HADITHI hii inaletwa kwenu kwa hisani kubwa ya Kampuni ya usafirishaji abiria ya FREYS LUXURY COACH Tanga hadi Singida kila siku, na Singida Tanga kupitia Moshi, Arusha na Babati, Tanga wasiliana na simu no, 0622 292990
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 9
ILIPOISHIA
Kamanda wa polisi alianza kubabaika. Alibabaika kutokana
na ukweli kuwa hakuwa
amepata taarifa yoyote wakati alikuwa ndiye kamanda
wa polisi wa mkoa huo.
“Sijapata bado” akasema kwa
sauti ya wasiwasi.
“Kwanini?”
“Leo wamenicheleweshea
taarifa”
“Eh! Mpishi wa Waziri Mkuu
ameuawa jana usiku, wewe huna taarifa. Sasa sisi tumuulize nani?”
Kamanda wa polisi alionesha kuhuzunika waziwazi.
“Hawa jamaa wananicheleweshea
taarifa na nilikwisha waeleza taaarifa za mauaji
waniwasilishie haraka. Sasa acha niwaulize halafu nitakupigia”
“Inaonekana katika ofisi yako
mambo hayaendi sawa!”
“Tatizo ni ucheleweshwaji tu
wa taarifa. Hilo
tatizo nitalirekebisha lisitokee tena”
SASA ENDELEA
Waziri wa Mambo ya Ndani
alikuwa ameshakata
simu.
Kamanda wa polisi alipogundua simu ilikuwa imeshakatwa
alimpigia haraka afisa wa chini yake ambaye ni afisa upelelezi wa mkoa.
“Nini kinaendelea hapo
ofisini kwako?” akamuuliza. Sauti yake ilikuwa tulivu lakini ilikuwa ya hasira.
“Afande nimepata taarifa za mauaji sasa hivi kutoka
kwa OCD wa Kinondoni” Sauti ya afisa upelelezi ilisikikika kutoka simu ya
upande wa pili.
“Ulikuwa unasubiri nikupigie
ndio uniarifu?”
“Hapana afande, taarifa
yenyewe nimeipata muda huu”
“Ni mauaji ya nani?”
“Nimeelezwa kwamba ni ya
msichana mwenye umri wa miaka ishirini na tisa anayeitwa Pili, mkazi wa Kinondoni
na ni mpishi wa Waziri mkuu”
“Aliuawa saa ngapi, aliuawa
na nani na tukio lilitokea wapi?”
“Nimeelezwa kwamba aliuawa
mahali pasipojulikana lakini maiti yake ilikwenda kuachwa katika kiwanja cha
shule ya Msingi ya Kinondoni saa nane usiku”
“Ameuawa kwa kitu gani?”
“Taarifa ya uchunguzi wa
mwili wa marehemu imeonesha kuwa marehemu alifyonzwa damu kupitia mshipa wake
wa shingo na kusababisha kifo chake”
“Mh! Alifyonzwa na nani?”
“Uchunguzi umeonesha kuwa
amefyonzwa na binaadamu lakini hajajulikana ni nani, kwa hiyo polisi ndio
wanaendelea na uchunguzi”
“Ni nani ambaye aliuoana
mwili wa marehemu ulipoachwa hapo kiwanjani?”
“Ni mlinzi wa ile shule”
“Ninahitaji kupata taarifa
kamili”
“Ninakuja nayo ofisini kwako
afande”
“Niletee
sasa hivi”
Baada ya robo saa hivi, afisa upelelezi
akaingia ofisini mwa kamanda wa polisi akiwa ameshika jalada.
Aliketi kwenye kiti kisha akampa jalada hilo
kamanda wa polisi.
“Taarifa kamili niliyoletewa
imo humu, unaweza kuisoma” Afisa upelelezi huyo akamwambia kamanda
wa polisi.
Kamanda alipolitwaa jalada hilo alilifungua na
kulisoma. Zilimchukua dakika kumi hivi kuyapitia maelezo yote haraka haraka.
Akauinua uso wake na kumtazama Afisa upelelezi.
“Hilo gari mtalipataje?”
“Tatizo ni kuwa magari aina
ya Toyota
Land Cruisser ya rangi nyeupe ni mengi
hapa Dar, ni afadhali kama yule mlinzi angeona
namba zake za usajili.
Tungeweza kulipata kwa urahisi”
“Unadhani ni akina nani
watakuwa wamefanya unyama huu?”
