Saturday, October 14, 2017

HADITHI, MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI SEHEMU YA 14

HADITHI inaletwa kwa hisani kubwa ya Kampuni ya mabasi ya usafirishaji abiria Tanga hadio Singida kila siku kupitia, Moshi, Arusha ma Bababti, na hufanya hivyo kutokea Singida kwenda Tanga, kwa mawasiliano piga simu, 0622 292990

MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA UKINGONI 14

ILIPOISHIA

“Labda tumepishana kiswahili. Uliponiamba kwamba jana ulitoka kazini saa nne usiku nilielewa kwamba ulikuwa na gari hili”

“Hapana, ni gari jingine”

“Sawa. Nitakwenda kuzungumza zaidi na Waziri Mkuu mwenyewe”

“Naamini atakueleza vizuri”

                                     ************

Jua lilikuwa linakaribia kuchwa wakati kachero Thabit Kombo alipofika nyumbani kwa Waziri Mkuu. Safari hii alikwenda peke yake akiwa na jalada lake mkononi.

Alikaribishwa sebuleni. Waziri Mkuu akamuuliza kama alihitaji kinywaji chochote.

Kombo akatikisa kichwa.

“Asante mheshmwa. Sitahitaji kinywaji chochote. Nimerudi tena kwa sababu kumejitokeza utata kidogo, ninahitaji ufafanuzi”

SASA ENDELEA

“Utata gani uliojitokeza?’

Ingawa sauti ya Waziri Mkuu ilikuwa tulivu lakini moyo wake ulikuwa ukienda mbio.

“Kama nilikusikia vizuri uliponipa maelezo yako kwa mara ya kwanza uliniambia kwamba marehemu Pili Amrani aliondoka kazini hapa nyumbani, jana saa kumi na moja jioni baada ya kueleza kuwa kchwa kilikuwa kinamuuma”

“Sasa ni utata gani uliojtokeza?’

“Nilipokuwa namhoji baba mzazi wa marehemu aliniambia kwamba hadi saa moja usiku mwanawe alikuwa bado yuko kazini hapa nyumbani. Je mheshimiwa waziri atatoa maelezo gani kuhusiana na utata huo?”

Waziri Mkuu alishituka lakini alifanikiwa kuuzuia uso wake usioneshe taswira ya mshituko.

“Yeye ana ushahidi gani kuwa mwanawe alikuwa hapa nyumbani hadi muda huo?”

“Alituambia kuwa waliwasiliana kwa meseji. Mzee Amrani alimtumia marehemu meseji muda huo kumuuliza kama alikuwa ameshatoka kazini. Marehemu akamjibu kuwa alikuwa bado yuko kazini”

Sasa macho ya mheshimiwa Waziri Mkuu yalianza kuwa makali. Kombo aliyakwepa kwa kugeuza uso wake kando.

“Alikwambia waliwasiliana muda gani?”

“Saa moja usiku”

Waziri Mkuu alitaka kutikisa kichwa lakini alipata hoja.

“Alikuonesha hiyo meseji ambayo marehemu alimtumia?”

“Alinionesha kwenye simu yake”

“Uliiona?”

“Ndiyo”

“Sasa unadhani ni nani alikupa maelezo yasiyo sahihi?” Waziri Mkuu akauliza kwa sauti iliyoonesha kuwa ametaharuki.

“Hatuko huko mheshimiwa. Mmojawapo anaweza kuwa ameghafilika”

“Nilichokueleza mimi kilikuwa sahihi. Kama kulikuwa na tatizo lilikuwa kwa marehemu mwenyewe”

“Tatizo, kivipi?”

“Inawezekana marehemu alimdanganya baba yake kuwa yuko kazini, kumbe alikuwa kwenye shughuli zake mwenyewe lakini hapa kwangu hakuwepo muda huo”

“Nimekuelewa. Yaani ni kwamba marehemu alimwambia baba yake kuwa bado yuko kazini, kumbe hakuwepo. Alikuwa ameshaondoka”

“Na ninadhani kutokana na maelezo hayo marehemu hakuwa anaumwa kama alivyotuambia bali alisingizia tu akiwa na sababu zake. Kama alikuwa anaumwa kweli angemwambia baba yake”

“Nimekuelewa”

“Una swali jingine?”

“Sina mheshimiwa”

“Karibu sana”

Kombo alihisi Waziri Mkuu alikuwa amechukia. Wakati anajiandaa kuinuka akaisikia sauti ya Waziri Mkuu.

