HADITHI
MBIO ZA SAKAFUNI HUISHIA
UKINGONI 4
ILIPOISHIA
Waziri alijiambia hatua aliyochukua ambayo aliiona ilikuwa ya
maana ya kuutupa mwili huo mahali hapo, ilikuwa ya kipumbavu. Hakuwa amefanya
uchunguzi sahihi na kugundua kuwa mahali hapo palikuwa salama.
Wazo la kuwa eneo hilo litakuwa na mlinzi
halikuwemo katika akili yake.
Waziri alijuta. Alijiambia
siku ya kuumbuka na kukatwa katwa mapanga ndiyo ile.
Wakati mlinzi akiendelea
kumfuata kwa mwendo wa haraka akiwa ameipunga sime yake, waziri alimrushia ule
mwili ukaanguka karibu yake
kwa kishindo.
Mlinzi akasita na kukitazama
kitu kilichokuwa kimetupwa mbele yake. Alipourudisha uso wake kwa waziri, waziri
hakuwepo.
Alikuwa ametimua mbio
kuelekea kwenye gari lake. Kwa vile mlango aliuacha wazi alikaa kwenye siti
haraka. Alishukuru kwamba gari hakuwa amelizima moto. Akatia gea ya kwanza na kuliondoa.
Mlinzi alikuwa kikimbia
kulifuata gari hilo.
“Simama wewe, umetupa nini
pale?” Mlinzi huyo alimwambia waziri akiwa ametinga mbele ya gari hilo.
SASA ENDELEA
Waziri alimkwepa. Ilibaki kidogo tu angemgonga. Mlinzi mwenyewe pia aliruka
kando kulikwepa gari hilo. Gari likampita na kutokea barabarani.
Waziri aliposhika barabara
alikanyaga mafuta. Gari lilikimbia kwa kasi!
Mlinzi alikuwa ametaharuki
baada ya kukoswa kuswa na gari la waziri. Alikuwa amesimama
akilitazama gari hilo
likikata mbuga!
Hakuweza kujua gari hilo lilikuwa likiendeshwa
na nani na kile kiu alichorushiwa kilikuwa kitu gani. Akarudi sasa kiukiangalia
vizuri.
Aliumwilika tochi mwili wa
Pili. Mlinzi akashituka
alipogundua kuwa ni mtu tena wa jinsia ya kike. Aligeuza tena uso akatazama
upande ule lilikoelekea gari la waziri kisha
akachutama na kuutazama vizuri mwili huo.
Kwanza alihisi mwanamke huyo alikuwa amelewa chakari kiasi
kwamba hakuwa akijiweza lakini akajiuliza aliyelewa hapumui na macho yake
hayapepesi?
Akaguna kisha akanyanyuka. Akaanza kutimua mbio
kuelekea kituo kidogo cha polisi kilichokuwa jirani na pale. Alipofika
aliwakuta polisi wawili waliokuwa wakisinzia. Akawaamsha.
“Kitu gani?” Polisi mmoja akamuuliza kwa kutaharuki baada ya kuamshwa
usingizini.
“Mimi ni mlinzi wa ile shule
ya msingi pale. Kuna mtu alikuja na gari akatupa mtu tena mwanamke…” Mlinzi
huyo aliwambia.
“Hebu tueleze vizuri, ni mtu
gani aliyetupwa hapo?” Polisi mmoja
akamuuliza.
“Sijui. Hebu twendeni
mkamuone”
“Huyo mtu yuko katika hali
gani?”
“Sijui amekufa…sijui ni
mzima…kwa maana hapumui!”
“Ni mwanamme au mwanamke?”
“Ni mwanamke”
Polisi mmoja akamwambia mwenzake afuatane na yule mlinzi
akamuone huyo mtu.
Polisi na mlinzi huyo walipofika mahali hapo, mlinzi
aliumulika tochi mwili wa Pili.
Polisi huyo baada ya kuutazama mwili huo alisema.
“Sijui amepigwa au amebakwa.
Kwenye shingo yake kuna damu”
“Unaona tairi za gari lenyewe
hizi hapa” Mlinzi alimwambia polisi huyo huku akizimulika alama za tairi za
gari la waziri zilizokuwa kwenye michanga.
“Lilitokea upande gani?”
“Lilitokea upande huu, mimi
nilikuwa nimekaa pale ninaangalia tu. Gari hilo lilipofika hapa ndipo mtu mmoja
akashuka, nikaona anatoa kitu. Mimi nikaja haraka. Aliponiona akanitupia huu
mwili na kukimbia kwenye gari…”
“Walikuwa watu wangapi?”
“Mimi niliona mtu mmoja tu
labda wenzake walikuwa kwenye gari”
“Ina maana walikuja kuutupa
huu mwili?”
“Labda”
Polisi huyo akatoa simu ya mkononi na kumpigia mwenzake
aliyemuacha kituoni.
“Aisee kuna mtu hapa…sijui
ameuawa au amezimia…ametupwa katika uwanja wa shule” Polisi
huyo alimwambia mwenzake alipopokea simu.
“Anaonekanaje…amepigwa au…?”
Sauti ya mwenzake ilisikika ikiuliza.
“Katika shingo yake kuna damu
iliyoganda…sasa sijui amenyongwa shingo au vipi…!”
“Ni mwanamke au mwanaume?”
“Ni mwanamke. Inawezekana
walimbaka kwanza ndio wakaamua kuja kumtupa hapa”
“Sasa kata simu niwapigie
polisi wa kituo kikuu walete gari”
“Sawa”
Polisi huyo akakata simu.
Polisi aliyekuwa kituoni akawapigia simu polisi wa kituo
cha Kinondoni.
“Nini kimetokea hapo?”
Inspekta Alex aliyekuwa katika zamu ya usiku kiuoni hapo alimuuliza.
“Kuna tukio limetokea sasa
hivi. Mlinzi wa shule ya msingi ya Kinondoni ametuletea taarifa kwamba kuna
mwanamke ametupwa karibu na eneo la shule”
“Nyinyi mmefika kumuona?”
“Aliyekwenda ni constebo
Faustus na amenipigia smu”
“Amesemaje?’
“Amemuona huyo mwanamke na
hana uhakika kwamba ameuawa au yuko hai”
“Hao waliomtupa ni kina
nani?”
“Ni watu waliofika na gari.
Walimshusha wakamtupa na kukimbia na gari”
“Kuna watu walioliona hilo gari?”
“Mlinzi aliliona”
“Sawa. Subiri tunakuja”
Waziri Mkuu alipofika
nyumbani kwake aliliingiza gari ndani ya geti akaliegesha katika banda la
kuegesha magari. Alipolizima gari aligundua kuwa alikuwa akihema kama aliyekuwa akikimbia kwa miguu.
ITAENDELEA usikose kwani KUMEKUCHA UMPYA
No comments:
Post a Comment