewabadili watu na zimeubadili ulimwengu wetu mpaka umekuwa
hivyo”
“Sasa sijui niende wapi?”
“Pata muda wa kutafakari
zaidi”
Ustaadhi aliponiambia hivyo
nikainuka. Kwa kweli nilikuwa nimechnaganyikiwa na kuchoka.
“Nimeshatafakari vya kutosha.
Lengo langu ni moja tu kumuokoa mke wangu na kumkomboa mama yangu na mwanangu”
nikamwambia huku nikitoka nyumbani kwake bila kumuaga.
Ni vizuri nikiri kuwa
nilikabiliwa na mtihani mgumu katika maisha yangu. Kulikuwa na kila dalili kuwa
nisingeweza kushinda mtihani huo.
Lilikuwa ni tatizo
lililohitaji elimu ambayo sikuwa nayo. Waganga ambao ndio niliokuwa nikitegemea
wanipe msaada wao walikuwa wananikatisha tamaa.
Wakati natoka nyumbani kwa
yule mganga, akilini mwangu niliunda picha ya mama yangu na mwanangu wakienelea
kuteseka kwenye lile pango hadi wanakufa kwa dhiki.
Vile vile niliunda picha ya mke wangu niliyekuwa
nikimpenda naye akichukuliwa kafara na kuwekwa katika pango hilo.
Kama hali itakuwa hiyo, nilijiambia. Sitaweza tena kurudi
kazini kwangu. Nitalazimika kubaki hapo hapo Korogwe nimhudumie mke wangu hadi
naye atakapokufa.
Na bila shaka, nikaendelea
kujiambia, hivyo ndivyo wanavyofanya watu wanaomiliki pesa za majini kama alivyokuwa baba yangu. Wanaendelea kuwahudumia watu
wao waliowatoa makafara huku wakifurahia pesa za bure walizopewa na majini.
Hili jambo halikuingia
akilini mwangu kabisa. Niliona sawa na kumfanyia unyama binaadamu mwenzako ilimradi
tu umiliki pesa.
Mtu unapomlaumu jambazi kuwa
anatumia bunduki kuua watu na kupora fedha, akumbuke kuna na huyu jambazi
mwingine anayemtoa kafara mke wake ili apate pesa.
Nilipofika nyumbani niliingia
chumbani kwangu nikajilaza kitandani na kuendelea kuwaza.
Nilikuwa mtu wa kuwaza tu wakati
wote. Nikiwa hapo kitandani niliwaza sana
lakini licha ya kupoteza muda mwingi sikuwa nimepata ufumbuzi wowote.
Pengine utashangaa kuwa
niliwaza kila kitu lakini wazo la kuwa tajiri halikupita akilini mwangu kabisa.
Nilitaka niendelee kuishi nikiwa masikini vile vile na nife nikiwa masikini.
Mshahara wangu ninaolipwa kila mwezi na jeshi ulitosha kabisa kuendesha maisha
yangu.
Utajiri ule wa pesa
zilizokuwa chini ya kitanda nilichokuwa nimekilalia wakati ule, sikuuhitaji. Ni
kweli kuwa hakuna mtu asiyetaka utajiri lakini utajiri wa kuangamiza maisha ya
watu haukuwa utajiri. Ni sawa na ujambazi tu.
Baada ya kuwaza kwa muda mrefu, usingizi ulinipitia
hapo hapo nikalala. Wakati nimelala nikaota ndoto. Niliota nimesafiri na boti kwenda
Pemba. Nikafika katika kijiji kinachoitwa
Giningi. Nikakuta kisima kilichochimbwa miaka mingi iliyopita.
Wakati nakishangaa kile
kisima nilisikia sauti ya mwanamke ikiita jina langu.
Nilipogeuka niliona mwanamke
amesimama kando ya mti akiniashiria kwa mkono nimfuate pale. Nikamfuata.
Nilipofika karibu yake nikagundua kuwa alikuwa ni yule mwanamke wa kijini
aliyekuwa mke wa baba yangu.
“Umefuata nini huku?”
akaniuliza.
“Nimekuja kumtafuta yule mzee
aliyempa pesa baba yangu”
“Nyumba yake ile pale”
Mwanamke huyo akanionesha
nyumba iliyokuwa mbali kidogo na mahali tulipokuwa.
Wakati naitazama ile nyumba akaendelea
kuniambia.
“Lakini hivi sasa hayuko
amekwenda shamba”
“Na wewe unafanya nini hapa?”
nikamuuliza na yeye.