“Nimesikia kwamba gari langu limekamatwa”

Kombo hakutaka kulizungumzia suala la gari hilo. Alipitisha sekunde mbili hivi kabla ya kumjibu.

“Mheshimiwa gari hilo lilikamatwa na trafiki baada ya dereva wake kugonga gari la mtu mwingine”

“Hilo ni suala dogo tu, kwani kuna mtu aliyejeruhiwa”

“Hakuna aliyejeruhiwa”

“Mbona dereva wangu amecheleweshwa sana, kama trafiki wameshapima ajali iliyotokea na labda wamezuia leseni yake, basi zifuate taratibu zingine”

“Natumaini hadi sasa watakuwa wamekamilisha hizo taratibu”

Kombo akainuka. Waziri Mkuu naye aliinuka na kumuaga.

“Karibu sana”

Wakati Kombo anatoka nyumbani kwa Waziri Mkuu aliliona gari la Waziri Mkuu likiwasili. Ndani ya gari hilo alikuwamo dereva wa gari hio na msaidizi wa Waziri Mkuu.

Polisi walikuwa wameshaliachia baada ya msaidizi w wa Waziri Mkuu kukubaliana na mwenye gari lililogongwa kuwa watagharamikia matengenezo yake.

                                           ********

Baada ya mazishi ya Pili Juma, upelelezi wa kesi hiyo ukaachwa. Na Waziri Mkuu hakuulizia tena suala hilo.

Sasa suala lililokuwa linakula vichwa katika familia ya Waziri Mkuu ni kile kitendo cha binti wa Waziri Mkuu kumfyonza damu mpishi wao hadi kumuua.

Baada ya vipimo vya hospitali kuonesha kuwa Sofia hakuwa na malaria, Waziri Mkuu alihisi kwamba binti yake huyo anaweza kuwa na matatizo ya akili. Akataka kumpeleka hospitali ili akafanyiwe uchunguzi wa akili yake lakini hakutaka uchunguzi huo ufanyike hapa nchini kwani alitaka uwe wa siri. Na matokeo yake pia yawe siri.

“Mimi nafikiri tumpeleke Nairobi” Waziri Mkuu alimwambia mke wake jumapili moja walipotoka kanisani.

“Ni sawa. Akifanyiwa uchunguzi kule, habari zake hazitajulikana”

“Mimi bado nina wasiwasi kuwa ana matatizo. Kuna siku naona anakuwa mkimya sana”

“Sasa atakwenda na nani huko Nairobi?”

“Uende naye wewe”

“Lini?”

“Nataka iwe haraka iwezekanavyo. Itabidi leo nifanye mawasiliano na ile hospitai ninayoifikiria. Ikiwezekana kesho kutwa muondoke”

“Sawa”

“Ninapokagua vitabu vyake vya shule anaonekana anaendelea vizuri tu, sijui ana tatizo gani. Kama ni matatizo ya akili ni vizuri yajulikane mapema na yapatiwe tiba kabla hali haijakuwa mbaya”

“Ni kweli”

Jumapili ile ile baada ya chakula cha mchana, Sofia na Monica waliingia chumbani kupumzika. Waziri Mkuu na mke wake walikuwa wamekaa sebuleni wakiendelea kuzungumza. Vero alikuwa hayupo nyumbani.

Kwa kawaida kila inapofika saa kumi jioni siku za jumapili Sofia na Monica huenda katika masomo ya tuisheni lakini siku ile waliendelea kubaki chumbani hadi muda huo.

Ilipofika saa kumi na nusu mke wa Waziri Mkuu alipata wasiwasi baada ya kutowaona Sofia na Monica, akawafuata chumbani walimokuwa.

Alifungua mlango na kuingia ndani. Alikuta hali iliyokuwa imemshangaza. Monica alikuwa amelala chini wakati Sofia alilala kichali chali kitandani huku miguu yake ikiwa chini. Alikuwa kama mtu aliyekuwa ameketi kisha akaamua kujilaza.

Kulikuwa na michirizi ya damu kwenye shingo ya Monica. Kadhalika kwenye midomo ya Sofia pia kulikuwa na damu na  tumbo lake lilionekana limejaa.

Mke wa Waziri Mkuu alimtazama Monica pale chini alipokuwa amelala. Akajiuliza maswali matatu.

Kwanini Monica alikuwa ameala chini?

Kwanini shingo yake ilikuwa na michirizi ya damu?

Damu ile ilitoka wapi?


Itaendelea kesho hapahapa usikose Uhondo huu nini kitatokea

No comments:

Post a Comment