“Ni mapema mno kudhani,
upelelezi wetu ndio utatoa jibu. Tukio kama hili ndio mara ya kwanza kutokea
hapa Dar”
“Sasa ni lazima vijana wako
wachunguze kujua huyu msichana jana alitoka kazini saa ngapi na alipotoka
kazini alikwenda wapi. Kama alirudi nyumbani
kwake, alitoka tena saa ngapi na alikwenda wapi. Vile vile ni muhimu kujua kwa
mara ya mwisho alikuwa na nani”
“Sawa afande,
nitalishughulikia hilo
suala”
Afisa upelelezi akainuka
kwenye kiti na kutoka.
Alipotoka tu, kamanda wa polisi akainua simu na kumpigia Waziri wa
Mambo ya ndani.
Baada ya kumueleza tukio
zima, waziri alimuuliza.
“Ni uchunguzi gani ambao
umefanyika hadi sasa?”
“Kitu cha kwanza kilikuwa ni
kupata taarifa ya uchunguzi wa mwili wa marehemu. Hatua ya pili ilikuwa ni
kuwapata jamaa wa marehemu ambao pia hawakuwa na taarifa yotote.
“Hatua ya tatu itakuwa kutuma
vijana kwenda nyumbani kwa mheshimiwa Waziri Mkuu kujua marehemu aliondoka kazini saa ngapi
jana na pia kwenda nyumbani kwake kujua kama alirudi nyumbani alipotoka kazini
na kama alirudi aliondoka saa ngapi na
alikwenda wapi”
“Ninachowaomba ni kwamba
chochote ambacho mtagundua mnifahamishe haraka” Waziri akamwambia kamanda huyo wa polisi.
“Tutakufahamisha”
“Sawa”
Waziri alitangulia kukata
simu kabla ya kamanda wa polisi.aliyekuwa
amempigia.
Haikutimia hata dakika moja
Mkuu wa Jeshi la Polisi akampigia kamanda wa polisi kumuulizia kuhusu tukio hilo.
“Ni kweli tukio hilo limetokea, polisi
wanaendelea na uchunguzi” Kamanda huyo alimjibu.
“Uchunguzi huo umefikia
wapi?”
“Kwa sasa hivi sina maelezo
ya kutosha lakini mpaka saa kumi jioni nitakuwa na taarifa kamili’
“Utanijulisha”
“Sawa afande”
Mkuu wa Jeshi la polisi
akakata simu na kamanda wa polisi akaurudisha
mkono wa simu mahali pake.
Waziri Mkuu alirudi nyumbani
kwake saa saba mchana. Alimkuta mke wake akiwa na fadhaa.
“Karibu” Mwanamke huyo
alimkaribishaWaziri Mkuu huyo sebuleni. Sauti yake haikuwa na uchangamfu wa
kawaida.
Dastan Lazaro aliketi kwenye kochi. Kama
kawaida yake aliuweka mguu mmoja juu ya mwingine akamtazama mke wake.
Vicky alipoona mume wake
anamtazama akamuuliza.
“Je?”
“Nimekuwa nikijiuliza swali
lakini sipati jibu, Sofia
amepatwa na tatizo gani?” Waziri Mkuu akamuuliza mke wake.
“Si rahisi kujua. Kama vipimo vya hospitali vinasema ni mzima, sisi
tutawezaje kujua kilichompata”
“Mimi kwanza nilidhani ni malaria
imempanda kichwani lakini malaria yenyewe haikuonekana”
“Mimi nimeogopa sana yule polisi
niliyezungumza naye kwenye simu aliponiambia sababu ya kifo cha Pili ni
kufyonzwa damu. Ina maana Sofia
alimfyonza damu nyingi”
“Halafu ile nguvu ya
kumdhibiti yule mwanamke aliipata wapi. Ukiwatazama Pili na Sofia, Pili ana
nguvu zaidi. Alimzidi vipi mpaka akaweza kumfyonza damu na kumuua?”
“Kisha
unajua kuwa mpaka muda huu Sofia
hajui alichotenda. Ina maana kwamba jana usiku alikuwa amerukwa na akili!”
“Inabidi tuendelee kumfanyia
uhunguzi zaidi wa akili yake…”
Waziri Mkuu akakatizwa na
mlio wa simu yake ya mkononi iliyokuwa kwenye mfuko wa koti lake. Hakuwa na
tabia ya kutoa simu kwa haraka inapoita lakini siku ile aliitoa haraka ili
kujua ni nani aliyekuwa akimpigia.
Akaona jina la waziri wa
Mambo ya Ndani Jackson Maro.
Akapokea simu.
“Hello Maro…!”
“Mheshimiwa nilitaka
kukufahamisha kuwa uchunguzi wa mauaji
ya mpishi wa nyumbani kwako Pili Amrani
unaendelea. Nimearifiwa kuwa polisi wanataka kuja nyumbni kwako kuchukua
maelezo”
ITAENDELEA kesho usikose uhondo huu hapahapa tangakumekuchablog, KUMEKUCHA UPYA
No comments:
Post a Comment