“Hapa ndipo nilipotoka mimi.
Na mzee uliyemuuliza ndiye baba yangu. Nataka nikukumbushe kitu, karibuni mama
yako atakufa nimekuja kuchukua idhini kwa baba yangu ili tumtoe kafara mke wako
achukue nafasi ya mama yako”
Maneno hayo yakanishitua.
“Sisi tunataka kuondoka
kurudi Dar, mke wangu huwezi kumpata”
“Hamuwezi kuondoka tena,
mtabaki pale pale Korogwe. Mke wako ataishi kwenye pango na ni wewe
utakayemuhudumia”
“Likizo yangu ikiisha
nitatakiwa kazini”
“Hatutakuruhusu uendelee na
kazi yako kwa sababu tumeshakupa utajiri”
Ndoto yangu ikaishia hapo
hapo. Nikajikuta nimezinduka kutoka usingizini. Kumbe kilichonizindua zilikuwa
kelele za simu yangu iliyokuwa inaita. Si unazijua simu hizi za kichina zilivyo
na sauti kali.
Nikaitoa simu hiyo kwenye
mfuko wa shati langu na kutazama skirini ya simu. Nikaona aliyekuwa akinipigia
alikuwa mke wangu. Sikujua ni kwanini moyo wangu ulishituka ukawa unanienda
mbio.
Nikaipokea ile simu.
“Hello!”
“Ulikuwa umelala?” Sauti ya mke wangu ikauliza.
“Simu yako ndiyo imeniamsha”
“Naisikia sauti yako umekuwa
nzito kama una mafua”
“Nilikuwa nimelala. Hamjambo?”
“Hatujambo. Nataka
kukujulisha kuwa kesho nakuja huko”
Nikaduwaa kwa sekunde kadhaa
kabla ya kujibu chochote. Akilini mwangu
niliwaza kwamba mke wangu akija Korogwe tu amekwisha.
“Kwani hali ya baba
inaendelea vizuri?”
“Ndiyo, yuko vizuri. Yeye
ndiye anayenihimiza nirudi kwa mume wangu. Ameniambia nimekaa kwake kwa muda
mrefu”
Nilishindwa kumwambia mke
wangu kuwa asije, angeniuliza sababu na nisingekuwa na jibu kwa wakati ule.
“Mume wangu mbona umenyamaza,
hutaki nije huko?” Sauti ya mke wangu ikauliza.
“Hapana. Nilikuwa nameza
dawa. Kichwa kinaniuma. Wewe njoo tu” nikajisemea baada ya kushutumiwa.
“Au una mwenzangu huko,
niambie tu usinifiche”
“Hapana mke wangu.Mimi niko
kwenye msiba wa baba, nitafute mwanamke wa nini!”
“Naona tangu jana nikikwambia
suala la kuja huko unasitasita”
“Sijasitasita ila wasiwasi
wangu upo kwenye hali ya mzee. Kama unasema
hivi sasa anaendelea vizuri basi unaweza kuja tu”
“Nitumie nauli”
“Nitakutumia”
“Ni hapo kesho
tutakapokutana”
“Mungu akituweka hai”
Mke wangu akakata simu.
Badala ya kuwa na furaha ya kuzungumza na mke wangu, moyo wangu ukajaa
machungu.
Kile nilichokuwa nikikihofia
sasa kilikuwa kinakaribia kutokea.
Mke wangu umeng’ang’ania kuja
huku lakini huku kuna matatizo ambayo siwezi kukuambia kwa sasa, nikajikuta
nikisema peke yangu.
Nikajiambia kama mke wangu
atakuja hapo kesho huenda huo ukawa ndio mwisho wake.
Licha ya kutambua bayana madhara ambayo yangeweza kumkuta mke wangu
nilishindwa kumzuia asije. Mwenyewe ameshaanza shutuma zisizo na msingi, hajui
jinsi dakika zake zilivyokuwa zinakaribia.
Wakati nikiwaza hivyo kichwa
changu kilikuwa kipo kwenye mchakato wa haraka haraka kutafuta ufumbuzi wa
suala hilo.
Nikakumbuka ile ndoto niliyoiota kwamba nilikwenda Pemba
mahali panapoitwa Giningi na kukutana na
yule mwanamke wa kijini.
Je nini kitatokea? Usikose kuwa nami kesho hapahapa kumekucha.com
No comments:
Post a Comment